HOTUBA YA MWENYEKITI WA CHAMA NGAZI YA WILAYA KWENYE MKUTANO MKUU WA WILAYA TAREHE 13 JULAI, 2020.
UTANGULIZI
Ndugu zangu wajumbe wa Mkutano Mkuu na wageni wetu waalikwa, wenzangu wakristo Bwana Yesu Asifiwe! wenzetu waislam; Asalaam Aleikum! Awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu na mwingi wa Rehma aliyetuwezesha tena siku ya leo kukutana mahali hapa kwa ajili ya ujenzi wa chama chetu kinachozidi kuwa tishio kubwa sana kwa uhai wa CCM na serikali yao.
Ni kipindi cha zaidi ya mwaka mzima na nusu sasa, tangu tulipoagana kwenye ukumbi huu baada ya kuhitimisha uchaguzi wa ndani ya chama mwanzoni mwa mwaka jana 2019 mwezi wa Februari. Kipekee kwa niaba ya viongozi wenzangu wote wa chama ngazi ya wilaya, nitumie fursa hii kuwashukuru sana kwa kura nyingi mlizotupatia na hatimaye mkatukabidhi jukumu hili zito la kukiongoza chama kwa wilaya nzima yenye vitongoji 361, vijiji 78 na kata zipatazo 30.
Ndugu zangu wajumbe wa Mkutano Mkuu, tangu kipindi hicho chote ambacho mlikitumia kutukabidhi majukumu; mimi Mwenyekiti wa Wilaya kwa kushirikiana na viongozi wenzangu wote wa wilaya na wale wa ngazi mbalimbali za chama, tumeendelea kukitumikia kwa uadilifu mkubwa, huku tukihakikisha kwamba, chama kinaendelea kuimaarika na kuwa na mtandao mpana na imara zaidi katika maeneo yote ya wilaya yetu ikiwemo huko kwenye kata zetu, matawini na hata kule chini kabisa vitongojini kwa maana ya kwenye misingi.
Tumepokea kijiti hiki cha uongozi wa chama katika kipindi kizito cha miaka miwili mfululizo ya chaguzi za kukabiliana na dola ya CCM na watu wake, lakini nataka niwahakikishie kwamba, hatuwezi kuwaangusha. Na katika kuhakikisha kwamba hatuwaangushi, tunaomba support yenu ya kutosha kwenye mapambano ya kuikabili na kuidhibiti CCM na watu wake nyakati za chaguzi kama hizi zilizoko mbele yetu, hasa pale watakapoanza kuleta janja janja kwenye michakato ya uchaguzi huu.
Tunaporejea tena huko katani na vijijini kwetu baada ya uchaguzi huu wa ndani ya chama, niwaombe na niwasisitize sana, nendeni mkaanze mara moja mikakati ya kuishughulikia CCM huko chini huku mkitambua kwamba, huku juu tumejipanga ipasavyo kuingia vitani na ni lazima tuwashinde tena iwe wanataka ama hawataki.
HAMA HAMA YA VIONGOZI WA CHAMA NA WANACHAMA
Ndugu zangu wajumbe wa Mkutano Mkuu, katika kipindi ambacho mmetukabidhi chama, tumeendelea kukabiliana na changamoto ya viongozi wa chama na wanachama wetu kukihama chama kwenda vyama vingine vya siasa hasa CCM kwa kile kinachoitwa kuunga mkono juhudi za Rais.
Katika kipindi chote hicho hadi leo hii tunapokutana hapa, wapo viongozi na wanachama mbalimbali ambao wamekuwa wakihamia CCM na vyama vingine kimya kimya kwa kigezo hicho hicho cha kuunga juhudi pasipo kutoa taarifa zozote ndani ya chama na wapo ambao hawaeleweki misimamo yao kama wamesimama wapi.
Pamoja na uwepo wa hatua hiyo ya hamahama ya viongozi na wanachama kutoka kwenye chama kwenda CCM na vyama vingine, chama chetu kimeendelea kuwa imara na tishio kubwa sana kwa CCM na Serikali yao kuliko wakati mwingine wowote ule.
SERA YA CHAMA YA JIMBO
Ndugu zangu wajumbe wa Mkutano Mkuu, chama ngazi ya wilaya kupitia sekretarieti ya chama, tumeandaa sera za chama za jimbo letu ambazo zitatumiwa na wagombea wetu wa Udiwani na Ubunge; wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka huu zitakazoanza mwezi ujao.
Sera hizi za jimbo letu; ni zao la sera za chama ngazi ya taifa na zimeeleza zaidi chama kitafanya nini kwenye maeneo mahalia ya jimbo ama wilaya yetu, endapo kitapewa ridhaa ya kuongoza Jimbo na Halmashauri yetu kupitia kwa Wagombea wake wa Udiwani na Ubunge.
Sera zimejikita zaidi katika kufafanua mambo kadha wa kadha yaliyoainishwa kwenye sera za chama ngazi ya taifa. Mojawapo ya mambo yaliyoainishwa kwenye sera za jimbo letu ni pamoja na haya yafuatayo;
Katiba Mpya, Huduma za Afya, Sekta ya Mifugo, Kilimo na Soko la Mazao ya Kilimo, Maji, Miundombinu, Sekta ya Utalii, Agenda ya Ajira, Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Masuala ya Waalimu, Haki za Binadamu, Uhuru wa kujieleza, Utoaji Haki, Utawala wa Sheria na Utawala Bora.
Pia Sera hizo zimeeleza kwa kina kuhusu; Uchumi wa Viwanda wenye tija, Usimamizi wa Sekta ya Madini, Ushirikishwaji wa Jamii katika maamuzi, Ukuaji wa Miji na Maendeleo Vijijini, Usimamizi wa Ardhi na Utatuzi wa Migogoro ya Ardhi.
SARE ZA CHAMA, BENDERA NA KADI ZA CHAMA
1: SARE ZA CHAMA
Ndugu zangu wajumbe wa Mkutano Mkuu, natoa wito kwa wanachama na viongozi wote wa chama kuwa na utaratibu endelevu wa uvaaji wa sare za chama wakati wote hususani katika kipindi chote cha uchaguzi na hata baada ya uchaguzi kama ilivyo kawaida yetu kama chama.
Kwenye hatua hii ya uvaaji wa sare za chama, kipekee sana nimpongeze Mbunge wetu Mstaafu wa Viti Maalum Mhe.Catherine Ruge kwa moyo na jitihada zake kubwa za kipekee alizofanya kwa ajili ya chama kuhakikisha kwamba, zaidi ya 90% ya viongozi wetu wa chama wa kata karibu wote wanapata sare za chama kwa maana ya vitenge kwa akina Mama wa Bawacha na t-Shirt kwa viongozi karibu wote wa Kata na hata kwa baadhi ya wanachama wa kawaida kabisa wasio viongozi.
