Ni vema watu tukawa wakweli wa nafsi zetu. Tanzania ni nchi maskini kwa vigezo vinavyofahamika. Lakini ndani ya Tanzania, kuna mikoa ni maskini sana, na kuna mikoa yenye unafuu mkubwa.
Ndani ya Tanzania, kuna mikoa ambayo watu wake wengi wameelimika na kuna mikoa, mpaka leo, unaweza kufika kwenye kijiji kizima, hakuna mtu ambaye ana elimu angalao hata ya shahada moja.
Kuna mikoa ambayo watu wake wana elimu kubwa ya fursa za kiuchumi zinazopatikana kwenye maeneo yao, kuna mikoa hawajitambui na wala hawajui wayatumie namna gani mazingira kujipatia maendeleo.
Mambo mengi yamechangia hali hiyo. Lakini kwa sura ya haraka, mikoa ya wafugaji, kwa kiasi kikubwa ni duni katika vigezo vingi. Ukiwa duni katika elimu, duni katika kipato, duni kuhusiana na elimubya mazingira yako, huwezi kujitambua, huwezi kuwa na ujasiri, na utabakia kuwa mshangiliaji wa watawala hata kama watawala hao hawakufanyii chochote cha pekee na cha maana.
Mikoa kama Kilimanjaro, Arusha, Iringa, Njombe, Mbeya, Dar, ni nadra sana kuona wakimhusudu mtawala. Hawana haja ya kujikomba kwa watawala kwa sababu wanaamini kuwa wana uwezo wa kuyategemeza maisha yao bila ya kumtegemea mtawala. Wanajua kuwa mtawala ni binadamu kama wao, kuwa mtawala hakujamwongezea chochote katika ubinadamu wake. Wanatambua kuwa mtawala anaweza kufanya vizuri au kukosea.
Umaskini wa elimu unakufanya kuwa maskini wa kipato, umaskini wa kipato unakufanya kuwa dhaifu na kukuondolea kujiamini.