View attachment 2060577
Papa Francis akiwa mimbari
I. Utangulizi
Ndani ya miaka 2020 iliyopita ya Ukristo, Mkutano Mkuu Kabisa wa 21 ndani ya Kanisa Katoliki, kama ambavyo huwa tunaongelea Anual General Meeting (AGM) ya Kampuni au azaki, ulijulikana kama Mtaguso wa Pili wa Vatican, na ulifanyika tangu mwaka 1962 hadi 1965.
Mkutano huu ndio ulianzisha utaratibu wa Kanisa zima kukutana kwa njia ya Sinodi za Kiaskofu katika ngazi ya Kanda, Bara na hata Dunia nzima kwa ajili ya mashauriano juu ya masuala muhimu ya Kikanisa.
Tayari zimefanyika sinodi 15 tangu 1965. Na sasa Sinodi ya 16 ya Maaskofu Katoliki Duniani inaendelea tangu ilipozinduliwa na Papa Francis tangu 10 Oktoba 2021 huko Roma.
Sinodi ya 16, itakayofanyika kwa miaka mitatu mfululizo, tangu 2021 hadi 2023, inanogeshwa na kauli mbiu isemaayo “Kwa Ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume.”
Sinodi hii itahitimishwa Oktoba 2023 huko huko Roma, baada ya Papa kupokea maoni ya walei na makleri kutoka duniani kote kupitia dodoso maalum kwa ajili hii.
Katika historia ya Kanisa, hii ni sinodi ya kwanza ya Kiaskofu duniani inayoanza kwa kukusanya maoni ya waumini walei kwa njia ya dodoso.
Kwa mujibu wa Mwongozo wa Vatican, swali la msingi katika dodoso hili ni hili:
Katika kutangaza Injili, kwa njia ya Kanisa la Sinodi, waumini “husafari pamoja.” Je, huku “kusafiri pamoja” kunafanyikaje leo katika Kanisa lako mahalia? Na je, ni hatua gani ambazo Roho Mtakatifu anatualika kuchukua ili tuweze “kusafiri pamoja” na kukua wakati wa “kusafiri pamoja”?
Kwa ajili ya urahisi wa kukusanya maoni ya waumini, swali hili linagawanyika katika maswali madogo 50 yanayogawanyika kwenye sehemu kumi zifuatazo:
- Sinodi kama safari ya Pamoja,
- Utamaduni wa kusikiliza,
- Utamaduni wa kuzungumza,
- Kuadhimisha Ekaristi,
- Kuwajibika kwa pamoja katika utume,
- Mazungumzo katika kanisa na jamii,
- Kushirikiana na madhehebu mengine ya Kikristo,
- Mamlaka na ushiriki,
- Kutambua na kuamua, na
- Kujiunda katika sinodi.
II. Maswali kuhusu Sinodi kama safari ya Pamoja
Ikizingatiwa kwamba, katika Kanisa na katika jamii, tuko bega kwa bega katika safari ile ile:
1. Katika Kanisa lako mahalia, ni akina nani “wanaosafiri pamoja”?
2. Tunaposema: “Kanisa letu,” ni nani aliye sehemu yake?
3. Ni nani anayetuuliza tusafiri pamoja?
4. Watu tunaoandamana kwa pamoja barabara ni akina nani?
5. Je Watu tunaoandamana kwa pamoja wanahusisha wale walio nje ya mipaka ya kanisa?
6. Ni watu au makundi gani yameachwa pembeni, kwa uwazi au kwa hakika?
III. Maswali kuhusu Utamduni wa kusikiliza
Kwa kuzingatia kwamba, kusikiliza ni hatua ya kwanza, lakini inahitaji kuwa na akili na moyo wazi, bila chuki:
7. Je, Kanisa letu “linahitaji kumsikiliza nani”?
8. Je, Walei, hasa vijana na wanawake, wanasikilizwa vipi?
9. Je, tunaunganishaje mchango wa Wanaume na Wanawake Waliowekwa wakfu?
10. Je, kuna nafasi gani kwa sauti ya walio wachache, waliotupwa na waliotengwa?
11. Je, tunatambua chuki na fikra potofu zinazozuia usikilizaji wetu?
12. Je, tunayasikilizaje mazingira ya kijamii na kitamaduni yanayotuzunguka?
IV. Maswali kuhusu Utamaduni wa kuzungumza
Kwa kuzingatia kwamba, wote wanaalikwa kuzungumza kwa ujasiri na kwa kuunganisha uhuru, ukweli, na upendo:
13. Tunakuzaje mtindo huru na wa kweli wa mawasiliano ndani ya jumuiya na mashirika yake, bila undumilakuwili na ukinyonga?