Kwa wale ambao hamjapata vitenge na t-shirt, naamini Mbunge atakuwa anaendelea kutafakari la kufanya ili wote muweze kupata sare zenu; isipokuwa kwa wale ambao wanahitaji kuzipata kwa gharama zao, sare ni nyingi sana na Diwani Mstaafu Mhe.Edina Ngereza ameanzisha Branch ya kuuza hizi sare hapa Mugumu Mjini, hivyo kwa yeyote aliye na uhitaji, anaweza kuwasiliana naye kwa msaada zaidi.
Ni vyema ieleweke wazi kwamba, hakuna wakati wananchi waliwahi kutamani kuwaona watu wa chadema wakiwa kwenye sare za chama kama wakati huu. Na wananchi walio wengi hivi sasa wanatamani sana kupata sare za chama chetu ili wazivae lakini wengi wao wanashindwa kutokana na gharama za sare hizi ama wengine kutojua jinsi ya kuzipata kwa urahisi, naamini hata ninyi wenyewe ni mashahidi wa hilo huko kwenye maeneo yenu mnayotokea.
2: BENDERA ZA CHAMA
Ndugu zangu wajumbe wa Mkutano Mkuu, kama chama ngazi ya wilaya tunao uhaba mkubwa sana wa Bendera za chama na tunatambua uhitaji mkubwa sana wa Bendera uliopo karibu maeneo yote ya wilaya yetu. Natoa wito kwa viongozi wote wa chama wa ngazi za kata, matawi na misingi kuendeleza ule utamaduni wetu wa kupeperusha Bendera za chama kwenye maeneo yetu yote.
Sisi kama Chama ngazi ya Wilaya kwa kushirikiana na viongozi wenzetu wa ngazi zingine za juu ndani ya chama, tunaendelea kufuatilia juu ya namna ya kupata Bendera za kutosha hasa katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu ambako kutakuwa na hitaji kubwa sana la Bendera kila kona ya jimbo letu. Tunaendelea kufanya mazungumzo na wadau mbalimbali kuona namna ya kulifanikisha jambo hili kwa wakati.
Aidha, chama kinatambua uwepo wa changamoto ya baadhi ya viongozi wa CCM na wale wa serikali kushusha Bendera za chama ama wakati mwingine wamekuwa wakiwaamuru viongozi wetu wa chama wakashushe Bendera za chama ili zibaki za CCM peke yake zikipepea. Huu ni ushenzi uliopita kiwango.
Kupitia Mkutano huu wa chama, natoa wito kwenu wote kuukataa na kuupinga ushenzi wa kiwango hiki kwa gharama zozote zile ili kuilinda heshima ya chama, na kila mmoja wetu alazimike kuwa na wivu dhidi ya chama hiki tunachokijenga kwa gharama kubwa sana hata za jasho na damu zetu.
Ifike wakati, wapuuzi wachache wanaotaka kukidharirisha chama wajikute katika wakati mgumu na iwe fundisho kwa wale wote wanaowatuma kufanya hivyo. Katika suala hili sitanii, nasisitiza tushughulike na tutakayemkuta kwenye eneo la tukio ama yeyote atakayebainika kufanya hivyo, hatuna muda mchafu wa kupoteza kwa kuwachekea watu wa CCM tena, anayedhani wale ni binadamu wa kawaida, amechelewa sana kusoma alama za nyakati.
3: KADI ZA CHAMA
Ndugu zangu wajumbe wa Mkutano Mkuu; kama chama hadi kufikia leo hii tunapokutana hapa tunaweza kusema, angalau tatizo la kadi kwa kiwango fulani tumeweza kukabiliana nalo na karibu maeneo mengi yana kadi za kutosha na yale maeneo machache ambayo hayana kadi, ni uzembe wa viongozi wa maeneo hayo kutofanya ufuatiliaji wa masuala yahusuyo chama kwenye ngazi zingine za chama.
Pamoja na udhibiti huo wa tatizo la kadi za chama tulioufanya, napenda kutumia nafasi hii kuwajulisha kwamba, chama chetu kimeingia kwenye hatua nyingine ya kisasa zaidi katika uendeshaji wa shughuli za chama, hivyo chama kimelazimika kubadili kadi za chama kutoka hizi kadi za karatasi na kuwa na kadi za kielekroniki maarufu kama kadi za plastiki zinazofanana na kadi za kupigia kura kimuundo.
Hivyo basi, kutokana na mabadiliko hayo ya kadi, chama kinaandaa utaratibu wa kuwasajili viongozi na wanachama wote kwa nchi nzima ili wapate kadi hizo lakini kwa sharti la kila mmoja wetu kulipia gharama za uchapaji wa kadi yake kadri chama kitakavyoamua bei ya uchapaji iwe kiwango gani.
Aidha, chama kupitia vikao vya juu kwa maana ya Baraza Kuu na Mkutano wa Chama uliokutana Jijini Dar Es Salaam mwishoni mwa mwaka jana 2019, iliazimiwa kuwa, ada ya kila Mwanachama iwe Tsh.2,500 kwa mwaka mzima, badala ya ada iliyopo sasa; na ada hii mpya itakuwa inalipwa kwa njia za kielekroniki hata kupitia njia za benki na huduma za simu za mkononi kama vile Airtel Money, M-Pesa, TigoPesa, Halopesa n.k.
MPANGO WA KUJENGA OFISI YA KISASA YA CHAMA HAPA WILAYANI
Ndugu zangu wajumbe wa Mkutano Mkuu; pamoja na uzito wa haya majukumu mazito ya ujenzi wa mtandao imara wa chama tuliyonayo hapa wilayani, ujenzi wa ofisi ya chama ya wilaya ni miongoni mwa majukumu hayo mazito tuliyoyapa kipaumbele ndani ya chama kwa sasa. Katika hatua za awali, tumeanza na mpango wa namna ya kupata fedha za kununua uwanja wa ofisi hii na hatimaye tutaanza hatua za ujenzi wa msingi wa ofisi na kuanza kupandisha kuta zake kadri ya upatikanaji wa fedha kutoka kwenye vyanzo tulivyoona kwamba, vinaweza kuwa vya uhakika kutuwezesha kupata fedha.
