Wataalamu wa kilimo wa Rwanda wapata maarifa mapya kutoka mradi wa mafunzo wa China

Wataalamu wa kilimo wa Rwanda wapata maarifa mapya kutoka mradi wa mafunzo wa China

ldleo

JF-Expert Member
Joined
Jan 9, 2010
Posts
1,310
Reaction score
1,265
未确认 24165.png

Ndani ya chumba cha mafunzo katika mji mkuu wa Rwanda, Kigali, mjadala kuhusu chakula, kilimo na teknolojia unaendelea wakati washiriki wakisikiliza, kuuliza maswali, na kubadilishana uzoefu na wataalamu wa China. Kwa wataalamu wa Rwanda wanaohudhuria kozi hiyo ya Teknolojia ya Uchakataji na Uhifadhi wa Bidhaa kwa Nchi za Nje tangu Agosti 19 hadi Septemba 17, mafunzo hayo yametoa zaidi ya mafundisho kuhusu uhifadhi wa chakula na teknolojia za uchakataji, na kutoa fursa mpya ya kutathmini changamoto zinazokabili sekta ya kilimo ya Rwanda.

Miongoni mwa wataalamu kutoka Rwanda ni Judith Niyonsaba, mhitimu wa sayansi na teknolojia ya chakula, na anafanya kazi katika Kiwanda cha Inyange cha nchini humo. Wakati mafunzo yakiendelea, mafundisho kuhusu uchakataji wa matunda na maziwa na mifumo ya mnyororo wa baridi inahusika zaidi na changamoto anazokutana nazo katika kazi zake za kila siku. Wakati wa msimu mrefu wa kiangazi, anasema upatikanaji wa maziwa unapungua, huku matunda kama nanasi na tunda la passion yanaweza yasitimize mahitaji ya wachakataji. Anaona kuwa, wakulima wanahitaji zaidi uelewa na ufundi ili kuongeza uzalishaji na kuhifadhi ubora wa kile wanachovuna.

Washiriki wengine wanaelezea mambo kama hayo wakati wa kujifunza na kutafakari. Roger Kayijuka Ndayishimiye, mtaalamu wa usimamizi na tathmini katika Kampuni ya Chai ya Rwanda Mountain, anasema mafunzo hayo yamewatambulisha washiriki katika teknolojia zinazoweza kusaidia kuifanya sekta ya chai ya Rwanda kuwa ya kisasa, ikiwemo mitazamo ya usimamizi wa mabaki ya viuatilifu na vipimo vya kasi vya usalama wa chakula. Anasema kozi hiyo ni msaada mkubwa kwake, na hata kwa nchi nzima, kwani wameweza kuona teknolojia tofauti zinazoweza kutumika ili kuifanya sekta ya chai kuwa ya kisasa zaidi.

Mkuu wa Idara ya Sayansi na Teknolojia ya Chakula katika Chuo Kikuu cha Rwanda, Bernard Rwubatse, anasema kozi hiyo imeongeza uelewa wake na itasaidia utafiti wake na shughuli za kubadilishana uzoefu. Pia, anasema mafunzo hayo yameonyesha jinsi teknolojia za kisasa zinavyoweza kuboresha usalama na ubora wa chakula wakati Rwanda ikipiga hatua kutoka mchakato wa kilimo cha jadi hadi kilimo cha kisasa, na kwamba washiriki wa kozi hiyo wametambulishwa teknolojia endelevu na zinazotegemeka zinazoweza kusaidia kudumisha usalama na ubora wa bidhaa zinazochakatwa.

Peng Hao, mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa katika Taasisi ya Kitaifa ya Utafiti wa Chakula na Viwanda vya Usindikaji ya China, (CNRIFFI), anasema mafunzo hayo yanawakilisha uratibu mwingine wa kina kati ya China na Rwanda unaolenga kushirikisha teknolojia na uzoefu wa China katika uchakataji na uhifadhi wa bidhaa za kilimo na wenzao wa Rwanda. Ameongeza kuwa, kozi za mafunzo kama hiyo zimefanyika nchini Rwanda mwaka 2019 na 2024, na wataalamu wa uchakataji wa bidhaa za kilimo, uhifadhi, na ukaguzi wa ubora na usalama kutoka China wakialikwa kutoa mafunzo yanayolenga maeneo husika na mwongozo wa kivitendo kutokana na mahitaji ya maendeleo ya kilimo ya nchini Rwanda.

Mafunzo hayo yaliyofadhiliwa na Wizara ya Biashara ya China na kuandaliwa na Taasisi ya Kitaifa ya Utafiti wa Chakula na Viwanda vya Usindikaji ya China, (CNRIFFI), yalileta pamoja washiriki 30 kutoka taasisi za umma za Rwanda, taasisi za utafiti, na wamiliki wa viwanda.
 
Back
Top Bottom