SI RAIS SAMIA SULUHU HASSAN ALIYEKO MADARAKANI KWA SASA WALA RAIS AJAYE, ATAKAYEMFUNIKA HAYATI RAIS MAGUFULI KIUTENDAJI, IWE KWA SIKU 100 AU MIAKA 100 IJAYO:
Naomba nianze kwa kusema kwamba, Kujaribu kulinganisha utendaji kazi wa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutimiza siku 100 madarakani, dhidi ya siku 100 alizotimiza hayati Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ni sawa na kufananisha kati ya ukubwa wa Mlima Kilimanjaro na Kichuguu, ambapo ni vitu viwili tofauti.
----------------------------------
Hivi sasa kuna mjadala unaoendelea nchini, ni kuhusu utendaji kazi wa Rais Samia Suluhu Hassan kutimiza siku 100 madarakani pamoja na mafanikio yake. Kwenye mjadala huu kupitia vijiweni, vyombo vya habari ikiwemo mitandao ya kijamii, kuna sifa kedekede zinazotolewa na makundi mbali mbali ya watu wakiwemo, wanaharakati, waandishi wa habari, wasomi, wanasiasa, pamoja na wananchi wa kawaida.
Wapo wanaosema mama ameanza vizuri, wapo wanaodai mama amekuja kuiponya nchi, wapo wanaodiriki kusema mama amerudisha utawala wa sheria, wapo wanaosema hakuna chombo cha habari kilichofungiwa, na pia wapo wanaosema hakuna aliyekamatwa au kufikishwa mahakamani kwa kosa la kuikosoa serikali kama ilivyokuwa huko nyuma, na wengine wanadai, hivi sasa nchi inapumua baada ya watu kubanwa kwa kipindi cha miaka mitano bila kufurukuta.
Ukifuatilia mjadala huu unagundua ni kama vile kuna mambo mawili. Moja watu wajaribu kuonyesha kana kwamba, kuna ushindani wa ubora kati ya utendaji kazi wa Rais Samia Suluhu Hassan aliyeko madarakani dhidi ya utendaji kazi wa hayati Rais Dkt. John Pombe Jiseph Magufuli, na jambo la pili ni kujaribu kuonyesha kwamba, Rais aliyeko madarakani ni mwema zaidi kuliko mtangulizi wake.
Baada ya kuufuatilia na kutafakari kuhusu mjadala huu, nimebaini kuhusu kuwepo kwa mapungufu matatu muhimu yanayowasumbua watanzania.
Jambo la kwanza, watanzania hatuna ufahamu wa kufuatilia maswala muhimu yanayolihusu taifa letu na badala yake tunajikita kusifia pamoja na kupongeza mambo madogo madogo yasiyokuwa na tija wala umuhimu katika maisha yetu. Kwenye eneo hili watu hawajishughulishi japo kuhoji kuhusu mkataba wa ujenzi wa bandari ya Bagamoyo ambao tuliambiwa, kutokana na masharti ya hovyo yaliyokuwemo kwenye mkataba huo, ni kichaa tu ambaye angeweza kuyakubali. Kwa watanzania, hilo si muhimu, kilicho muhimu kwao ni kupumua.
Aidha, vile vile watanzania hawajishughulishi kuhoji kuhusu waliokwapua mamilioni hazina na kujilipa posho, ni lini watafikishwa mahakamani, bali kilicho muhimu kwao ni kupewa uhuru wa kutukana mitandaoni pasipo kukamatwa. Watanzania hawajishughulishi kuhoji kuhusu wahujumu wa uchumi, na wezi wa mafuta waliotoboa bomba la mafuta ya serikali kule Kigamboni na watuhumiwa 14 kukamatwa watafikishwa lini mahakamani, isipokuwa kilicho muhimu kwao ni kuambiwa wadumishe amani huku nchi inateketea.
Kwenye eneo hili wanachosahau watanzania ni kwamba, kama kuna kiongozi aliyeingia madarakani, akashughulika na kero lukuki zilizokuwa zikiwakabili wananchi bila kupatiwa ufumbuzi, ikiwemo huduma mbovu za afya hususani kwa mama wajawazito kujifungulia chini, basi kiongozi huyo si mwingine isipokuwa ni hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.
Pia watanzania wanasahau kwamba, kama kuna kiongozi aliyeingia madarakani akakuta nchi imeoza, inanuka rushwa, ufisadi, matumizi mabaya ya madaraka pamoja na uporaji wa rasilimali ikiwemo madini, ujangiri wa tembo na mikataba ya ovyo, basi kiongozi huyo si mwingine bali ni hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.
Vile vile watanzania tunasahau kwamba, kama kuna kiongozi aliyeingia madarakani na kukuta ujambazi wa kutumia silaha umeshamiri kufikia hatua ya mabasi kutosafiri usiku baada ya saa 4.00 ukiachilia mbali ajali zilizoua watu makumi kwa mamia kika uchao na kukomesha hali hiyo, basi kiongozi huyo si mwingine bali ni Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.
Sanjari na hiyo, watanzania wamesahau jinsi Chama cha Mapinduzi kilivyonuka rushwa na ufisadi kila kona kiasi cha wanachama wake pamoja na mashabiki kuzomewa popote walipoonekana wsmevaa sare za Chama. Ni hayati Rais Msgufuli aliyeking'arisha na kukirudishia uhai wa kupendwa.
Ndani ya siku 100 za Magufuli, wagonjwa wote Muhimbili walilala kwenye vitanda badala ya kulala chini sakafuni au mzungu wa nne. Ndani ya siku 100 za Magufuli, madawati yalitengenezwa karibu nchi nzima. Ndani ya siku 100 za Magufuli watumishi hewa zaidi ya 19,000 walibainika kisha kuondolewa kwenye mfumo.
Ninachotaka kusema ni kwamba, kujaribu kulinganisha utendaji kazi wa siku 100 za Rais Samia Suluhu Hassan madarakani, na siku 100 za hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, ni sawa na kulinganisha Mlima na kichuguu.
Kwangu mimi ukiniuliza ni jambo gani Rais Samia Suluhu Hassan amefanya kwa siku 100 alizokaa madarakani ninaloweza kumpongeza, ni kushusha gharama za wateja kuunganishiwa umeme kutoka zaidi ya Tshs. 300,000/=, kuwa Tshs. 27,000/=, iwe kijijini au mjini.
Mengine yoote anayofanya ni kuwapa ahuweni wezi, wakwepa kodi, mafisadi, kuwaachia walioua Padiri, kumwagia watu tindikali pamoja na kuwaumiza wafuasi wa Chama chake waliokipigania Chama kwa gharama ya jasho la damu kupata ushindi katika mazingira magumu. Ndiyo maana majambazi wameibuka kwa kasi, mapato yameshuka, watu wanadiriki sasa kutoboa hadi bomba la mafuta, ajali zimerudi kuuwa abiria kama wote. Sijaona nimsifu Rais kwa lipi, kwa siku 100 alizokaa madarakani.
Yaani wakati Mbowe na Chadema yake wakiwapambania wafuasi wake wanaokitetea Chama katika mazingira ya kihalifu, ikiwemo kuitukana serikali, yeye mama anawafurahisha Chadema hao hao kwa kuwakomoa wafuasi waliokipigania Ccm katika mazingira magumu. Wakati utafika, pumba na mchele.