Mojawapo ya vyanzo vyetu vya uhakika tunavyovitegemea kupata fedha za uwanja wa ofisi hii kama mipango yetu itakwenda sawa kama tulivyoipanga ni pamoja na; waheshimiwa madiwani wetu wastaafu waliomaliza muda wao salama wakiwa waaminifu na watiifu kwa chama na chanzo kingine cha pili ni Mbunge wetu wa viti maalum Mhe.Catherine Ruge ambaye ametoa ahadi ya kuichangia ofisi hii fedha kiasi cha shilingi millioni moja na laki tano na amesema mbele ya vikao vyetu kuwa; kabla ya kuanza kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka huu kwa maana ya kabla ya mwezi wa nane ujao atakuwa ameiweka fedha hii kwenye akaunti ya chama.
Baada ya Mbunge Catherine kuahidi kiwango hicho cha millioni moja na laki tano, waheshimiwa madiwani nao kupitia umoja wetu wa madiwani hatukubaki nyuma, na tumeahidi kukichangia chama kiasi cha shilingi millioni tano na laki tano kwa viwango tofauti tofauti kwa kila mmoja wetu na fedha hii italipwa mara tu baada ya kila Diwani kupokea fedha zake za pensheni ya uwakilishi ndani mwezi huu wa saba ama mwezi wa nane ujao.
UCHAGUZI ULIOPITA WA SERIKALI ZA MITAA 2019.
Ndugu zangu wajumbe wa Mkutano Mkuu, itakumbukwa kwamba, mwishoni mwa mwaka jana 2019 kulikuwepo na uchaguzi wa serikali za mitaa ambao baadae chama chetu kilijitoa kwenye uchaguzi huo kutokana na dosari nyingi zilizojitokeza wakati wa michakato ya uchaguzi wenyewe.
Wakati wa kutangaza uamuzi wa chama wa kujitoa kwenye uchaguzi ule uliogubikwa na hila nyingi zilizokuwa na lengo la kuibeba CCM iliyokuwa inakwenda kuangukia pua vibaya sana, Mwenyekiti wa Chama Taifa Mhe.Freeman Aikael Mbowe alisema maneno yafuatayo;
”Katika misingi hii ndugu watanzania, tumelazimika kukaa na kutafakari, baada ya vikao tulivyofanya kwa siku nzima ya leo, tumeamua kutobariki uchaguzi huu, ubatili umefanywa na serikali, na chama cha mapinduzi, sisi kama chama hatutashiriki katika uchaguzi huu na hatuko tayari kujihusisha na ubatili".
”Tunawajua viongozi wengi wa chama cha mapinduzi ambao hata kusoma wala kuandika hawajui, jiji la Dar es salaam pekee tulikua na mitaa zaidi ya 500, lakini wamekatwa na kubaki mitaa 24, hali ni hiyo hiyo katika Vitongoji, Vijiji na Mitaa ya Miji, Halmashauri, Manispaa na Majiji yote kwa Nchi nzima.
Ndugu wajumbe wa Mkutano Mkuu, pamoja na changamoto kubwa ya utaratibu mbovu wa zoezi la uchukuaji na urejeshaji wa fomu za wagombea wa uchaguzi wa serikali za mitaa uliokuwepo kwenye ofisi za watendaji wa vijiji na kata mwaka jana 2019; katika wilaya yetu ya serengeti yenye vijiji 78 na vitongoji 361, mpaka tarehe ya mwisho ya kurejesha fomu za wagombea wa vijiji na vitongoji, sisi chadema tulifanikiwa kusimamisha wagombea wa vijiji 70 kati ya vijiji 78 vya wilaya nzima na tulifanikiwa kusimamisha wagombea wa vitongoji 318 kati ya vitongoji 361 vya wilaya nzima.
Ikilinganishwa na uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka 2014 ambao chama chetu kilikosa wagombea katika vijiji 14 kati ya vijiji 78; na katika uchaguzi huo wa mwaka 2014 wa serikali za mitaa, chama chetu kilikosa wagombea katika vitongoji 50 kati ya vitongoji 361 vya wilaya nzima. Kwa idadi hiyo, imekuwa tofauti kabisa na uchaguzi wa mwaka jana 2014. Chama chetu kimeonekana kufanya vizuri zaidi pamaja na kwamba; mazingira ya kushiriki uchaguzi ule hayakuwa rafiki.
Mpaka siku ya mwisho ya wagombea wetu kurejesha fomu zao kwenye ofisi za serikali, tulikuwa tumekosa wagombea wa vijiji 8 pekee kati ya vijiji 78 ikilingaishwa na uchaguzi wa mwaka 2014 ambao tulikosa wagombea kwenye vijiji 14. Aidha, tulikosa wagombea 43 pekee kati ya vitongoji 361 vya wilaya nzima, ikilinganishwa na uchaguzi uliopita wa 2014 ambao tulikosa wagombea kwenye vitongoji 50.
Ndugu wajumbe wa Mkutano Mkuu, zipo sababu nyingi sana zilizodhibitisha ni kwa kiwango gani mazingira ya uchaguzi ule hayakuwa rafiki na hata yakapelekea chama chetu kukosa wagombea kwa maeneo ya vijiji na vitongoji kadhaa nilivyovitaja hapo juu; naamini hata ninyi ni mashahidi wa jambo hili kutokana na ukweli kwamba, matukio mengi hasa yale ya watendaji wa serikali kutoroka maofisini ili wagombea wa chama chetu wakose fursa ya kurejesha fomu zao.
Kwa maksudi kabisa; na kwa sababu watendaji wa serikali walikuwa na maelekezo ya kuisaidia CCM ishinde, kwa maana ya “ushindi wa mezani”, waliamua kuendesha uchaguzi kinyume kabisa na misingi ya sheria, kanuni, miongozo na taratibu za uchaguzi ule, na ndio sababu sisi kama chama, hatukuona umuhimu wa kuushiriki maana kuushiriki ilikuwa ni kuunga mkono; na kuwa sehemu ya kuuhalalisha ubatili uliokuwa unafanyika.
Baada ya CCM na watu wao kugundua kwamba; tunakwenda kuwashinda vibaya sana kwenye Uchaguzi ule, wakaamua kuomba msaada wa mbeleko ya Tume ya Uchaguzi kupitia kwa watendaji wa vijiji na kata na wakawaengua wagombea wetu wote 69 wa vijiji kati 70 tuliofanikiwa kuwasimamisha kwenye vijiji na wakaamua kumpitisha mgombea mmoja pekee wa kijiji aliyetokana na chama chetu ambaye ni Mugaya Rhobi Bugau wa kijiji cha Kerukerege kilichopo katika Kata ya Nyambureti. Aidha, wakaamua kuwapitisha wagombea17 pekee wa vitongoji kati ya wagombea 318 tuliofanikiwa kuwasimamisha.
