Tarehe 6 Novemba 2005 nilirejea nchini na British Airways kutokea Heathrow, London, Uingereza nikiwa na mke wangu na mtoto wetu wa kiume baada ya kuishi nje ya nchi kwa miaka kadhaa. Huku Tanzania tuliacha timu kubwa ya watu ambao kabla nilikuwa nikiwaongoza katika huduma za watoto, shule na vijana kupitia Umoja wa Kujisomea Biblia (Scripture Union of Tanzania). Wao waliniona mimi kama kiongozi wao na mimi nilijihisi hivyo.
Siku hiyo tulipowasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Kambarage Nyerere, tulishangaa kukuta umati wa vijana wale wamekuja kutupokea! Furaha na fahari yao ilikuwa ni kumpokea kiongozi wao! Familia ilipisha maandalizi na ratiba yao. Hakukuwa na haja ya kuomba kibari kutoka kwa RPC, OCD, RC, DC wala Meneja wa Uwanja wa Ndege! Simba au Yanga wakitoka mbali kucheza mpira nao hupokelewa na washabiki wao.
Tundu Lissu aliondoka nchini pasipo kuaga na wala hakupenda kuondoka. Mazingira ya kuondoka kwake yalihuzunisha wengi akiwemo Rais ambaye alitoa pole kwake na kumtakia apone haraka. Watu wengi walishiriki kumuombea hata wasiomjua.
Sasa anarejea nchini baada ya kupona! Ndugu zake, rafiki zake, wanachama wenzake na hata watu wengine wasio wanachama wanayo hamu ya kumuona na kumpokea. Lissu sio mhaini. Ni raia wa Tanzania mwenye dhamana ya Uongozi katika Chama chake. Anayo haki ya kupokelewa na mtu ye yote na kupita katika barabara zilizojengwa kwa kodi za Watanzania akiwemo yeye mwenyewe.
Wakati Nyerere anarudi kwao Butiama baada ya kustaafu Urais au kung'atuka, mimi nilikuwa mkazi wa Kipawa. Tulijipanga barabarani kumuaga na wala yeye hakusimama kutuhutubia! Nelson Mandela alipokuja mwaka 1990, mimi nilikuwa mkazi wa Temeke. Tulitoka kila kona ya jiji pasipo kujali mvua kubwa siku ile, tulijipanga barabarani na wala hakutuhubia zaidi ya kufurahia upendo wetu kwake
Vivyo hivyo, kama watu watajitokeza kumpokea Lissu ni haki yao, ni hiari yao, ni uhuru wao, ni mapenzi yao. Wanachotakiwa kufanya ni kuepuka kuwabuguzi wengine au kufanya vitendo vya uhalifu na uvunjifu wa amani.
Viongozi wa CHADEMA wawe makini, wasiruhusu kufanya mkutano wa hadhara pale Uwanja wa Ndege. Watu wasizuie barabara ingawa wanaweza kukaa pembeni mwa barabara. Watu wasizuie wasafiri wengine pale Uwanjani. Polisi wanaweza kuwepo kulinda usalama lakini sio kuwazuia watu wasimpokee kiongozi wao.
Jeshi la Polisi liepuke kufanya jitihatada au maandalizi ya kimkakati kwa lengo la kutaka kuwazuia au kuwatawanya watu wanaokwenda kumpokea kiongozi wao kwa amani. Kufanya hivyo ni kuamsha hisia za watu pasipo sababu ye yote ya msingi. Jeshi la Polisi na Uongozi wa CHADEMA waonyeshe nia njema kwa kushirikiana katika kutunza utulivu na amani siku hiyo.
Katika kipindi hiki ambapo nchi iko katika maombolezo, ni vizuri wote wakiwemo Jeshi la Polisi, viongozi wa CHADEMA na wafuasi wao kuenzi utamaduni wa maombolezo kwa kuwa watulivu. Tahadhari ya Jeshi la Polisi kuhusu 'kusanyiko' la kumpokea Lissu ni muhimu kiusalama, lakini isilenge katika kutaka kuwazuia wala kuwatawanya watu. Jeshi la Polisi lisiwachokoze watu ambao hawajaonyesha dalili za kufanya vurugu! Uwanja wa Ndege siyo sehemu ya kufanyia mikutano ya hadhara. Hivyo haitarajiwi pia kama Lissu ataanza kuhutubia watu mahali pale kama hakuna maandalizi na mawasiliano na mamlaka husika.
NB: Nimeweka picha iliyoandaliwa na JamiiForums ambao ndio waliotoa taarifa kuhusiana na tukio hilo. Picha hiyo imebeba ujumbe wa Jeshi la Polisi kuhusiana na tukio hilo.
Mwana Kondoo Ameshinda! Tumfuate!
Askofu Mkuu Emmaus Bandekile Mwamakula - Mkuu wa Kanisa la Moravian Ia Uamsho Tanzania & Afrika Mashariki na Mwenyekiti Mwenza wa Umoja wa Makanisa ya Moravian ya Uamsho Duniani