Hebu soma na hii habari! Nadhani utaelewa kwa undani zaidi
Juma Kasesa (Tanzania Daima)
RAIS Jakaya Kikwete amenusurika kupata ajali baada ya gari alilokuwa amepanda kulegea gurudumu na kisha kung'oka muda mfupi baada ya yeye mwenyewe kuteremka katika gari hilo kwa dharura wakati akiwa ziarani jijini Dar es Salaam.
Tukio hilo lilitokea jana majira ya saa 9:15 katika Barabara ya Kilwa maeneo ya karibu na zilipo ofisi za makao makuu ya kampuni ya mafuta ya BP.
Kabla ya tukio hilo, msafara wa Rais Kikwete ulisimama ghafla na rais akahamishwa kutoka katika gari hilo aina ya Land Cruiser VX na kwenda katika gari jingine.
Watu walioshuhudia tukio hilo walilieleza Tanzania Daima kuwa, muda mfupi baada ya msafara wa rais kuendelea na safari, dereva wa gari alilohama rais alijaribu kulisogeza pembeni ya barabara, hatua iliyosababisha gurudumu la gari hilo kung'oka na kusababisha ligote chini upande wa mbele kulia.
Tukio hilo liliwashtua watu waliokuwa katika eneo hilo, ambao walianza kujadili ni nini kingetokea iwapo gurudumu hilo lingeng'oka wakati rais akiwa ndani ya gari hilo.
Mwandishi wa gazeti hili aliyekuwapo eneo la tukio alieleza hatua hiyo ilisababisha kuwasili katika eneo hilo kwa gari maalum la kubeba magari mabovu maarufu kwa jina la ‘breakdown'.
Tukio hilo la rais kulazimika kuhama kutoka katika gari alilokuwa amepanda lilikuwa ni la pili baada ya kufanya hivyo kwa mara ya kwanza akiwa katika maeneo ya Kimara Mavurunza.
Kikwete alikuwa katika ziara yake ya siku moja ya kutembelea miradi ya maji jijini Dar es Salaam.
Msafara huo ukiwa unaondoka Kimara ulisimama ghafla na kuzua taharuki kwa maofisa usalama na wananchi baada ya kuona Rais Kikwete akishushwa ndani ya gari alilokuwa amepanda na kuingia katika gari jingine baada kupata hitilafu huku mvua kubwa ikinyesha.
Tukio hilo la rais kushushwa katikati ya barabara ya Morogoro katika eneo hilo, lilichukua dakika nane na kusababisha msongamano wa magari kabla ya msafara huo kuruhusiwa kuendelea kuelekea Chang'ombe Toroli ambako alikuwa akienda kukagua mradi mwingine wa maji unaosimamiwa na mashirika ya maji Dar es Salaam.
Tanzania Daima ilipowasiliana na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Salvatory Rweyemamu, alikiri kutokea kwa matukio mawili tofauti yaliyosababisha rais alazimike kuhamishwa kutoka katika magari aliyokuwa amepanda.
"Ni kweli matukio hayo yalitokea, katika tukio la kwanza gari alilopanda lilipata hitilafu baada ya gea kugoma kubadilika wakati katika tukio la pili, gari alilopanda lilipata pancha," alisema Rweyemamu.
Alipoulizwa kuhusu taarifa za gari la pili kung'oka gurudumu hata kusababisha kuitwa kwa gari la kubeba magari mabovu, Rweyemamu alikanusha habari hizo na akasema hazikuwa sahihi.
"Ndugu yangu yaani ninyi mnaona taarifa za matatizo ya kawaida ya magari aliyopata rais ni muhimu kuliko adha za maji ambazo alikuwa akikagua katika Jiji la Dar es Salaam?" alihoji Rweyemamu.
Mwandishi wa habari hizi alimweleza Rweyemamu kuwa, gazeti hili liliona umuhimu wa suala hili kwa kuwa lilikuwa likigusa usalama wa kiongozi mkuu wa nchi moja kwa moja.