Ndugu zangu wajumbe wa Mkutano Mkuu, hata mara baada ya chama chetu kujitoa kwenye uchaguzi ule, sisi kama wilaya tulianza maandalizi ya kujipanga na uchaguzi Mkuu ambao leo hii tunatakiwa kumchagua mgombea wa nafasi ya Ubunge, hatimaye tutarejea kwenye Kata zetu kwa ajili ya kukamilisha michakato ya kuwachagua wagombea wa Udiwani kwenye Kata zetu na wale wa viti maalum ambao michakato yao itaratibiwa na kusimamiwa na kamati ya tendaji ya Baraza la wanawake ngazi ya wilaya kuanzia tarehe 19 Julai, 2020 hadi tarehe 20 Julai, 2020 ambako Kamati tendaji ya Bawacha wilaya itakutana kwa ajili ya usaili wa wagombea wote wa viti maalum na kesho yake ufanyike Mkutano Mkuu wa Bawacha kwa ajili ya uchaguzi wao.
Aidha, ili kuhakikisha kwamba watu wetu wanajiandaa vyema kudhibiti na kukabiliana na hujuma zote za CCM zilizojitokeza kwenye uchaguzi haramu wa serikali za mitaa uliopita; chama kinaendelea kujipanga kadri inavyostahili na katika uchaguzi huu, ushindi ni lazima kwa chama chetu; iwe CCM wanataka ama hawataki kama nilivyosema mwanzo.
Ni vyema kila mmoja atambue kwamba, uchaguzi huu hatuna muda wa kubembelezana na CCM ama vibaraka wao.Kazi yetu ni moja tu; tunakwenda kutafuta ushindi wa wagombea wa chama chetu kwenye Kata zote na jimbo zima.
MICHAKATO YA UCHAGUZI MKUU WA MWAKA 2020
Ndugu zangu wajumbe wa Mkutano, kupitia nafasi hii fupi, nitoe wito tukaisimamie michakato hii ya kuwapata wagombea wa Udiwani kwenye kata zetu kwa kuitisha mikutano mikuu ya kata zetu ndani ya muda uliopangwa ambao ni kati ya tarehe 15 Julai, 2020 hadi tarehe 18 Julai, 2020.
Na kila mmoja wetu atambue kwamba, uchaguzi wa mwaka huu, hakuna wa kujitoa; na kama chama tumejipanga kushiriki uchaguzi katika mazingira yoyote yale ambayo CCM na watu wao wataamua na tutawashinda kwa kishindo hawatakaa waamini.
Vile vile, nitoe wito kwa kamati ya utendaji ya Baraza la wanawake kuuzingatia muda huo uliopangwa na waitishe vikao vya Baraza lao kwa wakati ili kuukamilisha mchakato huu wa kuwapata wagombea wa nafasi za Udiwani wa viti maalum.
Ili kukimbizana na ratiba nzito iliyoko mbele yetu; kama nilivyosema hapo awali, kamati tendaji ya Bawacha ngazi ya wilaya italazimika kukutana tarehe 19 Julai, 2020 kwa ajili ya usaili wa watia nia wote wa Udiwani wa viti maalum na kesho yake tarehe 20 Julai, 2020 utafanyika Mkutano Mkuu wa Bawacha kwa wilaya nzima hapa Mugumu, kwa ajili ya uchaguzi wa madiwani wa viti maalum.
MICHAKATO YA KUCHUKUA, KUJAZA NA KUREJESHA FOMU
Ndugu zangu wajumbe wa Mkutano Mkuu, baada ya michakato yote ya kuwapata wagombea wa Ubunge, Udiwani wa Kata na wale wa viti maalum ndani ya chama, tutaingia kwenye mchakato mwingine wa kuchukua, kujaza na kurejesha fomu za serikali kwenye ofisi za watendaji wa kata zetu kwa upande wa madiwani na hatimaye kwenye ofisi ya Mkurugenzi wa wilaya kwa upande wa fomu ya Ubunge.
Katika michakato yote hii, nasisitiza umakini mkubwa sana hasa wakati wa kuichukua fomu, wakati wa kuijaza na wakati wa kuirejesha fomu husika. Katika hatua hii ya kuichukua fomu, kila mgombea, viongozi wa chama wa kata husika, kampeni meneja na wasaidizi wengine wote wa mgombea, watalazimika kuwa makini zaidi katika kufuata na kuzingatia kanuni, taratibu na miongozo ya uchaguzi inasema nini wakati wa kuchukua, kujaza na kuirejesha fomu ya mgombea ofisini kwa mtendaji wa kata husika.
Na kila mmoja kwa nafasi yake ahakikishe anatimiza wajibu wa kufuatilia na kujua kanuni, taratibu na miongozo ya uchaguzi huu inaelekeza nini kifanyike kwa kila hatua ili sote tushirikiane huku tukiwa na uelewa mpana wa haya mambo kuepuka watendaji wa kata kutuingiza chaka kizembe kwa maslahi ya waliowabeba migongoni mwao.
Aidha, katika hatua hiyo ya kuchukua fomu, wahusika wote niliowataja hapo juu watalazimika kuziba mianya yote ya wagombea feki kuchukua fomu za Udiwani na hata Ubunge ili kutafuta hoja ya kuwanyima fomu wagombea wetu halali walioteuliwa na chama.
Ndugu zangu wajumbe wa Mkutano Mkuu, kama nilivyosema mwanzo, uchaguzi huu hakuna wa kujitoa na chama kimejiandaa vya kutosha kushiriki uchaguzi huu katika mazingira ya aina yoyote ile; hii ni pamoja na ukweli kwamba, hata Tume hii ya Uchaguzi ipo kwa ajili ya kutaka kuibeba CCM Mgongoni; na awamu hii tumeamua, hatutakubari kuruhusu hujuma zozote zile zitokee kizembe hata kwa gharama nzito ya kiwango gani.
Ni vyema kila mmoja wetu atambue kwamba, Tume hii ya uchaguzi iliyojipanga kuibeba CCM ni hao watendaji wote wa serikali watakaokabidhiwa majukumu ya kuratibu na kusimamia uchaguzi huu.
Hivyo basi, chama kinatoa wito kwetu sisi viongozi wa maeneo husika kuhakikisha kwamba, tunakabiliana na hujuma za aina yoyote ile kupitia nguvu ya umma tuliyonayo na kuhakikisha kwamba, haki za wagombea wetu zinapatikana kule kule kwenye maeneo husika ya uchaguzi hasa humo humo kwenye maofisi ya watendaji.
Ndugu zangu wajumbe wa Mkutano Mkuu, uchaguzi huu ni ama sisi chadema tushinde ama wao CCM washindwe. Hivyo basi, kwa kuwa tumedhamiria kuwashinda CCM iwe wanataka au hawataki, ni lazima kila mmoja wetu awe sehemu ya kuufanikisha ushindi huu wa kishindo huko kwenye kata zetu na hatimaye kwenye jimbo kwa maana ya mbunge.
