View attachment 421962
View attachment 421964
View attachment 421965
Kwa miaka mingi sasa sekta ya utalii nchini imeshindwa kuchangia pato la taifa kama inavyostahili. Kuna changamoto nyingi sana ambazo zimesababisha jambo hilo lakini naomba nitaje chache kisha na wenzangu mnaweza kuchangia na kuishauri serikali hatua za kuchukua ili kuimarisha sekta hii muhimu kwa ustawi wa uchumi wetu.
1. Sekta hii haijatangazwa ipasavyo ndani na nje ya nchi na serikali
2. Sekta hii imekumbatiwa na watu wachache na kupitia umoja wao wameifanya sekta hii kuwa kama mali yao binafsi na ni wao wanaoishauri serikali kuweka masharti magumu ili kuendelea kunufaika wao peke yao.
3. Kuna masharti magumu yanayokwaza wafanyabiashara wadogo kuingia kwenye sekta hii na hivyo kunufaisha wadau wachache
4. Miundo mbinu katika hifadhi zetu ni kikwazo katika kukuza biashara hii ya utalii
5. Vyuo vyetu vya utalii ni vichache vinatoa mafunzo duni yasiyoendana na ukuaji wa sekta hii na wahitimu wengi wanaomaliza kusoma wanakuwa na uwezo wa kufanya kazi za chini na zile nafasi kubwa kushikwa na wageni
6. Kutokuwepo kwa vivutio na mahoteli makubwa katika miji mikuu yenye hadhi ambayo ipo jirani na mbuga zetu za wanyama
7. Kutokuwepo au kutoboreshwa kwa maeneo yenye historia ya miji mbalimbali hapa nchini
8. Maonyesho ya utalii kutopewa kipaumbele na kufanywa katika mikoa miwili tu Kilimanjaro na Arusha
9. Kutokuwepo kwa taarifa za mara kwa mara kuhusu takwimu za watalii wanaoingia nchini na nchi wanazotoka zaidi ya kupatikana kwenye hotuba za waziri bungeni.
10. Ushiriki mdogo wa maonyesho ya utalii nje ambapo serikali haisaidii kuwawezesha wafanyabishara wadogo wa utalii kushiriki maonyesho haya
Nini kifanyike:
1. Serikali ijikite kwa nguvu zote kutangaza utalii katika mataifa mbalimbali ili kuvutia watalii wengi zaidi kutembelea nchi zetu. Juhudi hizi ziende sambamba na kutoa mialiko maalum kwa watu maarufu duniani kutembelea vivutio vyetu na serikali kuchangia baadhi ya gharama na ziara hizo ziwekwe mwenye vyombo vya habari vya hapa nchini na nje.
2. Kuna fukuto la mgawanyiko katika umoja wa wafanyabiashara ya utalii kati ya wale wafanyabiashara wakubwa na wale wadogo. Na mgawanyiko huu unatokana na wafanyabishara wakubwa kutetea maslahi yao zaidi na kuwaacha wafanya bishara wadogo wakikosa pumzi. Serikali inatakiwa kutengeneza mazingira yatakayowawezesha wafanyabishara wa utalii kuwa na mazingira mazuri ya kufanya bishara zao bila kujali uwezo wao wa kimtaji, lakini pia kuwe na utaratibu wa kuwatambua wafanyabishara wanaouza safari kupitia mitandao ya kijamii na utaratibu huo iwe ni pamoja na kuwapatia leseni na utaratibu wa kulipa kodi, hii itasaidia serikali kuongeza mapato kwa ukusanyaji kodi kwani kwa miaka mingi sekta hii imekuwa ni kichaka cha wafanyabiashara wasio waaminifu kukwepa kodi kwa mbinu mbalimbali, Tunaweza kufanya utafiti kwa nchi kama Afrika Kusini na visiwa vya Mauritius na Shelisheli au Botswana ili kujua wenzetu wamewezaje kuboresha sekta ya utalii katika nchi zao na serikali inanufaikaje na mapato ya utalii katika nchi zao
3. Serikali ilegeze masharti ya kupata leseni za kuanzisha kampuni za utalii kwani siku hizi kuna aina nyingi za kuuza safari ambapo huduma nyingine zinaweza kufanywa na mtu mwingine kama huduma za ndege, huduma za magari kuna makampuni mengi ya kukodisha magari nk. Iwapo serikali itabadilisha masharti ya usajili wa makampuni ya utalii itaongeza wafanyabishara wengi katika sekta hiyo na hivyo kujiongezea kipato cha uhakika.
