Alikuwa ni kiongozi mbaya kupindukia. Japo alikuwa muuaji na katili, kiasi cha kila mpenda haki kupendelea kutokuwa na kiongozi wa namna ile, lakini nilisikitika kupokea taarifa za kifo chake. Ni jambo jema mwovu aendelee kuishi, ajutie uovu wake au abadilike na kuuchukia uovu wake wa kale. Nilipoisikia habari ile, nilishtuka, nikaamka. Nilikaa kimya kwa dakika, nikajawa na simanzi. Maana kwa kweli pamoja na kuwaaumiza watu wengi, haikuwahi kutokea akilini mwangu kufikiria kuwa, aheri afe. Ningependelea aondoke kwenye uongozi lakini siyo kufa. Lakini basi kwa kuwa ilitokea, mapenzi ya Bwana yalitimia kwa kipimo cha hekima yake Mungu.
Vyovyote iwavyo, kifo chake ni fundisho kubwa kwetu tulio hai. Cha kujiuliza, sisi tunafanya nini tofauti na uovu wake? Tunafanya nini sambamba na mazuri yake, hata kama yakiwa machache? Kuna wengine ni fundisho kubwa kwao mara mbili zaidi maana wakati wa utawala wake, walitenda uovu mwingi wakiamini yupo wa kuwalinda kwenye uovu wao.
Wapo waliomkufuru Mungu, hata wakamwita Magufuli ni Mungu, wengine wakasema ni zaidi ya Yesu, na wengine wakasema eti Mungu amshukuru Magufuli. Na wote sasa hivi wamebakia kama kondoo wasio na mchungaji.
Hii ilikuwa ni kufuru kubwa. Mbaya zaidi hata marehemu mwenyewe hakuwakemea. Mwalimu Nyerere alipopambwa kupita kiasi, alimaka na kusema, 'mmeniita mchongameno nimenyamaza, mmeniita Haambiliki nimenyamaza, lakini hili la Musa, kuniita Musa, hapana, sitaki kusikia'. Yaani Mwalimu aliona kuwa yeye hafanani wala kumkaribia kwa chochote nabii Musa aliyewaongoza wana wa Israel toka utumwani Misri. Nabii Musa alikuwa mwanadamu, lakini mwalimu aliona bado Nabii Musa ni mkubwa mno kuweza kufananishwa naye. Marehemu alilinganishwa na Mungu, yeye akakaa kimya. Lilikuwa kosa kubwa.
Kifo chake ni fundisho kwetu kuwa Mungu hana ushirika na mwanadamu yeyote katika Umungu wake. Tunafundishwa kuwa Mungu hana mwanzo wala mwisho. Kifo hiki kilitufundisha kuwa hata uwe na nini, wewe bado ni mwanadamu, unafanana na wanadamu wenzako katika kuzaliwa na kufa.
Tuendelee kuomba, Mungu atujalie hekima ya kujifunza kupitia kifo hiki, na wala kifo hiki kisitufanye kuzidi kumkosea yeye Mungu au wanadamu wenzetu.