Nendeni huko vijijini na kwenye kata zetu tukajipange dhidi ya kulinda kura zetu katika mazingira yoyote yale mpaka washindi wa chama chetu waweze kutangazwa pale itakapoonekana kwamba wameshinda uchaguzi na si vinginevyo.
Sisi kama chama ngazi ya wilaya tutaendelea kuutimiza wajibu wetu unaostahili na kwa wakati sahihi katika nyanja zote; lengo letu kubwa likiwa ni kuhakikisha kwamba, hakuna mtu au watu wetu watakaoonewa ama kunyanyaswa na mtu au watu wa CCM na vibaraka wao wakati wakiutimiza wajibu wao wa kuipigania haki katika uchaguzi huu.
Na katika kuliweka sawa suala hili, tunawataka CCM na walioko nyuma yao watambue kwamba, katika uchaguzi huu, endapo kwa maksudi wataamua kutozingatia kanuni, taratibu na miongozo ya uchaguzi na wakaanza kuwaonea ama kuwanyanyasa watu wetu kwa namna yoyote ile, tutakula nao sahani moja na watajikuta katika wakati mgumu pasipo kutarajia na hatutanii katika suala hili.
ULINZI WA KURA ZA WAGOMBEA WA CHAMA (DIWANI, MBUNGE NA RAIS) PAMOJA NA MAWAKALA WA CHAMA CHETU.
Ndugu zangu wajumbe wa Mkutano Mkuu, wakati wa kulinda kura za wagombea wetu wa chama, hakikisheni pia mnaweka utaratibu mzuri wa kuwapa uylinzi wa kutosha mawakala wetu watakaokuwa vituoni ili kudhibiti hujuma za watu wa CCM ama wale wanaojifanya kwamba ni maafisa wa Tume kuwatisha na kuwazongazonga mawakala wetu ili kuwatia hofu kwa lengo la kufanikishe mipango na nia zao ovu za kutaka kuiba kura vituoni.
Hakikisheni mnapinga na kudhitibiti ipasavyo hila na hujuma za aina hiyo na ikibidi mhusika au wahusika wafundishwe taratibu za uchaguzi zinasema nini kwa vitendo.
MICHAKATO YA KAMPENI ZA UCHAGUZI MKUU WA UDIWANI, UBUNGE NA URAIS.
Ndugu zangu wajumbe wa Mkutano, kama nilivyosema hapo mwanzo; kuhusu mchakato wa kuchukua, kujaza na kurejesha fomu za wagombea wetu, pia tutakuwa na michakato ya kampeni za uchaguzi huu itakayohusisha kampeni za Udiwani, Ubunge na Urais.
Katika hatua hii, wagombea wote wa Udiwani na Ubunge, watalazimika kuendesha kampeni za mtu kwa mtu, nyumba kwa nyumba, kitongoji kwa kitongoji, kijiji kwa kijiji na hatimaye kampeni za majukwaani ili kuelezea sera za chama na kuomba kura kwa wapigakura.
Ndugu zangu wajumbe wa Mkutano Mkuu, twendeni tukashiriki uchaguzi huu huku tukiwa kifua mbele kwa sababu chama chetu chadema kinakubalika mbele za wananchi wa maeneo yetu (wenye vyama na wasio na vyama) kuliko wakati mwingine wowote ule na hata CCM na serikali yao wanalitambua hilo, na ndio maana kwa kipindi chote cha miaka mitano, serikali ya CCM imetumia Nguvu kubwa sana ya vyombo vya dola kutuzuia tusikutane na wananchi kwenye mikutano ya hadhara.
Ninachotaka kuwaambieni, wananchi wa maeneo yetu wanayo hamu kubwa sana ya kutusikiliza kuliko tunavyoweza kudhani.
HOJA YA WASHINDI WETU WA UDIWANI, UBUNGE NA URAIS KWAMBA HATA WAKISHINDA HAWATANGAZWI.
Ndugu zangu Wajumbe wa Mkutano Mkuu, katika kipindi chote cha karibu miaka 28 sasa tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992 na chadema ikaanza kushiriki kwenye chaguzi za kitaifa kama hizi za Udiwani, Ubunge na Urais, hakuna kipindi ambacho CCM na watu wake wanaojiita Tume ya Uchaguzi waliwahi kutupatia ushindi wa mezani pasipo wananchi kupitia nguvu yao ya umma kukataa na kupinga hujuma za CCM na serikali yao.
Pale walipojaribu kuiba kura na kutaka kupindisha matokeo ya washindi wa chadema, wahusika wa hujuma hizo wamekuwa wakionyeshwa cha mtema kuni na washindi wetu wamekuwa wakitangazwa na kupelekea grafu yetu ya kuishinda CCM na serikali yake imekuwa ikipanda kutoka mwaka mmoja wa uchaguzi hadi mwaka mwingine wa uchaguzi; na pamoja na kuwepo kwa mazingira mazito ya uchaguzi kwa miaka yote hiyo chini ya Tume hii hii inayoibeba CCM kwa mbeleko kila mwaka, hakuna mwaka wa uchaguzi ambao chadema tulipunguza idadi ya madiwani, wabunge na hata kura za urais.
Ndugu zangu wajumbe wa Mkutano Mkuu, ifuatayo hapa chini ni Historia ya ushindi wa chadema kwenye chaguzi mbalimbali tangu ulipoanza uchaguzi wa kwanza kabisa wa kuwapata madiwani mwaka 1994 na baadae mwaka 1995 ulipoanza kufanyika uchaguzi wa wabunge na rais;
Mwaka 1994 chadema iliposhiriki uchaguzi kwa mara ya kwanza ilipata madiwani 42. Katika mwaka huo wa 1994 haukufanyika uchaguzi wa wabunge na rais na badala yake, uchaguzi ule wa mwaka 1995 ulikuwa wa kuwapata wabunge na rais.
Mwaka 1995 ulipofanyika Uchaguzi wa Wabunge na Rais, Chadema ilipata Wabunge 4 na kwenye nafasi ya Urais, chama chetu (Chadema) hakikusimamisha Mgombea na badala yake kiliwaunga mkono Chama cha NCCR-Mageuzi kupitia Mgombea wao wa Urais wa wakati ule Agostino Lyatonga Mrema.
Mwaka 2000 ulipofanyika uchaguzi Mkuu wa madiwani, wabunge na urais, chadema ilipata madiwani 72, wabunge 5 na mwaka huo vile vile hatukusimamisha mgombea wa urais na badala yake tuliwaunga Mkono chama cha wananchi CUF kupitia kwa mgombea wao wa wakati ule Prof.Ibrahim Lipumba.
