Ni upotoshaji tu na ukanjanja wa kuwapiga noti watu wenye imani haba na kutoelewa mafundisho yaliyoandikwa kwenye Biblia.
Wajanja ndiyo hupita humo na kukunja noti kiulaini kabisa kupitia uposhaji unaofanywa na makanisa ya leo yanoyojiita ya kiroho.
KUNENA KWA LUGHA KULIANZAJE KIHISTORIA?
Ukisoma kwenye Biblia kunena kwa lugha kulitokea siku ya Pentekoste ( Yaani siku ya Hamsini baada ya Kupaa kwa Yesu).
Katika maandiko tunaona kuwa ujumbe wa neno la Mungu ulikuwa umepokelewa katika jamii moja lakini dhima ilikuwa ni ujumbe huu usambae Ulimwenguni kote. Yaani kwa mfano, tuchukulie kwamba ujumbe wa neno la Mungu ulifikia Tanzania ambapo lugha inayotumika kwa mawasiliano ni Kiswahili, lakini ujumbe wa neno la Mungu ulitakiwa ufike Djibout, Malawi, DRC, Ethiopia na kwingineko Ulimwenguni ambapo hata hawakijui Kiswahili.
KULITOKEAJE?
Kunena kwa lugha kulitokea kwa wale Mitume sio kwa kubadili na kuacha kutumia lugha zao za asili au walijifunza lugha za Mataifa waliyoenda kuhubiri, la hasha, bali walitumia lugha zao za asili lakini waliokuwa wakihubiriwa waliupata ujumbe kwa kuusikia kwa lugha zao wenyewe.
Yaani tukirejea katika huo mfano hapo juu, ni kwamba, wewe Petro Mtanzania ukiwa unazungumza Kiswahili chako sanifu kabisa lakini unawahubiria watu wa DRC na wao wanasikia ujumbe unaowapa kupitia lugha wanayoielewa wao mfano, Kilingala, au Kifaransa.
Kwahiyo ni kama leo hii baada ya kuja teknolojia Uhutubie pale UN lakini wawakilishi wa Oman wanakusikia unaongea Kiarabu kilichonyooka, au Ujumbe kutoka Rome unaona unagonga kile Kilatini chenyewe kabisa, au wajumbe kutoka Brazil wanaona unakibomoa kireno ipasavyo.
Na kwa njia hiyo ndivyo ujumbe wa neno la Mungu ukaweza kuenea Ulimwenguni kote na maandiko kuweza kutafsiriwa katika lugha mbalimbali kulingana na sehemu ujumbe wa neno la Mungu unapelekwa
UPOTOSHAJI WA MAKANISA YA LEO YANAYOJIITA YA KIROHO:
Viongozi wengi wa hayo Makanisa hawaijui dhana ya kunena kwa lugha kwa mapana yake, na kama wanafahamu basi wanatumia ujinga wa waamini wao kufanya upotoshaji wa Makusudi kwa Maslahi yao binafsi.
Ukienda kwenye Makanisa ya leo yanayojiita ya kiroho yamejaa upotoshaji juu ya dhana hii ya kunena kwa lugha kwa kukuta hao viongozi wa makanisa hayo wanaongea lugha ambazo hata waumini wao hawazielewi nini wakimaanisha au ujumbe gani unatolewa kupitia matamshi hayo.
Nachelea kusema usikute hata wao hawajui ni kitu gani wanaongea na wala hawajui hiyo lugha gani wanatamka.
NB: Kunena kwa lugha sio kama kupandisha mashetani na kuongea vitu visivyoeleweka, bali ni njia iliyowatukia Mitume katika zama hizo ili neno la Mungu liweze kufika mahali pote Ulimwenguni.
Kwa ulimwengu wa sasa sidhani kama hiki kitu bado ni applicable.