Kinuju
JF-Expert Member
- Mar 20, 2021
- 2,386
- 5,325
Handeni. Waziri wa Maji, Jumaa Aweso ameliagiza jeshi la polisi wilayani Handeni kuwakamata na kuwaweka ndani watumishi wawili wa wizara hiyo na mkandarasi anayejenga bwawa la Kwenkambala kwa kushindwa kumpa taarifa sahihi kuhusu ujenzi wa bwawa hilo.
Waziri Aweso ametoa agizo hilo leo Jumanne April 12 kwenye ziara yake ya kukagua ujenzi wa bwawa la maji la Kwenkambala na miradi ya maji katika kijiji cha Msomera, ambapo wasimamizi wa mradi wa Kwenkambala kutoka Ruwasa na Mkandarsi walishindwa kutoa taarifa alizotaka waziri na kuagiza wakamatwe.
Waliokamatwa na jeshi la polisi ni mtaalamu wa bwawa kutoka Ruwasa Hamisi Matunguru, mkandarasi Robert Lupinda na Mhandisi Amos Mtweve mthibiti ubora kutoka makao makuu ya Ruwasa.
Waziri amesema kuwa fedha zilipelekwa watu wapate huduma ya maji ila kwa makusudi kuna waliohujumu fedha za mradi na kushindwa kuendelea mpaka sasa.
"Kwa wataalamu wetu ambao kwa makusudi wanaendeleza hizi hujuma sitasita kuwachukulia hatua, hata awe mkubwa vipi lazima atachukuliwa hatua, niombe radhi kwa wananchi na viongozi wa Handeni kwa hili lililotokea".
Mkandarasi Robert Lupinda kwa upande wake amesema amesimama kuendelea na ujenzi wa bwawa hilo baada ya kusimamishwa.
"Sasa hivi nimesimama kazi kwasababu nimepewa oda ya kusimama, tulifanya kikao mara ya mwisho Dar es Salaam nikaambiwa natakiwa kusimama," amesema mkandarasi.
Kwa upande wa viongozi kutoka Ruwasa alioagiza wakamatwe Waziri Aweso amesema kesho Jumatano atakaa kikao na wataalam wengine Dodoma ili kujua shida iko wapi na atachukua hatua.
Hata hivyo mwenyekiti halmashauri ya mji Handeni Mussa Mkombati ameongeza kuwa kuna suala la mkataba wa Tsh. Milioni 132 mwingine nje ya ule wa Bilioni 1.9 za mradi ambao ni tofauti, hivyo kumuomba waziri pia kuufuatilia.
Amesema pia wananchi wote ambao wamezungukwa na mradi hawajalipwa fidia zao mpaka sasa huku mkandarasi akilipwa asilimia zaidi ya 30 za fedha kwaajili ya kuanza kazi, jambo ambalo limefanya wananchi walalamike.