Mwaka 2005 wakati wa uchaguzi wa madiwani, wabunge na Rais, chadema ilipata madiwani 103, wabunge 11 na mwaka huu kwa mara ya kwanza tulisimamisha mgombea wa urais ambaye alikuwa; Mhe.Freeman Aikael Mbowe na kama chama, mwaka huu tulipata Kura 668,756 za Urais ambazo zilikuwa ni sawa na 5.8% ya kura zote zilizopigwa.
Mwaka 2010 wakati mgombea wetu wa Urais akiwa Dk.Wilbroad Peter Slaa; pamoja na mazingira magumu ya uchaguzi yaliyokuwepo wakati ule kwa wale mnaokumbuka, lakini Chadema ilipata madiwani 467, wabunge 49 na tulipata kura 2,271,941 za urais ambazo ni mara tatu zaidi ya kura za Uchaguzi wa mwaka 2005 wakati Freeman Mbowe alipokuwa mgombea sawa na Asilimia 26% ya kura zote.
Uchaguzi Mkuu uliofuata wa Mwaka 2015 wakati mgombea wetu wa Urais akiwa Edward Lowassa, Chama chetu (Chadema) kilipata Madiwani 1,084, Wabunge 71 na tulipata kura 6,072,848 za Urais ambazo ni mara tatu zaidi ya kura za uchaguzi wa mwaka 2010 wakati Dk.Slaa alipokuwa mgombea ambazo ni sawa na Asilimia 39.9% ya kura zote zilizopigwa.
Ndugu wajumbe wa Mkutano Mkuu na wageni wetu waalikwa, kauli za viongozi wa CCM na makada wao waliopo serikalini hasa (watendaji) zina lengo la kututia hofu na kutukatisha tamaa. Lakini kubwa zaidi wanalenga kutuondolea ari na dhamira kubwa tuliyonayo ndani ya mioyo yetu ya kutaka kuiondoa CCM madarakani ili waendelee kulikandamiza na kulinyonya taifa letu.
Aidha ikumbukwe kwamba; Historia hiyo ya kuanzia mwaka 1994 hadi mwaka 2015 ilijengwa katika kipindi ambacho Chama chetu (Chadema) kilikuwa hakijaimaarishwa vizuri kwenye misingi, matawi, kata, majimbo, wilaya, mikoa, kanda na taifa.
Je, baada ya zoezi la Chadema ni Msingi lililofanyika kwa nchi nzima na kukiimarisha chama katika ngazi zote za nchi hii; mnadhani mwaka huu chama kitapata madiwani, wabunge na kura ngapi za urais?
SALAAM ZA PONGEZI NA SHUKRANI
Ndugu zangu wajumbe wa Mkutano Mkuu na wageni wetu wa heshima, kwa niaba ya chama, napenda kutumia fursa hii kuwapongeza, viongozi wa chama na wanachama wote ambao; pamoja na changamoto nzito za hapa na pale walizopitia na wanazoendelea kuzipitia katika mapambano ya kuitafuta haki, lakini bado walisimama na wameendelea kusimama imara katika kuitetea, kuipigania na kuilinda chadema kama mboni ya jicho.
Kipekee sana, niwapongeze waheshimiwa madiwani wastaafu wenzangu wote walioamua kuvumilia kipindi chao chote cha uwakilishi wa miaka mitano katika maeneo yao na hadi leo hii wapo hapa ndani wakiendelea kukipigania chama chetu. Natambua tuliianza safari hii tukiwa jumla ya madiwani 25 kwa maana ya madiwani 18 wa kata, madiwani 7 wa viti maalum na Mbunge wa Jimbo, lakini mpaka kufikia siku ya leo; wakati tunajiandaa kuingia kwenye uchaguzi mwingine baada ya miaka mitano, tumebakia madiwani 13 pekee kati ya 25 kwa maana ya madiwani 7 wa kata na madiwani 6 wa viti maalum.
Aidha, kwa niaba ya chama; natambua mchango mkubwa wa Mbunge mstaafu wa viti maalum Mhe.Catherine Nyakao Ruge ikiwa ni pamoja na heshima aliyoilinda kwa ajili ya chama hiki pasipo kuuza utu wake kwa vipande vya sarafu. Kwa kuutambua mchango wao mkubwa ndani ya chama; tumewaandalia vyeti vya heshima na shukrani kwa uaminifu wao kwa chama chetu kwa kipindi chote cha utumishi wao kwa wananchi wa wilaya yetu ya serengeti na wote watakabidhiwa vyeti vyao hapa ndani kama ishara ya kuutambua na kuuheshimu mchango wao.
Ndugu zangu wajumbe wa Mkutano Mkuu na wageni wetu wa heshima, chama kimeutambua mchango mkubwa wa Mzee David Maganya Masama; Diwani Mstaafu wa Kata ya Nyamatare (2010-2015) ambaye pia alikuwa Mhazini wa chama ngazi ya wilaya kabla ya kustaafu kwa hiari yake mwenyewe mwaka jana 2019.
Chama kitamtunuku Mzee David Maganya cheti cha heshima na shukrani kwa uaminifu wake ndani ya chama ikilinganishwa na mazingira ya kisiasa aliyokuwa akiyapitia hasa alipokuwa Diwani pekee wa Chadema kwenye Mkoa wetu mzima wa Mara.
Chama kinatoa salaam za pongezi kwa familia ya Mzee David Maganya Masama kwa uvumilivu wao katika kipindi chote ambacho Mzee Maganya amekuwa akikitumikia chama hata katika mazingira magumu.
Ndugu zangu wajumbe wa Mkutano Mkuu, chama kimeutambua mchango mkubwa sana wa Marehemu Mzee Elias Majura Ngereza aliyekuwa Katibu wa kwanza kabisa wa chama chetu hapa wilayani Serengeti. Marehemu Mzee Ngereza alikitumikia chama hiki kwa uaminifu na uadilifu mkubwa sana; na katika mazingira magumu sana ya kisiasa huku akisaidiuana na wazee wetu wa heshima ambao mpaka leo hii wapo ndani ya chama wakiendelea na mapambano ya kukipigania chama.
Kwa niaba ya Wazee wengine wote wa heshima ndani ya chama, Mzee Mturi Tibango Mwenyekiti Mstaafu wa chama ngazi ya wilaya; naye atatunukiwa cheti cha heshima na shukrani kwa utumishi wake uliotukuka ndani ya chama. Wazee hawa wameendelea kuwa mfano wa kuigwa ndani ya chama kwa uvumilivu wao ndani ya chama na hata jinsi wanavyotoa ushirikiano wa karibu katika kushauri mambo mbalimbali ya kichama ukiachilia mbali kwamba ni wastaafu.