14. Tunakuzaje mtindo huru na wa kweli wa mawasiliano katika jamii ambayo sisi ni sehemu yake?
15. Ni lini na jinsi gani tunaweza kusema yaliyo muhimu kwetu?
16. Je, uhusiano na mfumo wa vyombo vya habari (sio vyombo vya habari vya Kikatoliki pekee) hufanya kazi vipi?
17. Ni nani wanaozungumza kwa niaba ya jumuiya ya Kikristo, na wanachaguliwa jinsi gani?
V. Maswali kuhusu Kuadhimisha Ekaristi
Kwa kuzingatia kwamba, "kusafiri pamoja" kunawezekana tu ikiwa kunategemea kusikiliza Neno la jumuiya na adhimisho la Ekaristi:
18. Je, sala na maadhimisho ya kiliturujia hututia moyo na kuelekezaje “kusafiri pamoja”?
19. Je, sala na maadhimisho ya kiliturujia yanahimizaje maamuzi muhimu Zaidi miongoniwetu?
20. Je, tunakuzaje ushiriki hai wa Waamini wote katika liturujia na utendaji wa kazi ya kutakatifuza ulimwengu?
21. Je, ni nafasi gani zinatolewa kwa ajili ya watoa huduma za usomaji wa masomo Kanisani?
VI. Maswali kuhusu Kuwajibika kwa pamoja katika utume
Kwa kuzingatia kwamba, sinodi iko katika huduma ya utume wa Kanisa, ambapo washiriki wake wote wameitwa kushiriki, kwa vile sisi sote ni wanafunzi wa kimisionari:
22. Ni kwa jinsi gani kila mtu aliyebatizwa anaitwa kuwa mhusika mkuu katika utume?
23. Je, jumuiya inaunga mkono vipi wanachama wake waliojitolea kutumikia katika jamii (jitihada za kijamii na kisiasa, katika utafiti na mafundisho ya kisayansi, katika kukuza haki ya kijamii, katika ulinzi wa haki za binadamu, na katika kutunza Nyumba ya Pamoja, n.k.) ?
24. Je, unawasaidiaje kuishi ahadi hizi katika mantiki ya utume?
25. Je, utambuzi kuhusu maamuzi yanayohusiana na utume hufanywaje, na ni nani anayeshiriki katika hilo?
26. Ni kwa jinsi gani mapokeo mbalimbali yanayounda urithi wa Makanisa mengi, hasa yale ya Mashariki, yanaunganishwa na kurekebishwa, kuhusiana na mtindo wa sinodi, kwa mtazamo wa ushuhuda mzuri wa Kikristo?
27. Je, ushirikiano hufanyaje kazi katika maeneo ambako Makanisa tofauti yapo?
VII. Maswali kuhusu Mazungumzo katika kanisa na jamii
Kwa kuzingatia kwamba, mazungumzo ni njia ya ustahimilivu inayojumuisha pia ukimya na mateso, lakini yenye uwezo wa kukusanya mang’amuzi ya watu na watu:
28. Je, ni maeneo gani na njia gani za mazungumzo ndani ya Kanisa letu mahalia?
29. Je, tofauti za maono, migogoro na matatizo yanatatuliwa vipi?
30. Je, tunakuzaje ushirikiano na Dayosisi jirani, pamoja na miongoni mwa jumuiya za kidini katika eneo hili, pamoja na miongoni mwa vyama na mienendo ya walei, n.k.?
31. Je, ni uzoefu gani wa mazungumzo na ahadi ya pamoja tuliyo nayo na waumini wa dini nyingine na wasioamini?
32. Je, Kanisa linajadiliana vipi na kujifunza kutoka sekta nyingine za jamii: ulimwengu wa siasa, uchumi, utamaduni, jumuiya za kiraia, maskini?
