KWA NINI UAGIZE KUTOKEA SOKO LA JAPAN BADALA YA NCHI NYINGINE?
Utangulizi
Kwa kua tuna uzoefu mzuri kwenye eneo hili la magari yatokayo nje, tumeona ni vyema leo tugusie kwa ufupi changamoto zinaweza kumpata mtu anayeagiza gari yake nje ya Japan.
Kabla ya kuamua kulipia gari husika ni muhim ukaangalia kwa uhakika gari yako inatokea nchi gani. Mfano, kwenye website ya kampuni kama Beforward utakuta baadhi ya Gari zimeelezwa kwamba zipo U.K au Dubai au U.S au Singapore au Korea au Japan...si kila gari utakayokuta kwenye website husika ipo Japan na hili ni muhimu ulizingatie
Baadhi ya Watu walioagiza magari kutoka nchi kama Uingereza, Singapore, Dubai n.k walipotumia gari zao kwa mda mfupi zilipata matatizo ya kiufundi ikilinganishwa na wale walioagiza magari kama hayo kutokea soko la Japan.
KINACHOVUTIA MTU KUAGIZA GARI KUTOKA NCHI KAMA UINGEREZA AU SINGAPORE BADALA YA JAPAN
1. Gharama ndogo.
Bila kujua kwamba unanunua gari hiyo kwa bei chini sana lakini mwisho wa siku yaweza kuja kukusumbua na kukufanya utumie gharama zaidi kwenye matengenezo
2. Viti vya ngozi na mvuto wa ndani.
Hii iko zaidi kwenye gari zinazotokea Singapore. Hawa jamaa ni wazuri sana kwenye kumvutia mteja kwa macho na hata picha wanajua kuzipiga vizuri, lakini ni mara chache kukuta gari zao hazina matatizo mengine ya kiufundi hivyo usivutike na mvuto wa viti vya ngozi pekee unatakiwa kuangalia mbali zaidi ya viti.
3. Majina ya magari.
Kwa mfano mteja atasema anataka Mazda 6 na sio Mazda Atenza au anataka Mazda 3 na sio Mazda Axella, Mwingine atasema anataka Toyota Yaris na sio Toyota Vitz au anataka Honda Jazz na sio Honda Fit n.k ila ukweli ni kua Yaris ndio Vitz, Axella ndio Mazda 3, Honda Jazz ndio Fit n.k kilichofanya gari zitofautoane majini ni kusudio la nchi gari husika itakapokwenda kutumika.
CHANGAMOTO ANAZOWEZA KUPATA MTEJA ANAYEAGIZA GARI NJE YA JAPAN
1. Hayafanyiwi ukaguzi kabla ya kutafutiwa meli kama ilivyo kwa gari za Japan hivyo kuna uwezekano gari yako ikaja na matatizo ya kiufundi na badala yake ukaguzi hufanywa hapa hapa TZ baada ya gari kufika.
2. Kuna uwezekano gari yako itokayo nje ya Japan haswa Singapore na Dubai ikawa imechezewa kilomita ili kukuvutia zaidi na mwisho wa siku ndio huishia kukusumbua tofauti na kilomita zake zilivyo chache na ukizingatia kwao hizi sio biashara kuu sana hivyo serikali hazijaweka nguvu za kutosha kudhibiti hili.
3. Utalazimika kuingia gharama ya Ukaguzi baada ya gari kufika ambayo yawezekana hata hukuiwazia. Gari za Japan zinafanyiwa ukaguzi kule kule na Gharama yake unakua umeilipa kwenye CIF tofauti na zinazotoka mataifa mengine.
Mwisho
Uamuzi ni wa mteja husika kuamua gari yake anataka itokee kwenye soko la nchi gani. Kuna gari ambazo hazipatikani kwenye masoko ya Japan, hivyo unakua huna namna zaidi ya kuchukua kutoka hayo masoko mengine. Lakini pia hii haiondoshi ukweli kua gari zilizotengenezwa ulaya ni bora zaidi kuliko za Japan, hapo juu tumeelezea zaidi ubora wa soko la gari used na sio gari ikiwa mpya kabisa.