Mkuu 'Proved':, nashukuru kwa kunialika hapa kwenye mada hii, ambayo mwanzilishi wake..., aaahaaa; acha nisiende huko.
Kaandika vizuri, sasa sijui kama kweli anatafuta ufumbuzi wa haya maswala mazito yanayotukabili sasa hivi kama taifa, au ni gheresha tu, kama aliyofanya kwenye ile mada nyingine inayofanana na hii.
Maoni yangu (mchango) wangu kwenye maswala ya namna hii ni rahisi kabisa na wala sina kusita juu yake.
DP World, au mwingine yeyote anayetafuta biashara ya kuja kufanya hapa kwetu, akipata faida halali ya kazi yake , nasi tukipata manufaa ya uwekezaji wake bila kuhatarisha mali zetu... anakaribishwa sana.
Sijui kama kuna mTanzania anayekataa jambo kama hilo.
Mzozo uliopo na unaokwepwa kama ukoma na hawa wenzetu wanaokomalia huyu DP World, ni kama kwamba ni huyo huyo pekee ndiye anayeweza kufanya kazi hiyo kwa ufanisi, na hakuna mwingine yeyote anayeweza kama yeye. Kuweka ushahidi juu ya hili, ni kuwa huyu DP World hakushindanishwanna mwingine yeyote katika kuwania kazi hiyo.
Mbaya zaidi, ni hapo waTanzania wanaposoma yanayoitwa "Makubaliano" yaliyofikiwa baina ya Tanzania na hiyo nchi nyingine, anakotoka huyo DP World.
"Makubaliano" ambayo wengi wanayatafsiri kama "Mkataba" yanayo 'demand' kwa Tanzania kufanya mambo ambayo haijawahi kuyafanya tokea nchi yetu iwe huru. Haya ndiyo yanayowastua watu wengi na kuhoji, na sasa kupiga kelele kabisa kwa hofu kuwa raslimali zetu zinauzwa kwa wageni bila ya uwepo wa ukomo, na kupitia katika hali hiyo, nasi raia tunaingizwa kwenye mpango wa kuwatumikia hawa wageni kama watumwa wao.
Acha nisiandike mengi, kwa sababu hapa ninatiririka tu bila kupumua.
Nimalize kwa hili ninalolichukulia kuwa la muhimu zaidi kuliko yote niliyoandika huko juu; nalo ni hili:
Nchi yetu tumepata uhuru tokea 1961, tuna umri zaidi ya miaka 60 sasa. Sisi kama binaadam ni watu wenye umri mkubwa sasa.
Ninasikitika sana kwa viongozi wetu kutoona maana ya umri wetu huu. Tutakuwa wategemezi wa kufanyiwa mambo yetu, hata madogomadogo kama haya ya kuendesha bandari hadi lini?
Ni lini sisi tutaanza kufikiria angalao kujijengea uwezo, hata kama ni taratibu ili lengo likiwa kufanya mambo yalliyomo katika uwezo wetu?
TICTS tumekaa naye hapo bandarini takribani zaidi ya miaka 20 hivi. Hatukujifunza chochote kutoka kwake katika muda wote huo? Hii kazi ya bandari inaugumu kiasi gani hicho?
Hapana. Ninafahamu wapo waTanzania wenye uwezo kabisa wa kufanya kazi pale bandarini, ni wao wanaofanya kazi zote hadi sasa.
Juzijuzi tumesikia sifa bandari yetu ikionyesha ufanisi katika kazi zao. Serikali ilizisikia hizi habari? Serikali ilifanya juhudi gani kuwatia moyo hawa wazalendo ili ufanisi zaidi uendelee kuwepo hapo bandarini?
Tunachosikia sasa ni "mifumohaisomani", ndiyo maana lazima tumlete DP World asomeshe mifumo..., kwa masharti gani? Kuuza raslimali za waTanzania na kuwapeleka utumwani?
Watu wanasema hatuna pesa za kuwekeza pale, sawa; lakini mbona tumekopa WB ili kupapendezesha kabla hatujagawa chee kwa DP World?
Viongozi na watu vipofu wa akili wanasema waTanzania hawawezi kufanya chochote cha maana, ndiyo maana ni lazima tulete DP World afanye kazi.
Na mimi ninasema hivi, kwa mantiki hiyo hiyo, tunahitaji kuwaondoa akina Samia na serikali yake yote, tulete wenye uwezo wa kuendesha serikali kwa ufanisi zaidi.
Ukiona makosa humo ndani, fahamu kwamba nilikuwa ni kama nakimbia marathon wakati nikiyaandika haya.
Mkuu 'Proved', yangu ndiyo hayo. nakushukuru tena kwa kunialika hapa.