Kuna ujumbe unasambazwa WhatsApp, una kichwa kinachosema Maswali Sita kwa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) je, ni wa kweli?
- Tunachokijua
- Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (kwa Kiingereza Tanzania Episcopal Conference, TEC) ni muundo wa Kanisa Katoliki unaokutanisha maaskofu wake wote wa nchi ya Tanzania, wakiwa wanaongoza jimbo, au ni waandamizi, wasaidizi au wamestaafu.
Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) limetoa tamko tarehe 18, 08, 2023 juu ya mkataba (makubaliano) wa bandari ya Tanzania ambao wameweka msimamo wao wa kutouunga mkono mkataba huo.
Mara baada ya kutolewa kwa tamko hilo, umeonekana ujumbe ambao unasambaa kupitia mtandao wa WhatsApp, ukidaiwa kuandikwa na Shemasi George Rugambwa wa Seminari ya Ntungamo, Bukoba, Ujumbe huo una kichwa cha habari, Maswali Sita kwa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC)
Ni upi ukweli kuhusu ujumbe huu?
JamiiForums ilifanya mawasiliano na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) ili kupata kujua ukweli wa ujumbe huo, ambao wamekanusha kuwepo kwa Shemasi mwenye jina la George Rugambwa katika hiyo Seminari wala kuwepo kwa Shemasi yoyote Seminari ya Ntungamo.
"Hakuna Shemasi katika hiyo Seminari anayejulikana kwa jina hilo na wala hakuna Shemasi kabisa katika hiyo seminari" Walisema TEC
Kufuatia TEC kukanusha kuwepo kwa Shemasi yeyote katika Seminari ya Ntungamo, JamiiForums Imejiridhisha kuwa ujumbe wenye kichwa Maswali Sita kwa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) unaodaiwa kuandikwa na Shemasi George Rugambwa wa Seminari ya Ntungamo kuwa ni wa kuzushwa na hauna ukweli wowote.