Gloria Tesha
Daily News; Thursday,May 29, 2008 @00:05
MBIO za Mwenge wa Uhuru ni moja ya matukio yenye kulinda na kukuza historia ya nchi. Matukio hayo yanalenga kuwaenzi wanaharakati, viongozi na wananchi waliopigana kufa na kupona, kuhakikisha kuwa taifa linakuwa huru kabla na baada ya Uhuru mwaka 1961.
Kwa mara ya kwanza Mwenge wa Uhuru, uliwashwa juu ya kilele cha Mlima Kilimanjaro Desemba 9 mwaka 1961 na Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere. Tangu mwaka huo, serikali ikiongozwa na chama tawala cha Tanganyika African National Union (TANU) iliratibu na kuendeleza Mbio hizo za Mwenge wa Uhuru.
Baada ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964, mbio hizo ziliimarishwa zaidi katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ziliimarishwa kwa lengo la kukuza umoja na mshikamano miongoni mwa Watanzania bila kujali tofauti za kabila, rangi, itikadi na dini. Hivyo, kwa miaka mingi kazi ya kuendesha Mbio za Mwenge, ilikuwa ikifanywa na TANU.
Hata hivyo, taarifa mbalimbali za historia ya Mwenge wa Uhuru, zilizopatikana kutoka wizara inayoratibu mbio hizo, ambayo ni Wizara ya Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana hasa Idara ya Maendeleo ya Vijana, zinaeleza kuwa mfumo wa kukimbiza Mwenge wa Uhuru ilibidi ubadilishwe mwaka 1993, kutokana na mabadiliko ya kisiasa, yaliyotokea nchini mwaka 1992.
Mwaka huo, nchi iliacha mfumo wa chama kimoja cha siasa na kuingia katika siasa ya vyama vingi. Kutoka mwaka huo, Mbio za Mwenge wa Uhuru zilirejeshwa chini ya utaratibu wa Serikali mwaka 1993.
Sasa ni mwaka wa 15 tangu Serikali ianze kuratibu na kusimamia mbio hizo, lengo likiwa ni kuondoa dhana ya kwamba Mwenge wa uhuru ni wa chama tawala, ambacho kwa sasa ni CCM. CCM ilizaliwa kutokana na muungano wa TANU na ASP ya Zanzibar. Huko nyuma, utaratibu wa mbio za Mwenge wa Uhuru, ulikuwa ukifanywa na Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM).
Mbio za Mwenge wa Uhuru hupita katika nchi, mikoa, wilaya na vitongoji mbalimbali, kwa kufuata falsafa ya Mwenge wa Uhuru, iliyoanzishwa na Mwalimu Nyerere enzi za uhai wake. Humulika palipo na giza na kwa sasa unamulika rushwa na maovu ya watendaji katika ngazi mbalimbali nchini.
Mbio za Mwenge ni kielelezo cha mshikamano Mwenge wa Uhuru umetoa mchango mkubwa katika kudumisha mshikamano wa kitaifa, amani, upendo na umoja miongoni mwa Watanzania.
Vilevile, mbio za Mwenge huo zimeweza kuleta msukumo wa pekee katika maendeleo ya Watanzania, hasa katika shughuli za kiuchumi, kijamii na kiutamaduni. Serikali imekuwa ikihamasisha wananchi na makundi mbalimbali, kuunganisha nguvu, kwa kuchangia kwa hali na mali ili kufanikisha miradi mbalimbali ya maendeleo.
Mwenge huzindua miradi ya kijamii Mbio za Mwenge wa Uhuru zimekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha dira ya maendeleo inapatikana, kwa kuweka nguvu kwenye mapambano dhidi ya Ukimwi na vita dhidi ya umasikini na ukosefu wa ajira kwa vijana.
Mchango wake unajidhihirisha wazi, kwani mbio hizo zimewezesha kuanzishwa kwa miradi mingi ya kijamii. Kwa mujibu wa taarifa za Wizara hiyo mwaka 1961 hadi mwaka 1998, miradi yenye thamani ya Sh bilioni 15 iliweza kuzinduliwa tofauti.
Na tangu mwaka 1998 hadi sasa, miradi mingine ya zaidi ya Sh bilioni 80 imezinduliwa. Miradi hiyo ni sekta ya afya na ujenzi wa shule, kupitia michango ya wadau, wahisani na wananchi wenyewe. Aidha, mbio hizo zimeelekeza nguvu katika Utandawazi, haki ya mtoto iliyopitishwa katika mikataba mbalimbali ya kimataifa.
Pia, mbio hizo zinahimiza umuhimu wa kudumisha amani na upendo wa kweli, vilivyoiwezesha nchi na wananchi wake kuwa ndugu. Kumekuwapo na ushirikishwaji au usawa kijinsia na uhamasishaji wa Watanzania, juu ya masuala mbalimbali ya maendeleo ya kiuchumi kijamii na kiutamaduni.
Ujumbe wa Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka jana, ulizingatia dira, programu, malengo, mikakati na masuala muhimu, yanayowakabili Watanzania na jamii ya Kimataifa. Mbio hizo zinaimarisha juhudi za serikali katika kufikiria nini kifanyike na kwa wakati gani kwa maslahi ya Taifa.
Licha ya vita dhidi ya Ukimwi, Mbio za Mwenge wa Uhuru zimeelekeza vita dhidi ya rushwa, kwa kaulimbiu na hotuba za viongozi katika kila mkoa, wilaya, tarafa, kata, vijiji na maeneo unakopita kukemea kwa dhati wote wanaojihusisha katika vitendo vya rushwa na ufisadi.
Mbio za Mwenge wa Uhuru hutoa elimu kuhusu majanga mbalimbali ya kitaifa, ikiwa ni pamoja na namna ya kufahamu sheria za ardhi, rushwa, mazingira na haki za binadamu ili kutoa fursa kwa wananchi kujua haki zao. Hulinda utamaduni Kwa upande wa utamaduni, ngoma za makabila mbalimbali huchezwa Mwenge unakopita.
Ngoma hizo huwa na nyimbo na maneno ya kukumbusha mila na utamaduni, kwa watu wa rika mbalimbali ili kuhakikisha historia haipotei. Pia, huwapo maonyesho ya bidhaa zilizo za kiutamaduni na zinazolenga kufikisha ujumbe wa kaulimbiu ya mwaka husika.
Waraka wa Mbio za Mwenge ulipitishwa mwaka 2000 na Baraza la Mawaziri ili kuruhusu mabadiliko kadhaa. Waraka huo ulipitisha kuwa katika kilele cha Mbio za Mwenge kila mwaka, kuwe na Wiki ya Maonyesho ya kazi za Vijana na wadau wengine.
Waraka huo pia uliongeza idadi ya wakimbiza Mwenge, kutoka wanne hadi sita, huku msisitizo mkubwa ukiwa ni kwa wanawake, angalau wawe wawili. Suala hili limeimarisha harakati za usawa wa kijinsia.
Hakika Mbio za Mwenge wa Uhuru, zimesaidia kulinda uhuru wa nchi, kupiga vita maadui wa jamii na kuhimiza matumizi mazuri ya rasilimali za nchi kwa faida ya vizazi vijavyo. Mungu Ibariki Tanzania, Mungu wabariki Watanzania.