Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Tundu Lissu leo ameandika barua kulaani shambulio Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu wa Katoliki Tanzania (TEC), Padri Dkt.Charles Kitima, na tukio la kushambuliwa na kutekwa kwa mwanaharakati Mdude Nyagali.
"Nalaani vikali shambulio dhidi ya Padre Dk. Charles Kitima na kushambuliwa kwa kipigo kikali na kutekwa kwa Mdude Nyagali. Rais Samia na Serikali yake wanahusika na vitendo hivi viovu vya kigaidi. Natoa wito kwa Rais Samia na serikali yake kuhakikisha kuwa Mdude Nyagali anaachiwa mara moja na anapata huduma ya dharura ya matibabu anayohitaji.
Kwa Padre Kitima, namtakia ahueni ya haraka na kumsihi yeye na Maaskofu wa Tanzania kudumisha misimamo yao thabiti na yenye misingi mikuu katika mapambano ya kudai Tanzania ya haki, usawa na demokrasia.
Kwa viongozi wa CHADEMA, wanachama, wapenzi, na wananchi wa Tanzania kwa ujumla, nawaomba kutokata tamaa wala kukatishwa tamaa katika kupigania demokrasia ya nchi yetu. Ninataka wajue kwamba nipo thabiti kabisa na siyumbishwi, na hakuna kuta za gereza zitavunja roho yangu. Ninawapenda wote, na nitarudi.
P.S. Nisipopelekwa kortini Jumanne kama inavyostahili, nitaanza mgomo wa kula."