Kwa niaba ya wananchi wa mji mdogo wa MALAMPAKA ulioko wilaya ya MASWA mkoa wa SIMIYU ktk jimbo la MASWA MAGHARIBI chini ya mbunge wangu ndugu Mashimba (CCM) naandika kulalamikia upatikanaji wa umeme kwa sababu umekuwa kero kubwa na kusababisha athari nyingi na kubwa za kiuchumi na kijamii kwetu sisi wananchi na hata tumeshindwa kuvumilia
Kwa takribani wiki mbili mfululizo sasa umeme umekuwa ukikatika katika hovyo hata mara 20 kwa siku. Na kuna wakati TANESCO mnakata hata masaa zaidi ya 48 bila umeme
Mji wa Malampaka ni wa pili kwa ukubwa katika wilaya ya Maswa baada ya makao makuu ya wilaya.
Mji huu ndiyo kituo kikuu cha reli kwa mkoa wote wa Simiyu.
Aidha huu ni mji wa viwanda vidogo dogo vingi hasa vya kusaga nafaka (unga), kukoboa mpunga na mji huu ni kituo kikuu kimkoa kwa biashara ya Michele
Mji huu mdogo unakadiriwa kuwa na wakaazi (population) ya watu karibu 25,000
Umeme ni nishati muhimu sana kwetu kwa ajili ya shughuli za uzalishaji kwenye viwanda vidogo dogo vya kusaga nafaka (unga), kukoboa mpunga ili kupata mchele, kupoza juice kwenye friji ili tuuze tujipatie kipato, umeme na saluni za kunyoa na za wanawake, stationeries kuendeshea computers nk
Si hivyo tu, bali tunategemea umeme wa TANESCO ili uendeshee machine ya kusukuma maji kwenye matenki ili wakaazi wapate maji kwenye magati
Sasa hebu fikiria, masaa 48 unapokuwa huna umeme unawaathiri watu kwa kiwango gani? Ni wazi kabisa, kuwa, ni kwa kiwango kikubwa!
Kibaya zaidi ni kuwa TANESCO hawatoi taarifa yoyote kueleza tatizo ni nini na litachukua muda gani kutatuliwa. Hivyo hutudharau na kutuacha wananchi ktk sintofahamu kubwa isiyo na maelezo
Nakumbuka waziri wa nishati ndugu Medard Kalemani mapema mwezi Februari, 2018 alikuja hapa Malampaka na kufanya mkutano na wananchi ktk viwanja vya TTCL na kuawaahidi kuwa tatizo la kukatika katika umeme Malampaka na Maswa kwa ujumla litakuwa historia ifikapo mwezi Mei, 2018 kwa sababu serikali inajenga line kubwa mpya mbili za umeme;
¶ Moja toka Ibadakuli, Shinyanga hadi Maswa kisha Bariadi
¶ Na ya pili toka Mwabuki - Misungwi - Mwanza ipite hapa Malampaka hadi Maswa kisha iungane na ile inayotoka Ibadakuli - Shinyanga kuelekea Bariadi
Aidha Waziri aliahidi na kuagiza yafuatayo kufanyika pia;
¶ Mosi, TANESCO kufungua ofisi ndogo hapa Malampaka kuhudumia wananchi.
Hili limefanyika japo kiuhalisia hakuna ofisi bali kuna Tent (turubai) tu na kuna vijana wawili ambao kazi yao ni kupokea malalamiko tu ya wateja
¶ Mbili, TANESCO wajenge kituo kidogo cha kupozea umeme pale MASWA ili kusaidia kuleta stability ya upatikanaji umeme ktk eneo hili
Sina hakika kama maagizo haya yalitekelezwa na wahusika kwa sababu laiti kama ingekuwa hivyo, watu tusingekuwa tunalalamika hivi hata kuona kuwa umeme ni tatizo kuliko hata virusi vya CORONA!
HIVI, ninavyoposti taarifa sasa ikiwa ni SAA 4:30 usiku huu, hatuna umeme tangu jana!
Ulikatika around saa 9alasiri jana tarehe 10/3/2020. Ukawaka tena leo saa 6 mchana. Umekuwa hivyo hivyo ukiwaka na kukatika katika hivyo na umekatika moja kwa moja ilipofika saa 12jioni na haieleweki utarudi lini!!
Sasa hebu TANESCO mtuambie, mna matatizo gani? Mnakwama wapi? Kwanini inakuwa ni ngumu kuwasiliana na sisi wateja wenu ili tujue na watu tujiandae kutafuta nishati mbadala?
Msituambie kuwa tatizo ni mvua zinazonyeesha na kuathiri miundo mbinu ya usafirishaji umeme
Hili linaweza lisiwe kweli kwa sababu hata umeme unapokuwa umewaka, unakuwa haupo stable. Ndani ya saa moja unaweza kuwaka na kuzima hata mara 10 mpaka hufikia watu tunajisemea "labda fundi mitambo anajifunza kuwasha na kuzima!!"
Rais JOHN POMBE MAGUFULI mwaka 2015 alipoingia madarakani, alitamba sana kuwa umeme wa mgawo na ile hali ya kukatika katika hovyo nchi hii itakuwa historian
Sasa hii ahadi yake mbona inakuwa kama zilikuwa nguvu ya soda ya coca cola tu? Kwanini mnanyanyasa wananchi hivi nyie serikali ya CCM ya wanyonge??