VIII. Maswali kuhusu Kushirikiana na madhehebu mengine ya Kikristo
Kwa kuzingatia kwamba, mazungumzo kati ya Wakristo wa maungamo mbalimbali, yaliyounganishwa na Ubatizo mmoja, yana nafasi ya pekee katika safari ya sinodi:
33. Tuna uhusiano gani na ndugu na dada wa madhehebu mengine ya Kikristo?
34. Je, ndugu na dada wa madhehebu mengine ya Kikristo wanahusika na maeneo gani?
35. Tumepata matunda gani kutokana na ‘kusafiri pamoja’ na ndugu na dada wa madhehebu mengine ya Kikristo?
36. Kuna matatizo gani kutokana na ‘kusafiri pamoja’ na ndugu na dada wa madhehebu mengine ya Kikristo?
IX. Maswali kuhusu Mamlaka na ushiriki
Kwa kuzingatia kwamba, Kanisa la Sinodi ni Kanisa shirikishi na linalowajibika pamoja:
37. Tunatambuaje malengo ya kufuatwa, njia ya kuyatimiza, na hatua zinazopaswa kuchukuliwa?
38. Je, mamlaka yanatekelezwaje ndani ya Kanisa letu mahalia?
39. Je, ni kazi gani hufanyika kwa njia ya uwajibikaji wa Pamoja ndani ya kaniza mahalia?
40. Je, huduma za walei na utekelezaji wa wajibu kwa Waamini walei hukuzwaje?
41. Je, vyombo vya sinodi hufanya kazi vipi katika ngazi ya Kanisa mahalia?
42. Je, vyombo vya sinodi ambavyo hufanya kazi katika ngazi ya Kanisa mahalia vinatoa ushuhuda wenye manufaa?
X. Maswali kuhusu Kutambua na kuamua
Kwa kuzingatia kwamba, kwa mtindo wa sinodi, maamuzi hufanywa kwa njia ya utambuzi, kulingana na maafikiano yanayotokana na utii wa kawaida kwa Roho:
43. Je, kwa taratibu na mbinu gani tunatambua pamoja na kufanya maamuzi?
44. Je, taratibu hizo za kufanya maamuzi zinaweza kuboreshwaje?
45. Je, tunakuzaje ushiriki mpana katika kufanya maamuzi ndani ya jumuiya zenye uongozi ulio na muundo wa hierakia?
46. Je, tunaelezaje uhalali wa mfumo wa maamuzi ndani nya Kanisa unaotenganisha awamu ya walei kutoa ushauri kwa makleri na awamu ya makleri kufanya maamuzi?
47. Je, ni kwa jinsi gani na kwa zana zipi tunakuza uwazi na uwajibikaji katika mfumo wa maamuzi ndani nya Kanisa unaotenganisha awamu ya walei kutoa ushauri kwa makleri na awamu ya makleri kufanya maamuzi?
XI. Maswali kuhusu Kujiunda katika sinodi
Kwa kuzingatia kwamba, hali ya kiroho ya kusafiri pamoja inaitwa kuwa kanuni ya kielimu kwa ajili ya malezi ya utu wa kibinadamu na ya Mkristo, ya familia na jumuiya:
48. Je, tunaundaje watu, hasa wale wanaoshikilia majukumu ndani ya jumuiya ya Kikristo, ili kuwafanya wawe na uwezo zaidi wa “kusafiri pamoja,” kusikilizana na kushiriki katika mazungumzo?
49. Je, ni malezi gani tunayotoa kwa ajili ya utambuzi na utumiaji wa mamlaka?
50. Ni zana gani hutusaidia kusoma mienendo ya utamaduni ambamo tumezama na athari zake kwa mtindo wetu wa Kanisa?
XII. Tafakari yangu
Napenda sasa kufanya tafakari ya jumla kuhusu swali kuu la sinodi ya 16 ya Maaskofu, itakayohitimishwa mwaka 2023.
Uhai wa Kanisa la Kisinodi unategemea uwepo wa safari ya pamoja, safari ya pamoja inamaanisha uwepo wa Umoja wa Kikanisa, na Kanisa ni jumuiya ya watu wengi.
Kama ambavyo umoja wa vitu viwili hutegemea uwepo wa kitu cha tatu kinachoviunganisha vitu hivyo viwili, umoja wa kitu chenye sehemu nyingi (the unity of a compound thing) hutegemea uwepo wa kitu cha ziada, mbali na sehemu hizo, ambacho kinaziunganisha sehemu hizo pamoja hadi kuitwa kitu kimoja.
Kadiri kanisa linavyohusika, kitu kinachowaunganisha wanakanisa ni imani ambayo huweka msingi wa matendo na matumaini ya pamoja (credenda, agenda and speranda).
Kwa hiyo, pasipo "imani ya pamoja" hakuna "safari ya pamoja", na bila safari ya pamoja hakuna "Kanisa la Kisinodi."
Kama hivyo ndivyo, "imani ya pamoja" ndani ya Kanisa Katoliki, yaani imani yenye kulifanya Kanisa hili lijihesabu na kuhesabiwa kama kitu kimoja, hasa ni kitu gani na sio kitu gani?
