Tukio la kusikitisha sana nchini kwetu Kupigwa Risasi kwa Mbunge wa Singida Mashariki (Tundu A Lissu) ndani ya eneo la Makazi yake ambalo ni makazi ya wabunge spika na wanaofanya kazi Dodoma.
Tukio hili na tukio la Nape kutolewa bastola hadharani, Roma Mkatoliki kutekwa, Ben Saanane kupotea ni kati ya matukio mengi ambayo yametokea nchini yasiyo na majibu.
Matukio haya yana sura za kisiasa - sio ujambazi - ni siasa .
Demokrasia inaendana na uvumilivu - Tukiachia Taifa lijengwe na watu wasio na uwezo kuhoji kisa wanaogopa wakihoji maswali magumu watapotezwa, pigwa risasi tutaangamia wote.
Hakuna ubaya Taifa kuwa na watu wadadisi - Kila darasa huwa linakuwa na wanafunzi waliozidi wenzao akili na mara nyingi waalimu huwaona wasumbufu kwani kuna wakati mwanafunzi anamzidi mwalimu kuelewa - ila mwalimu makini anatumia wanafunzi wenye uelewa wa kasi kusaidia wengine na yeye mwenyewe.
Kosa la Lissu ni uwezo wake wa akili na udadis,Kosa la Nape lilikuwa ni uthubutu wake - Kosa la Roma ni akili zake nyingi kwenye utunzi wa nyimbo zake - Kosa la Saanane ni akili yake ya udadisi na wengine wengi sana.
Badala ya kuogopa watu wenye uwezo mkubwa washirikishe wapewe majukumu makubwa waweze kutumia akili na udadisi wao.
Yanayotokea kwa sasa nchini ni kuwadharau wenye uwezo na kuwakumbatia vilaza- sasa tunapata watekaje, wapiga risasi na wauaji.
Ni akili za ajabu kufikiri kuna uwezekano wa kutisha watu milioni 50 kwa kuwateka, kupiga, kuwauwa au kuwafanya lolote baya.
Binadamu ameumbwa kuzoea mazingira yawe ya amani au vita, mateso au amani, raha au karaha- unapomlazimisha binadamu aone maisha yake ni yahatari wanageuka kuwa wanyama.
Huu sio muda wa kushabikia - Tanzania ni nchi yetu wote - vitendo vya kinyama haviwajahi kumwacha mtu, utawala, kikundi, jamii salama.
Tunataka majibu kutoka serikali hawa wauji ni akina nani- minong'ono imekuwa mingi na ni hatari sana kwa amani ya nchi - wananchi wasiachwe wakajitafutia mbaya wao au wabaya wao itakuwa dark war.
Tume ya Kijaji huru iundwe kuchunguza haya matukio - Haiwezekani mtu apigwe Risasi saa saba mchana halafu zitoke lugha nyepesi, Nape alitolewa bastola mchana mbele ya Camera na mtuhumiwa mpaka leo hakuna kimetokea- sasa wamepiga Risasi saa saba mchana ndani ya Gari bila kujali wangapi wangekufa - ni mambo hatari sana haya.
Tukiyafumbia macho hili neno la watu wasiojulikana litakuja kuwa mwiba kwetu wote.
Iwe ni siasa, visa, chuki, au kitu chochote kile sio jambo jema kulishangilia - Nchi ina katiba, polisi, mahakama, jela na magera kwa sababu ya kutokufanya mambo kama haya. Tusiruhusu haya matukio ndio yawe namna ya kutoa haki.
Hakuna atakayebaki salama mto ukitibuka.