Mabibi na mabwana nimebahatika kuwa miongoni mwa waliojihimu vilivyo kwenda kumuaga mzee wetu.
Asiyejua kufa na akaangalie kaburi.
Mzee katutoka na kweli ni huzuni kubwa.
Sisi kama waswahili uvumilivu, na hasa kuvumiliana misibani ndiyo tunu zetu hizo. Wenyewe tunaita "subira."
Mbele ya marehemu kwa waswahili wastarabu, wote ni ndugu. Huwa hayupo mwenye msiba, bali msiba huwa wa wote.
Wahurumiwe wote ambao kwa kujua au kutokujua kwao wanajikuta kwa namna yoyote ile wakifarakanisha waombolezaji. Wakidhani labda wana haki zaidi msibani kuliko wengine.
Anasema Messiah: "uwasamehe kwani hawalijui walitendalo."
Ni kweli kuwa uwanja ulikuwa umefurika vilivyo. Katikati ya janga hili la gonjwa huu tulilomo, kwa hakika isingewezekana kabisa kwa watu wote kuendelea kujazana mle bila kikomo.
Tumshukuru mola kwa yote. Aliyeweza kuingia ndani na aliyeshindwa kuingia sote lililokuwa limetupeleka kule lilikuwa moja. Sisi sote tu wamoja.
Makamanda, kwa hakika mmeionyesha sehemu yenu ya nia njema kwa kuungana na watanzania wote kwa kufika kwa wingi wenu, kumuaga mzee wetu.
Hata kwa mlioshindwa kuingia ndani kwa sababu yoyote ile, bado mmefanya sehemu yenu ya kufika kwa nia moja.
Mzee wetu tumemuaga. Yote heri. Mzee wetu akapumzike kwa amani.
Kwa hakika kwa mara nyingine mmedhihirisha Tanzania ni moja.
Washindwe maadui zetu popote kule walipo ambao kwa sababu zao zozote walizo nazo, wangependa kuona tunagawanyika.
Watakaoweza, tuwakilishane Lupaso.
Pumzika kwa amani Rais mstaafu Benjamin Mkapa.
Mungu ibariki Tanzania.