Chan...
Nimejadili suala hili katika kitabu cha Abdul Sykes (1998):
''Vyanzo tofauti vya takwimu vinatoa takwimu tofauti zinazopingana kuhusu hesabu ya Waislam na Wakristo katika Tanzania.
Hii inatokana na ukweli kuwa somo hili ni nyeti.
Katika nchi za Kiafrika ambazo zina wafuasi wengi wa dini hizi mbili, kwa mfano Tanzania na Nigeria, uchunguzi wa kuwa ni dini gani ina wafuasi wengi kupita mwenzake ni chanzo cha mgongano na mzozo.
Tatizo hili lipo Tanzania.
D.B. Barret anasema kuwa Waislam Tanzania ni wachache wakilinganishwa na Wakristo.
Takwimu zake zinaeleza kuwa Waislam ni 26%, Wakristo 45% na Wapagani ni 28%.
Takwimu za Tanzania National Demographic Survey za mwaka wa 1973 zinaonyesha kuwa Waislam ni wengi kidogo kupita Wakristo wakiwa 40%, Wakristo 38.9% na Wapagani 21.1%.
Lakini takwimu za Africa South of the Sahara, zinaonyesha Waislam ni wengi Tanzania kwa 60%.
Takwimu hizi zimebaki hivyo bila ya mabadiliko toka mwaka 1982.
Kwa kuwa utafiti wa Waislam wenyewe katika suala hili ni mdogo sana au haupo kabisa, suala la wingi wa Waislam katika Tanzania halijafanyiwa utafiti na Waislam wenyewe.
Mgao wa madaraka na kugawana vyeo haikupashwa kuwa sababu ya migongano na mifarakano katika Afrika.
Lakini kwa bahati mbaya sana hii imekuja kuwa sababu ya mifarakano katika serikali za wananchi wenyewe.
Jambo hili limekuwa ni suala nyeti kwa sababu ukabila, udini na kujuana ni kitu muhimu katika serikali za Afrika.
Mgawanyo wa madaraka na wingi wa wafuasi katika dini au kabila havikuwa vitu vilivyokuwa vikiwashughulisha wananchi wakati wa ukoloni kiasi cha kuleta mifarakano katika jamii.
Kwa bahati nzuri ukabila hauna nguvu Tanzania lakini dini imekuwa chanzo cha ubaguzi toka zama za ukoloni, tofauti ni kuwa wakati wa ukoloni waliokuwa wakiwabagua Waislam hawakuwa Wakristo weusi bali Wazungu.''
(Kutoka kitabu cha Abdul Sykes)
Prof. Mazrui kalieleza tatizo hili kwa kirefu: Ali A. Mazrui, ''African Islam and Competitive Religion: Between Revivalism and Expansioní,'' in Third World Quarterly Vol. 10. No. 2.
Mimi binafsi nimekuwa nalikwepa ila nililizungumza kwa kirefu katika mhadhara niliotoa University of Iowa nilipoletewa takwimu za CIA zinazoonyesha kuwa idadi ya Waislam ni ndogo Tanzania ukilinganisha na Wakristo.
Nilirejesha suala hili kwao na kuwauliza kama kuna nchi yoyote duniani ambayo ilivamiwa na wageni kutoka nje kama Wejerumani walipofika kwetu na waliosimama kupambana na wageni hao kwa silaha wakawa ni minority.
Hapa nilitoa mfano wa mapambano ya Wajerumani.
Nikawauliza pia kama ipo histori ya nchi yoyote ambayo siasa za utaifa zilipopamba moto baada ya WW II waliosimama kuongoza kudai uhuru walikuwa wale wachache na wengi wakawa pembeni.
Hapa nikatoa mfano wa harakati za kupigania uhuru wa Tanganyika.
Ukumbi mzima ulibaki kimya.
Hakuna aliyechukua changamoto hii.
Katika hadhira hii kulikuwa na maprofesa wanne ambao wanaijua vyema historia ya Tanzania: Prof. James Giblin, Prof. Michael Lofchie, Prof. Jonathon Glassman na Prof. James Brennan.
Hawa wote wameandika vitabu wengine zaidi ya kimoja kuhusu historia ya Tanzania.
Jonathon Glassman kutokana na mjadala huu akanialika chuoni kwake Northwestern University, Chicago, tukafanya mjadala kama huu tuliofanya University of Iowa.
Niliukubali mwaliko na nilizungumza Northwestern University.
Katika mhadhara huu suala la Takwimu za CIA na Waislam wa Tanzania halikujitokeza.
Majibu niliyowapa University of Iowa nadhani yaliwatosheleza.