4. Tuna miundo mbinu mibovu sana katika vivutio vyetu vya utalii na mfano halisi ni ilipo mbuga ya Selous. Hii ni mbuga ambayo ingetumiwa na wageni wanaokuja jijini Dar kutembelea na kuona wanyama mbalimbali ukiwemo mto Rufiji. Hii ni mbuga ambayo ingeweza kutuingizia kipato kama kungetengenezwa mazingira ya kuwepo kwa Treni itakayokuwa inafanya safari zake hadi Kisaki na kurudi kila siku na pale kukawa na Hoteli kubwa na wawekezaji wa utalii wakapewa maeneo ya kujenga ofisi zao na kuboreshwa kwa barabara inayoingia Selous ingerahisisha watalii kutumia treni hadi Kisaki na pale wanapokelewa na kupelekwa mbugani na magari kwa kupitia barabara zilizoboreshwa. Naamini wageni wengi wanaoishi jijini Dar wangetumia fursa hii kutembelea Selous kila mwishoni mwa wiki. Kwa sasa njia ya usafiri wa gari unachukua saa kumi kupitia Matombo na saa 7 kupitia Rufiji ili kuingia mbugani huku ndege ndogo zikitumia dakika 45 lakini ni ghali sana watu wenye kipato cha kawaida kumudu. Serikali inaweza kuwashirikisha wadau wa utalii ili kupata mawazo yao namna nzuri ya kuboresha miundo mbinu yetu katika hifadhi zetu
5. Serikali iongeze vyuo vya utalii ikiwa ni pamoja na kuboresha mitaala ili kuinua elimu inayotolewa na vyuo hivyo. Kwa sasa vyuo vyetu vya utalii ni vichache na elimu inayotolewa humo ni ya kuwaandaa vijana wetu kuja kuwa vibarua na siyo kuwa viongozi katika sekta hiyo. Kwa sasa sekta ya utalii ndiyo inayoajiri wageni wengi kuliko sekta nyingine hapa nchini huku wengine wakiingia na kufanya kazi kiujanja. Tunahitaji mkakati makini ambao utaboresha elimu ya utalii kwa vijana wetu ili kupunguza ukosefu wa ajira. Zipo baadhi ya nafasi katika mahoteli yetu na makampuni ya utalii ili kuzishika labda ukapate elimu hiyo nje ya nchi au upate mafunzo kazini. Hii ni aibu kwa nchi yetu yenye vivutio vingi vya utalii kutegemea nguvu kazi kutoka nje huku vijana wetu wakiendelea kuwa vibarua
6. Tunahitaji katika mikoa ambayo iko karibu na vivutio waalikwe wawekezaji wa kuwekeza katika mahoteli na pia katika mikoa hiyo yatengwe maeneo ya historia ya makabila ya mkoa huo na maeneo mbalimbali yatengwe kwa ajili ya utalii na yaboreshwe ili watalii wanapokuja kabla ya kutembelea vivutio vyetu huko mbugani wapate fursa ya kujifunza utamaduni wa eneo husika na kujua asili ya eneo hilo na watu wake.
7. Serikali kwa kushirikiana na wadau wa utalii iboreshe maeneo yenye historia ya miji mbalimbali hapa nchini na kuitangaza ikiwemo ujenzi wa masanamu ya watu walioacha historia katika miji hiyo kama kule Tabora kina Mtemi Milambo au kina Kishosha Ng’wanamalundi
8. Kuwe na mkakati wa kutoa kipaumbele kwenye maonyesho ya utalii na yawe yanafanywa katika mikoa yote yenye vivutio ili kuimarisha utalii wa ndani hii iwe ni tofauti na ile ya kimataifa inayofanyika Arusha na Moshi, lakini hata hiyo ya Arusha na Moshi inapaswa kuboreshwa kwa kuiga wanavyofanya katika nchi za wenzetu
9. Taarifa za mara kwa mara kuhusu takwimu za watalii wanaoingia nchini na nchi wanazotoka ni muhimu ili kuwarahisishia wafanyabishara wa utalii kujua soko liko wapi, uwepo wa kitengo kitakachokuwa kinakusanya taarifa hizo na kuziweka mtandaoni kutasaidia kujua ni wapi tumejitangaza na wapi hatujajitangaza ili kuelekeza nguvu zetu huko.
10. Kuwe na mkakati wa kuhakikisha wafanyabishara wa utalii wanashiriki kwa wingi kwenye maonyesho ya utalii katika nchi mbalimbali ili kupata fursa ya kutangaza vivutio vyetu.
Naomba nipishe michango mingine kutoka kwa wadau mbalimbali ili tuweze kuishauri serikali namna nzuri ya kuboresha sekta hii ya utalii.