TUNDU LISSU ANAMHOJI SHAIDI WAKE AMAN GOLUGWA MAHAKAMANI
SEHEMU YA 13
MAHAKAMA IMEREJEA
1. Majaji wameingia.
2. Mheshimiwa Tundu Lissu yupo kizimbani.
3. Amani Sam Golugwa yupo ukumbini.
4. Mawakili wa Serikali wapo tayari.
5. Watu wamekaa katika nafasi zao.
Jaji Ndunguru: Tuendelee.
Ajuaye Zegeli: Waheshimiwa Majaji, kolamu ipo vilevile.
Tupo tayari kumsikiliza shahidi namba 3 wa upande wa utetezi.
Jaji Ndunguru: Mshtakiwa, upo tayari?
Lissu: Nipo tayari, Waheshimiwa Majaji.
Amani Sam Golugwa anapanda kizimba cha shahidi.
Jaji Ndunguru: Shahidi, unakumbushwa bado upo chini ya kiapo.
Lissu: Asante, Waheshimiwa.
Shahidi, tulipo-break ulikuwa unaelezea masuala ambayo niliyazungumza kwenye huo mkutano wa tarehe 03 Aprili mwaka jana.
Na ukawa umefikia masuala yote ambayo nilikuwa nimeyazungumza katika vitongoji na mitaa kwa uchaguzi wa 2024.
Baada ya hapo tuka-break.
Amani Sam Golugwa: Waheshimiwa Majaji, mambo ambayo Tundu Lissu aliyazungumza katika mkutano huo ni masuala ya mauaji ambayo yalikuwa yametokea katika chaguzi mbalimbali.
Lissu: Eleza nilisema nini.
Amani Sam Golugwa: Alitaja mauaji yaliyokuwa yametokea Manyoni kwa mgombea wa CHADEMA.
Mauaji yaliyokuwa yametokea Tunduma na Dar es Salaam.
Alitaja pia matukio mengine ya mauaji kwenye marudio ya uchaguzi mdogo wa Ubunge Kinondoni.
Lissu: Baada ya kutaja hiyo mifano ya mauaji katika chaguzi mbalimbali, hoja yangu nilisema nini?
Amani Sam Golugwa: Mheshimiwa Tundu alitoa hoja...
Jaji Ndunguru: Sema “ulisema”. Ukisema “alisema” inakuwa kama unamzungumzia mtu mwingine. Akikuuliza “nilisema nini?”, usiseme “alisema”.
Nadhani tupo sawa.
Lissu: Tupo sawa, Waheshimiwa.
Shahidi, endelea. Nilisema nini?
Amani Sam Golugwa: Ulisema, kuliko kupitia mabalaa haya yote ya watu kuuawa katika chaguzi, vurugu na fujo, tupo tayari uchaguzi uahirishwe na usogezwe mbele ili, kama Taifa, tuweze kushughulikia matatizo haya yaliyopo kwenye mifumo yetu ya uchaguzi.
Na ulisema tuna maana, tupo tayari na sheria zetu zina ruhusa uchaguzi kusogezwa mbele.
Lissu: Jambo lingine nililolizungumzia unalolikumbuka?
Amani Sam Golugwa: Waheshimiwa Majaji, jambo lingine ulisema kwa ambaye anawaza kugombea uchaguzi huu, sasa asahau, aende akafanye kazi ya kuwaelimisha wapiga kura wake ili Watanzania watuunge mkono.
Jambo lingine ulisema na wewe una hamu ya kugombea urais na unataka kugombea urais, ila hutogombea, na unataka uchaguzi usogezwe mbele.
Ukasema utaenda kuwaelimisha Watanzania na utazunguka nchi nzima ili wakuunge mkono.
Lissu: Kuna jambo lingine unataka kuliongezea, unalolikumbuka?
Amani Sam Golugwa: Waheshimiwa Majaji, hayo ndiyo ninayokumbuka.
Sina la kuongezea.
Lissu: Mtu akikuletea haya maneno niliyokusomea mwanzo:
“........Msimamo huu unaashiria uasi, ni kweli, ni kweli kwa sababu tunahamasisha uasi........”
Mtu akatumia haya maneno kusema nimetengeneza nia, akaacha hayo yote uliyoyaeleza, wewe unaonaje?
Amani Sam Golugwa: Waheshimiwa Majaji, imetengenezwa ili kuonyesha kuna kosa.
Hivyo ndiyo nitakavyoona.
WEKA EMOJI KAMA UNASOMA
SHARE ZAIDI UJUMBE UFIKE MBALI