Baada ya mke wangu kujifungua mtoto wa pili ziwa moja likaanza kumuuma anaponyonyesha,
Tukaenda kwenye hospitali moja ya serikali,
Wakampima na kumpa dawa azitumie kwa siku 30 kisha turudi tena
Lakini kutokana na maumivu ilibidi mke wangu asitishe kumnyonyesha mtoto, maana pia lile ziwa lilianza kuvimba,
Tukarudi hospitali na kuwaeleza, tukawaambia pia kuwa ziwa lina uvimbe,
Doctor akamcheki tena, akatuuliza bado unanyonyesha? Tukamwambia hapana,
Akasema hiyo ni hali ya kawaida ikiwa utasitisha unyonyeshaji ghafla, akatufafanulia kuwa kuna tezi za maziwa zinaweza kuvimba kwa sababu mtoto hanyonyi, tukapewa dawa na tukaambiwa turudi tena baada ya kumaliza dawa,
Ziwa likazidi kuvimba, tukaenda hospitali binafsi, wakampima upya, wakakata kinyama kwenye ziwa la mke wangu kwa ajili ya vipimo,
Tukaambiwa turudi baada ya wiki mbili,
Tuliporudi tukaambiwa mke wangu ana saratani ya ziwa stage 2 na inaelekea 3, tukaanza matibabu ya saratani haraka, tuliandikiwa tuende KCMC moshi, tukauguza hapo for almost 2 years, akapata nafuu tukarudi nyumbani,
Baada ya muda ikarudi tena, tukarudi kcmc, akatibiwa hapo kwa miezi nane na akafariki hapo , sijui wa kumlaumu hapo, japo moyo wangu haujawahi kupona kabisa, nadhani sekta ya afya kwa nchi hii ina shida kubwa, nakumbuka doctor aliyetupima kwenye hospitali ya serikali tulimkuta tena kwenye hospitali hiyo ya binafsi na akatuhudumia tena.