Mimi namuonea huruma huyo dereva kufanya mauaji hadharani kwani wanaomshabikia hapo kwenye eneo la tukio na huku mitandaoni hawatakuwepo iwapo mambo yataenda mahakamani. Kwa kitendo chake cha kurudia kumkanyaga huyo anayesemekana mwizi mara tatu mfulululizo tafsiri yake ni kuua kwa kukusudia kabisa. Huyo mwizi kama ana ndugu zake waelewa basi huyo dereva atakuwa na hali ngumu sana kisheria na si ajabu maisha yake yote yaliyobaki hapa duniani akayamalizia nyuma ya nondo. Wezi kama hawa usijifanye sana wewe ndio bingwa peke yako unajua kuua wengine wakae pembeni acha mumpige watu wengi mpaka afe hata polisi wakifika wanashindwa wamkamate nani na waanzie wapi uchunguzi wao. Polisi wakishathibitisha tu kuwa ni kibaka wanaishia tu kuandika taarifa na kuutangazia umma kuwa mtu mmoja aliyesadikiwa kuwa kibaka kauwawa na wananchi wenye hasira kali.
Mimi siwapendi kabisa vibaka kwani walishaniibia wakati naanza maisha hapo zamani kidogo. Na ilinichukua muda kurudi kukaa sawa. Lakini angalizo langu kubwa ni kuwa huku kuchukua sheria mikononi wakati mwingine sio sahihi sana kwa sababu ya matukio yaliyowahi kutokea kipindi cha nyuma. Kuna watu wameuwawa wakati ni watu wema kabisa lakini wakasingiziwa na kupigiwa kelele za mwizi. Baadaye ukweli unakuja kujulikana ni ugomvi wa kimapenzi, pesa, mali, ugomvi wa barabarani, madeni n.k. wakati huo mtu ameshapoteza maisha. Na watu wengi tukishasikia kelele za mwizi huwa hatujiulizi mara mbili zaidi mwenye panga haya, mwenye rungu haya, mwenye beleshi haya, mwenye sururu haya, mwenye sime haya,n.k. Na mbaya zaidi hakuna nafasi ya kujitetea kati ya kelele za mwizi na watu kuanzia kutoa kipigo kwani hata ujieleze vipi hakuna anayekusikiliza. Ndio maana hata huyo jamaa aliyekuwa anakanyagwa na gari kila mtu anaelezalake mara mwizi wa piki piki, mara simu mwisho wa siku usijeshangaa ukaambiwa jamaa hana hatia wakati jamaa kashakata pumzi.
Iliwahi kutokea takribani miaka 10 iliyopita jamaa kama watatu wakawa wanamkimbiza jamaa mpaka mtaani kwetu wanapiga kelele mwizi huyo. Basi kama kawaida wananzengo wakamkamata na kuanza kumshushi kipigo. Bahati nzuri ilikuwa mchana (ogopa kibaka akamatwe usijku hapo hata shoka linatumika) kwa hiyo watu wakawa wanampiga tu ngumi na mateke. Jamaa kila akijitetea wapi watu wanashusha kipigo. Jamaa kumbe Mungu anampenda ghafla muda huo huo wakatokea askari wakazuia watu wasimuadhibu halafu wakauliza jamani kaiba nini na ni nani aliyeibiwa hapa. Aisee kuangalia jamaa watatu waliokuwa wanamfukuza na kumpigia kelele za mwizi hawapo hata mmoja. Tukabaki na aibu zetu tunaangaliana wote. Jamaa kuulizwa vipi we umeiba nini huwezi amini jamaa kuanza kueleza akasema wale jamaa watatu ndio vibaka wamemuibia simu na pochi halafu wakaanza kumpiga jamaa kujitetea akaanza kukimbia ndipo jamaa wakamuanzishia mwizi huyo mwizi huyo. Ilibidi polisi watupe darasa kidogo na kutonya ilivyo hatari kuchukuwa sheria mkononi. Na wakatuambia kabisa iwapo jamaa angekufa bila hatia basi tusingekwepa mkono mrefu wa dola kwa njia yoyote ile. Na hapo Mungu saidia jamaa alikuwa hakupigwa sana kwani ndio kwanza wananzengo walikuwa wameanza kupiga kabla polisi hawajaja kumuokoa. Aisee kuanzia siku hiyo kila aliyekuwapo kwenye tukio alikuwa anaomba Mungu jamaa asiwe kapata madhara makubwa. Kila askari wakipita mtaani na shughuli zao ilikuwa mshikemshike tunaiona ohooo kumekucha wamekuja kutuchukuwa watuhumiwa lakini Mungu saidia hayo mambo yaliisha kimya kimya.