Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma linamshikilia dereva wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), Sath John Masawa (31), baada ya kubainika kutumia bastola ya kuchezea (toyi) kumtishia dereva wa basi la abiria, huku akiwa ametumia namba za usajili za kughushi kwenye gari la Serikali.
Tukio hilo lilimhusisha dereva wa basi la Kampuni ya Satco lenye namba za usajili T 308 EME, Said Fadhil (54), linalofanya safari zake hapa nchini.
Akizungumza kuhusu kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo leo, Septemba 22, 2026, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Gallus Hyera, ameeleza kuwa uchunguzi wa kina wa Jeshi la Polisi ulibaini chombo alichokitumia mtuhumiwa huyo hakikuwa silaha halisi ya moto.
"Baada ya kumkamata mtuhumiwa huyo, Jeshi la Polisi lilifanya uchunguzi na kubaini kuwa kitu hicho hakikuwa bastola halisi kama ilivyodhaniwa awali, bali kilikuwa ni bastola ya kuchezea (toyi)," amebainisha Kamanda Hyera.
Katika hatua nyingine, Jeshi la Polisi limebaini kuwa wakati wa tukio hilo, gari hilo la TARURA lilikuwa likitumia namba za usajili T 881 ENZ badala ya namba zake halisi za usajili wa Serikali ambazo ni STM 5806, huku namba hizo za bandia zikigundulika kuwa ni mali ya mtu mwingine.
Kufuatia kubainika kwa ukiukaji huo wa sheria, Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma limetoa onyo kali kwa madereva na wamiliki wote wa vyombo vya moto nchini kujiepusha na matumizi ya namba za usajili zisizo halali.
#SasaLive #PolisiDodoma #TARURA #GallusHyera #SatcoBus UsalamaBarabarani Dodoma Tanzania
View attachment 3675775