Hapa napendekeza kwamba, imani ya kidini, kama vile imani ya Kanisa Katoliki, ni itikadi mojawapo kati ya itikadi nyingi zilizopo ulimwenguni.
James W. Sire (2009) ameandika toleo la tano la kitabu kiitwacho, "The Universe Next Door: The Worldview Catalogue," kilichochapishwa kupitia kampuni ya "InterVarsity Press," huko Marekani.
Natafsiri jina la kitabu hiki kama "Kuna Itikadi Tofauti Mlango wa Pili: Katalogi ya Itikadi za Duniani."
Sire (2009) ameorodhesha itikadi kama vile Theism, Deism, Naturalism, Nihilism, Existentialism, Pantheism, Postmodernism, na kuendelea.
Baada ya kuorodhesha itikadi hizi, anasema kuwa zote zinafanana katika jambo moja kuu, kwani, kila moja ni "itikadi (worldview)" ya namna yake. Yaani, Sire (2009) anasema kwamba:
"A worldview is a commitment, a fundamental orientation of the heart, that can be expressed as a story or in a set of presuppositions (assumptions which may be true, partially true or entirely false) that we hold (consciously or subconsciously, consistently or inconsistently) about the basic constitution of reality, and that provides the foundation on which we live and move and have our being." (uk.20).
Anachosema Sire (2009) kuhusu itikadi kinaweza kunyumbulishwa kwa kusema kwamba:
"A worldview is a set of beliefs about basic anatomy of reality that influence one's perceptions, thoughts and behaviours."
Kwa uchache, imani ya mtu kuhusu "anatomia ya msingi ya uhalisia" ni kama mti wenye matawi yafuatayo: metaphysics, epistemology, cosmology, teleology, theology, anthropology, axiology, deontology, praxiology, ecology, economy, sociology, politology, etiology, sexology, biology, psychology, matrimoniology, ethicology.
Hivyo, napendekekeza kuwa Imani Katoliki, kama ambavyo inapatikana kwenye Kanuni ya Imani ya Nikea, Kanuni ya Imani ya Constnatinopole, Kanuni ya Imani ya Mtakatifu Athanazi, na kwenye Kanuni ya Imani ya Mitume, ni aina mojawapo ya itikadi zinazokubaliana na fasili ya Sire (2009:20).
Lakini hapa nataka kuongeza kwamba, itikadi zote zilizotajwa na Sire (2009) zinatofautiana katika namna zinavyofafanua kile ambacho Sire (2009) amekitaja kama "basic constitution of reality," yaani imani kuhusu "anatomia ya msingi ya uhalisia wa mambo."
Tofauti hizi zinaweza kuonekana kwa kutumia mfano wa mche pembetatu (prizimu), miale ya mwanga wa uhalisia inayotua kwenye upande mmoja wa prizimu, na miale ya mwanga wa uhalisia inayopita na kuchomoza kwenye upande wa pili wa prizimu.
Mwanga wa kawaida ukipitishwa kwenye prizimu huzalisha safu nane za rangi zifuatazo: Red, Orange, Yellow, Green, Bluee, Indigo, na Violet (ROYGBIV).
Vivyo hivyo, mwanga wa uhalisia ukipenya kwenye prizimu ya itikadi yoyote, utazalisha miale ifuatayo ya kiimani: metaphysics, epistemology, cosmology, teleology, theology, anthropology, axiology, deontology, praxiology, ecology, economy, sociology, politology, etiology, sexology, biology, psychology, matrimoniology, ethicology.
Kwa mfano, mwanga wa uhalisia ukipitishwa kwenye "prizimu ya itikadi katoliki" utazalisha miale ifuatayo: mwale wa "theology" wenye kuonyesha kwamba "mungu yupo"; mwale wa "deontology" wenye kuonyesha kuwa "hakuna mtu mwenye haki ya kuzuia mimba"; mwale wa "politology" wenye kuonyesha kuwa "kazi ya serikali ni kusimamia maslahi ya pamoja katika Taifa"; mwale wa "matrimoniology" wenye kuonyesha kwamba kila ndoa inajumuisha tunu mbili pekee za umoja na uzazi; na orodha inaendelea.
Lakini, kwa kiasi fulani, mwanga wa uhalisia ukipitishwa kwenye "prizimu ya itikadi ulutheri" utazalisha miale iliyo tofauti na miale inayozalishwa kupitia "prizimu ya itikadi katoliki."
