RAIS SAMIA AKUTANA NA MTOTO HAMIMU ALIYEMSAIDIA KUPATA MATIBABU YA UGONJWA WA AJABU WA NGOZI.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan leo Jumatano Aprili 26, 2023 amekutana na kuzungumza nae mtoto Hamimu Mustapha Baranyikwa (15) mkazi wa Nyakanazi mkoani Kagera. Mtoto huyo Hamimu alifika Ikulu- Dar es Salaam kwa ajili ya kumshukuru Mhe. Rais kwa msaada aliompatia wa matibabu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili Jijini Dar es Salaam. Rais alimuona mtoto huyo kwa mara ya kwanza wakati wa Ziara yake Nyakanazi Mkoani Kagera tarehe 16 Oktoba, 2022 na kuagiza apatiwe matibabu baada ya kuhangaika kwa muda mrefu.
Mtoto Hamimu aliwatoroka wazazi wake mwaka jana kumfuata Rais Samia ili kuokoa maisha yake baada ya kuhangaika kwa muda mrefu na ugonjwa wa ajabu wa ngozi ambapo ngozi yake ilikuwa imeharibika vibaya sana.
Wazazi walimkataza kutoka nje kuhofia watu watamkimbia au kumpiga kutokana na ugonjwa wake wa ajabu wa ngozi waliohangaika nao sana na kukata tamaa.
"Nilisikia Rais Samia anapita Nyakanazi na mimi kwetu ni pale pale Nyakanazi. Wazazi walinikataza, wewe usiende na hali hiyo uliyokua nayo watu wanakukimbia. Unaenda kufanya nini, watakupiga."
Mtoto huyo alienda kwenye mkutano huo wa Rais Samia Nyakanazi ndipo Rais Samia alipomuona na kutoa maelekezo atibiwe haraka na kugharamia matibabu yake yote.
Hamimu, ambaye wazazi wake walihangaika kumpeleka kwa waganga wa kienyeji na hata kuuza mali za familia bila mafanikio, alikuwa amekata tamaa kama angekuja kupona ugonjwa wake wa ajabu
Ngozi yake ilikuwa imeharibika, uso wake ukawa hautazamiki hadi watu wazima na watoto wakawa wanamkimbia na alishindwa hata kukunja na kukunjua vidole vya mikono yake kutokana na maradhi hayo.
Wahenga wanasema penye nia pana njia. Rais Samia Suluhu Hassan alipofika Nyakanazi wakati wa ziara yake ya mkoa wa Kagera, alimuona mtoto huyo amekaa pembeni ya barabara akiwa amenyong'onyea akawatuma wasaidizi wake waende kuongea naye wajue tatizo lake ni nini.
"Nilipofika nikakaa pembezoni mwa barabara. Ule msafara wake (Rais Samia) ulipofika, yale magari yake wakaniona. Waliokuwa wanaongozana naye (Rais) wakaniuliza maswali... Kuna mmoja aliyekuwa ameongozana nao ni dokta, akanishika ngozi yangu," alisema Hamimu.
Kwa mujibu wa kijana huyo, daktari aliyekuwepo kwenye msafara wa Rais Samia akasema kuwa akipelekwa Muhimbili wanaweza kujua chanzo cha ugonjwa wake wa ngozi na kumpatia matibabu sahihi.
Kufuatia ushauri wa daktari, Samia aliagiza mtoto huyo asafirishwe haraka kutoka Nyakanazi hadi hospitali ya Taifa ya Rufaa ya Muhimbili iliyopo Dar es Salaam kwa uchunguzi na matibabu.
Siku chache baada ya maagizo ya Rais, Hamimu akaanza kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Muhimbili tarehe 21 Oktoba, 2022.
Hamimu alilazwa Muhimbili kwa matibabu kwa muda wa miezi sita kwa msaada wa Rais Samia.
Ilipofika tarehe 19 Aprili 2023, madaktari wake wakajiridhisha kuwa sasa mtoto huyo amepona na anaweza kurudi nyumbani kwao mkoani Kagera.
Kabla ya kurudi kwao Kagera, Hamimu aliomba aonane na Rais Samia kumpa shukrani zake uso kwa uso na ndipo leo Jumatano amekutana nae Ikulu kwenda kumshukuru Rais Samia kwa kuokoa maisha yake.
"Sidhani kama ningepona. Ilifika hatua nikasema, mniache nife. Kwa jinsi nilivyohangaika kupona ilishashindikana. Isingekuwa yeye (Rais Samia) mimi mpaka muda huu sidhani kama ningekuwa hai."