Vile vile, chama kimeutambua mchango mkubwa wa Mwenyekiti Mstaafu wa Chama Ngazi ya Wilaya Ndg.Sang’uda Mossy Manawa ambaye kwa sasa ni afisa wa chama anayehudumu katika kurugenzi ya ulinzi na usalama wa chama makao makuu ya chama jijini Dar es salaam. Chama kimeutambua mchango mkubwa wa Ndg.Sang’uda Manawa kutokana na kazi kubwa na nzuri aliyoifanya ya kuongoza na kuendeleza ujenga wa chama ndani ya wilaya yetu kwa kushirikiana na viongozi wenzake wa ngazi mbalimbali za chama waliokuwepo wakati ule.
Ndugu zangu wajumbe wa Mkutano Mkuu, vile vile, chama kimeutambua mchango mkubwa wa katibu wa chama ngazi ya wilaya aliyekuwepo kipindi cha Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka 2014 na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 Ndg.Julius Anthony Wambura.
Chama kimeutambua mchango wake kutokana na jitihada kubwa alizozifanya kwa kushirikiana na Viongozi wenzake wa Chama wa Ngzi zote kuhakikisha kwamba, Chama kinapata ushindi kwenye Uchaguzi ule wa Serikali za Mitaa wa 2014; na hata Uchaguzi Mkuu uliofuata baadae mwaka 2015 ambao ulipelekea chama chetu kuichukua Halmashauri ya Wilaya yetu na kufanikiwa kushinda kiti cha Ubunge wa Jimbo letu.
Kutokana na heshima hii, wafuatao hapa chini, nao wanastahili kupata vyeti vya heshima na shukrani kwa kuilinda heshima ya Chama na Wananchi katika kipindi chote cha utumishi wao tangu walipoaminiwa; ama na Chama, ama na Wananchi wa maeneo yao wanakotokea;
1:Mhe.Catherine Nyakao Ruge – Mbunge Mstaafu wa Viti Maalum Mkoa wa Mara ambaye pia ni Mhazini wa Bawacha Ngazi ya Taifa.
2: Mhe.Francis Muhingira Garatwa - Diwani Mstaafu wa Kata ya Nyansurura ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama Ngazi ya Wilaya na Mwenyekiti Mstaafu wa Kijiji cha Nyansurura.
3:Mhe.Joseph Mwita Kihungwe- Diwani Mstaafu wa Kata ya Mugumu ambaye pia ni Mwenezi wa Chama chetu Ngazi ya Wilaya.
4:Mhe.Marwa Chacha Michael - Diwani Mstaafu wa Kata ya Machochwe na Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Chama Ngazi ya Taifa.
5:Mhe.Modesta Juma Masese - Diwani Mstaafu wa Viti Maalum na Katibu wa Baraza la Wazee Ngazi ya Wilaya.
6: Mhe.Charles Tunda - Diwani Mstaafu wa Kata ya Stendi Kuu ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati tendaji ya Chama Ngazi ya Wilaya na Mwenyekiti Mstaafu wa Madiwani.
7: Mhe.Ester Nyamhanga Gairigi - Diwani Mstaafu wa Viti Maalum na Mjumbe wa Kamati tendaji ya Chama Ngazi ya Wilaya.
8: Mhe.Mtoni Manyaki Mlale - Diwani Mstaafu wa Kata ya Kyambahi ambaye pia ni Katibu Mwenezi wa Chama chetu Kata ya Kyambahi.
9: Mhe.Nyangi Mwikwabe Matiko - Diwani Mstaafu wa Kata ya Matare ambaye pia ni Katibu wa Baraza la Wazee Kata ya Matare.
10: Mhe.Marwa Chacha Girimwa - Diwani Mstaafu wa Kata ya Nyamoko ambaye pia ni Mwenyekiti Mstaafu wa Kijiji cha Itununu.
11: Mhe.Samwel Kitome - Diwani Mstaafu wa Kata ya Kisaka ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti Mstaafu wa Halmashauri yetu ya Wilaya ya Serengeti.
12: Mhe.Bertha Evaris Tumbago - Diwani Mstaafu wa Viti Maalum ambaye pia ni Mhazini Mstaafu wa Madiwani.
13: Mhe.Edina Elias Ngereza - Diwani Mstaafu wa Viti Maalum ambaye pia ni Mwenyekiti Mstaafu wa Bawacha Wilaya ya Serengeti.
14: Mhe.Rose Joakim Ngowi - Diwani Mstaafu wa Viti Maalum ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bawacha Kata ya Natta.
15:Mhe.Happynes Chacha Nyigana– Diwani Mstaafu wa Viti Maalum ambaye pia ni Mjumbe Mstaafu wa Kamati tendaji ya Chama Ngazi ya Wilaya.
Ndugu zangu Wajumbe wa Mkutano Mkuu, kupitia Mkutano huu Mkuu wa chama, nitumie fursa hii kuwashukuru na kuwapongeza wadau, viongozi na wanachama mbalimbali wa chama chetu waliojitolea kwa namna moja ama nyingine katika kuhakikisha kwamba, tunapata chochote kutoka kwao ili kuufanikisha huu Mkutano wetu Mkuu wa leo.
Vile vile, nawashukuru na kuwapongeza wale wote waliokuwa karibu nasi katika kipindi chote cha maandalizi ya Mkutano huu na shughuli nyingine zote za ujenzi wa chama zilizokuwa zikiendelea ndani ya chama ili kujiandaa na uchaguzi huu mkuu ikiwemo mafunzo ya kuwajengea uwezo viongozi wetu wa kata zote 30 yanayoendelea hivi sasa kwenye kata zetubaada ya kumaliza hatua ya pamoja kama wilaya hapa mugumu mjini.
Kipekee sana kwa niaba ya wengine wote; niwashukuru, Bw.Godfrey Mokiri Masaga Mkazi na Mfanyabiashara wa Kata ya Magange kwa mchango wake wa hali na mali kwa chama chetu, nimshukuru na kumpongeza Mbunge Mstaafu wa viti maalum na Mhazini wa Bawacha Taifa Mhe.Catherine Nyakao Ruge kwa mchango wake mkubwa na wa moyo wa kipekee sana ambao karibu kwa zaidi ya asilimia 90% ya gharama za kuufanikisha Mkutano huu amezisimamia yeye mwenyewe kwa kuchangia kwenye chama fedha taslimu kupitia akaunti ya chama.
