Hii ni hatua nzuri na kubwa sana kwa watanganyika, inaonesha vile tukiamua kupigania jambo kwa umoja wetu, hayupo yeyote wa kutushinda.
Sasa kwa hatua hii, ndio inathibitisha bila shaka, ule mkataba kati ya serikali na DPW ni haramu, haufai kuachwa uendelee kuwepo kwasababu umevunja sheria zetu za ndani tulizojiwekea ili kulinda rasilimali zetu wenyewe.
Natumai hatua ya mwisho itakuwa ni kuuvunjilia mbali ule mkataba haramu hii ni kazi ya serikali ya Samia, hata kama akiendelea kuziba masikio lazima auone na kuufanyia kazi ukweli, lazima serikali yake iheshimu sheria zetu za ndani.
Mwisho kabisa, kwa bunge kukataa kupitisha ile sheria, imeonesha mhimili wa bunge umeidharau mahakama kuu, ambayo ilitoa mapendekezo kwenye hukumu yake ikilitaka bunge likafanye marekebisho ya sheria ili kuendana na ubovu wa ule mkataba wa bandari.
Mahakama kuu kanda ya Mbeya imejidhalilisha yenyewe, badala ya kutoa order ikiri ule mkataba wa bandari ni wa hovyo, ikalipa bunge maelezo nini lifanye, na bunge nalo sasa limegoma, naamini hapa mhimili wa mahakama umejifunza jambo, wasifanye kazi kwa mazoea ya kumfurahisha mtawala.
Pongezi ziende kwa wote waliopinga na wanaoendelea kuupinga ule mkataba wa hovyo wa bandari, likiwemo Kanisa Katoliki kupitia waraka wake, ambao sasa nguvu zake zinathibitika kuanzia serikalini mpaka bungeni, wanasheria, na wengine wote wenye kuitakia mema Tanganyika yetu.