Kwa hiyo, uwepo wa "Kanisa la Kisinodi" unatokana na "safari ya pamoja" kwa mujibu wa "imani ya pamoja," imani ambayo hapa nimeiita "itikadi ya pamoja." Walioko nje ya barabara inayotumiwa na waumini wanaotembea kama "Kanisa la Kisinodi" wanayo itikadi tofauti.
Ni katika mazingira haya ya kiitikadi, dodoso la Sinodi ya 16 ya Maaskofu linauliza: "Ni hatua gani ambazo Roho Mtakatifu anatualika kuchukua ili tuweze 'kusafiri pamoja' na kukua wakati wa 'kusafiri pamoja' ”?
Ni kwa sababu ya kufafanua mambo haya, Robert Wuthnow (1993), ameandika kitabu kiitwacho Christianity in the Twenty-first Century: Reflections on the Challenges Ahead (New York: Oxford Universit y Press, 1993).
Katika kitabu hiki, Wuthnow (1993) amejadili Changamoto Zinazolikabili Kanisa Katika Karne ya Ishirini na Moja, kwa kuzigawanya katika makundi makubwa yafuatayo: changamoto za kitaasisi, kimaadili, kiimani, kisiasa, na kiutamaduni.
Hapo juu nimejaribu kupanua wigo wa matatizo anayoyajadili Wuthnow (1993) ili kuonyesha kwa mpigo matawi yote ya changamoto husika.
Kwa ujumla, kuna mageuzi makubwa inabidi kufanyika ili kukamilisha ndoto ya Papa Francis aliyeanzisha mchakato huu.
XIII. Hitimisho
Papa Francis ameanzisha utafiti mkubwa. Na kama majawabu yatakayokusanywa yatafanyiwa kazi, yanaweza kuleta mabadiliko makubwa ndani ya Kanisa Katoliki kutokana na msukumo ulioanzia ndani ya Kanisa lenyewe.
Matengenezo makubwa kwa kiwango hiki yamewahi kufanyika mara mbili.
Katika karne ya 16 yalifanyika kutokana na shinikizo la Mtawa aliyeitwa Martin Luther wa Ujerumani, aliyeorodhesha dosari 95 na kulialika Kanisa kuzijadili na kuzitolewa majibu. Matokeo yalikuwa ni kuanzishwa kwa Kanisa Jipya la Walutheri.
Na mwaka 1962-65 pia kulifanyika matengenezo makubwa ndani ya Kanisa Katoliki kupitia Mtaguso wa pili wa Vatican.
Dhana ya Kanisa la Kisinodi ilianzia kwenye mtaguso huu. Lakini, Papa Yohanne Paul II na Papa Benedicto XVI hawakuiendeleza. Badala yake, walitunga sheria na kanuni za Kanisa zinazofifisha dhana hii kabisa.
Sasa amekuja Papa Francis ambaye ni muumini wa dhana hii. Anafanya matengenezo kwa ajili ya kurejesha ndoto ya Mtaguso II wa Vatican kuhusu Kanisa la Kisinodi.
Kwa ajili ya kufanikisha azima yake atalazimika kufumua na kufuma upya sheria na kanuni nyingi za Kanisa Katoliki zilizotungwa tangu mwaka 1983. Miaka mitatu ijayo ndipo tutaujua ukweli.
Lakini, kwa mujibu wa dodoso hili, Papa Francis anapanga mageuzi makubwa sana.
Hivyo, yafaa aongezewe ulinzi dhidi ya Wahafidhina ndani ya Kanisa. Vinginevyo, yanaweza kumkuta yale yaliyomsibu Papa Paul I (Albino Luciani), aliyekalia kiti cha Upapa kwa siku 33 pekee.
Mara tu baada ya kuteuliwa kwake, alikuwa ameweka “Mpango wa Sera Sita” kwa ajili ya Mageuzi ndani ya Kanisa.
Mambo hayo yalikuwa ni:
- Kufanya mageuzi ndani ya Kanisa kwa mujibu wa sera zilizopitishwa na Mtaguso wa II wa Vatican;
- Kurekebisha sheria za Kanisa;
- Kulikumbusha Kanisa kuhusu wajibu wake wa kuhubiri Enjili;
- Kupigania umoja wa Kanisa bila kumomonyoa mafundisho ya Kanisa;
- Kukuza majadiliano; na
- Kuhami amani ya dunia na haki ya kijamii.
Hakupata nafasi ya kutekeleza program hii. Kwani, alikalia kiti cha Upapa tarehe 26 Agosti 1978 na kufa siku 33 baadaye.