Vile vile niutambue mchango wa mjumbe wa kamati tendaji ya kanda Ndg.Thomas Nyahende alioutoa kwa chama kwa ajili ku-support mafunzo elekezi ya uchaguzi. Kwa niaba ya chama, nimshukuru pia Ndg.Maguye Simon Maguye kwa kile kidogo alichoweza kutoa ili kuongezea nguvu ya kuufanikisha huu mkutano wetu wa leo; Mungu awabariki sana wote!
Ndugu zangu wajumbe wa Mkutano Mkuu, leo ni siku muhimu sana kwa mustakabari mzima wa Chama chetu kwa miaka mingine mitano ijayo. Tunakwenda kufanya Uchaguzi wa Kura ya maoni ndani ya Chama kwa kumchagua Mgombea wa nafasi ya Ubunge wa Jimbo letu.
Kura hii ya maoni sio hitimisho la nani atakuwa mgombea wa ubunge kwenye jimbo letu na badala yake, kwa mujibu wa katiba ya chama chetu, haya yatakuwa mapendekezo, lakini baada ya hatua hii, Vikao mbalimbali vya chama vitaketi na kufanya Uteuzi wa mwisho wa nani atakuwa Mgombea wa nafasi hii kwenye jimbo letu.
Niwashukuru waheshimiwa madiwani wastaafu wote kwa mchango wa kusaidia kufanikisha mafunzo elekezi ya uchaguzi, sambamba na wajumbe wenzangu wa kamati ya utendaji ya chama ngazi ya wilaya kwa mchango wake wa hali na mali walioutoa ili kuhakikisha kwamba, chama kinafanikiwa kutoa mafunzo kwa wapiganaji wake.
UMOJA, MSHIKAMANO, UPENDO NA USHIRIKIANO
Ndugu zangu wajumbe wa Mkutano Mkuu, kama kiongozi wa chama, natoa wito kwa kila mmoja wetu kuhakikisha kwamba; tunaendelea kudumisha umoja, mshikamano, upendo na ushirikiano mwema miongoni mwetu hata mara baada ya hatua hii ya kura ya maoni. Sio kwa Wajumbe pekee, lakini pia; natamani kuona umoja, upendo na mshikamano huo ukitamalaki hata miongoni mwa wagombea wetu watakaosimama hapa mbele yetu leo kuomba ridhaa ya kuwa wagombea wa nafasi hii ya uwakilishi wa wananchi bungeni.
Chagueni Mgombea sahihi atakayeweza kukivusha Chama hasa katika kipindi hiki kigumu cha uchaguzi wa kukabiliana na CCM kwa nguvu ili kudhibiti hujuma za kipindi cha uchaguzi kutokana na ukweli kwamba, totally CCM imeshapoteza ushawishi mbele ya Wananchi mpaka kiwango cha mwisho.
Chagueni Mgombea atakayekuwa tayari kuwajibika na kujituma katika suala zima la Kampeni za Uchaguzi. Lakini aliye tayari kutambua uzito wa jukumu lililoko mbele yetu na mbele yake hasa wakati wote wa Kampeni za Uchaguzi.
Ndugu zangu wajumbe wa Mkutano Mkuu, wakati tunapokwenda kufanya chaguzi zetu za Ngazi zote kwa maana ya Udiwani wa viti maalum, Udiwani wa Kata na Ubunge wa Jimbo letu ambalo sehemu ya eneo lake kubwa ni vijijini, tukumbuke hali ya Uchaguzi wa sasa ilivyo, na tukumbuke kwamba; michakato ya Uchaguzi inaanzia kwenye hatua za kukabiliana na watendaji wa serikali huko Maofisini wakati wa kuchukua, kujaza na kurejesha fomu za Wagombea wetu.
CCM kwa kushirikiana na watendaji wa Umma, kwa maksudi kabisa wakati wa chaguzi, huwa hawataki kufuata Sheria, Kanuni, taratibu na miongozo ya Uchaguzi bila kulazimishwa; hivyo, kupitia chaguzi zetu za nafasi za Udiwani na Ubunge, nasisitiza tupate Wagombea walio tayari kwa kurupushani za kila aina na walio tayari kwa lolote wakati wa kudhibiti hujuma za CCM na watu wao.
HITIMISHO
Ndugu zangu Wajumbe wa Mkutano Mkuu na wageni wetu waalikwa, katika uchaguzi huu wa leo, natambua kila mmoja wetu kwa nafsi yake anaye Mgombea anayemuona kwamba anafaa kuipeperusha bendera ya chama chetu, huo ni utaratibu wa kawaida kabisa wa kiubinadamu ambao katika mazingira ya aina yoyote ile hauwezi kukwepeka.
Hivyo basi, pamoja na uwepo wa hali hiyo; naamini baada ya hatua hii ya kura ya maoni kupitia huu uchaguzi wetu, sote tutalazimika kuunganisha nguvu ya pamoja ili kuanza mapambano ya kuikabiri CCM na wake wake ili kuulinda ushindi wetu na kudhibiti hujuma.
Napenda ieleweke hivi, sisi Chadema huwa hatukosani, ila tunatofautiana mitazamo kutoka jambo moja kwenda jambo linguine na automatically hiyo ndio Demokrasia yenyewe inayotajwa kwenye jina la chama chetu yaani Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na kutofautiana mtazamo katika jambo hili ama lile sio dhambi maana kwa hulka za kawaida za kiubinadamu, ni vigumu sana watu wote kuwa na mawazo ama mitazamo inayofanana.
Kubwa zaidi ninalosisitiza kama Kiongozi wa chama, kutofautiana kwetu kwenye masuala ya msingi yahusuyo Chama, hakupaswi kuchukuliwa kama uhasama, ugomvi ama vita na hata ukapelekea kuhatarisha na kuuyumbisha umoja, upendo na mshikamano uliopo miongoni mwetu na badala yake, nasisitiza; kutofautiana huko kuchukuliwe kama njia za kutuimaarisha na kutuleta pamoja kama ndugu wa tumbo moja ambaye mzazi wetu ni Chadema.
Aidha, ushindi wa Mgombea yeyote yule kati ya hawa wote watakaosimama hapa mbele yetu kuomba ridhaa, utakuwa ni ushindi wa Chadema kama taasisi. Hivyo basi, baada ya uchaguzi huu, natamani kuona watu wote tukifurahia pamoja na kupongezana kwa ajili ya chama chetu kuikamilisha hatua hii muhimu ya mapendekezo ya kumpata mgombea wa ubunge kwenye jimbo letu.
Nawatakieni Uchaguzi mwema!
Mungu Awabariki sana!
Mungu Aibariki Tanzania!
Mungu Aibariki Chadema!
Ahsanteni kwa kunisikiliza!
Francis M. Garatwa,
Mwenyekiti CHADEMA (W) Serengeti.
13 Julai, 2020.