Jibu hilo lilisababisha Rweyemamu amuombe mwandishi afuatilie kuhusu ukweli wa taarifa hizo na ndipo baada ya muda usiozidi dakika 30 alipiga simu chumba cha habari na kulihakikishia Tanzania Daima kuwa hitilifu za magari alizokabiliana nazo Rais Kikwete zilikuwa ni za kawaida.
Akiwa katika ziara hiyo jana, Kikwete alishuhudia wananchi wakiwabana kwa malalamiko na wakati mwingine kuwazomea maofisa watendaji wa Shirikika la Maji Safi na Maji Taka Dar es Salaam na Pwani (DAWASCO) na Mamlaka ya Maji Safi jijini Dar es Salaam (DAWASA).
Kufuatia hali hiyo ya kuzomewa katika eneo la Kimara, Rais Kikwete na Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Prof. Mark Mwandosya kwa nyakati tofauti walilazimika kuingilia kati na kutoa ufafanuzi kwa wananchi waliokuwa wakiwabana kwa maswali maofisa hao wa Dawasa na Dawasco.
Ofisa Mtendaji wa Dawasco, Alex Kaaya na Archad Mutalemwa wa Dawasa walikumbana zahama hizo baada ya diwani wa kata hiyo kuanika kero ya upatikanaji wa maji inayowakabili kwa muda mrefu na hivyo kumlazimu Rais Kikwete kuwataka watoe majibu.
Ziara hiyo ilianzia kwa Kikwete kutembelea Makao Makuu ya Dawasco ambapo alipata fursa ya kupata maelezo ya utendaji wa mashirika hayo kuhusu kero ya upatikanaji maji jijini Dar es Salaam.
Akiwa hapo alielezwa na maofisa hao hatua zilizochokuliwa na mashirika hayo katika kuondoa kero hiyo kwa kuanzisha miradi wa uchimbaji visima, ikiwamo kuhakikisha wanavikarabati vyanzo vya maji vya Ruvu Chini na Ruvu Juu ili kuondoa tatizo hilo.
Kaaya alisema tatizo linalosababisha kero ya maji jijini ni uchakavu wa miundombinu, upotevu wa asilimia 50 ya maji, njiani na miundombinu iliyokuwapo sasa kutoendana na ongezeko la idadi ya watu.
Alisema miundombinu iliyopo ilijengwa mwaka 1976 na ilikuwa inatosheleza kwa wakati huo tofauti na sasa ambapo Dar es Salaam inakadiriwa kuwa na wakazi wanaofikia milioni saba.
Naye Mutalemwa akitoa ufumbuzi wa tatizo la maji jijini, alisema wanatarajia kuanzisha mradi wa uchimbaji visima Julai mwaka huu, na kubainisha kuwa wamejipanga ifikapo mwaka 2013 tatizo la maji liwe limekwisha jijini.
Aidha, akiwa hapo, Rais Kikwete alimnyanyua Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Bakari Kingobi na kumtaka aeleze kwa nini jiji linakabiliwa na uchafu, ambapo alizitupia mpira halmashauri kuwa ndizo zenye dhamana ya kuondoa uchafu na yeye hana mamlaka ya kuziagiza kusimamia.
Kauli hiyo ilionekana kumuudhi Rais Kikwete na kumuuliza Kingobi anataka apewe mamlaka gani ili aweze kuzisimamia halmashauri hizo na kumfanya mkurugenzi huyo kubakia kimya pasipo na majibu.
Katika hatua nyingine, Rais Kikwete aliagiza kujengwa kwa kiwango cha lami kwa barabara ya Mavurunza hadi Segerea ili kupunguza kero ya usafiri.
Baada ya ziara hiyo, Rais Kikwete alikutana na viongozi wa Jiji la Dar es Salaam katika Ukumbi wa Karimjee na kuwataka kusimamia ipasavyo majukumu waliyopewa.