The Roman Catholic Church is among the most conservative institution. Yaani:
Kanisa Katoliki la Roma ni miongoni mwa taasisi zisizobadilika katika mafundisho na taratibu zake.
MASHOGA WASIJIPE TUMAINI KUWA KUNA SIKU KANISA LITABARIKI USHOGA KUWA NI JAMBO JEMA.
Kanisa Katoliki halijawahi kubariki ushoga na wala halijawahi kutoa kauli ya kubariki ushoga. Ushoga unahusisha mambo ya kuingiliana kinyume cha maumbile, na kwenye kuingiliana kimaumbile kunahusisha maneno haya magumu yasiyopendeza kuyatamka lakini tunalazimika kuyatamka, UFIRAJI na ULAWITI. Matendo haya ni dhambi, na hata siku moja Kanisa Katoliki kwa msingi wake, haliruhusu kubadilisha amri yoyote ya Mungu, manabii wa Mungu au mitume wa Kristo.
Baadhi ya watu, au kwa makusudi au kwa kukosa uelewa, wakaja na maneno ya uwongo kuwa Kanisa Katoliki kwa kupitia Kiongozi Mkuu wa Kanisa, Papa Francis eti limebariki ushoga.
Na hayo waliyatoa kutoka kwenye kauli aliyoitoa Papa kuhusiana na mashoga, baada ya kuulizwa na wanahabari kuhusiana na haki za mashoga. Papa Francis, jibu lake lilikuwa wazi kabisa na thabiti kwa wenye uelewa: Kwa kauli yake alisema, "HOMOSEXUALITY IS NOT A CRIME BUT IT IS A SIN. Kitu ambacho kila mwenye uelewa atakubaliana nacho.
NINI MAANA YA CRIME na SIN, na NINI UTOFAUTI WAKE:
Mtu anayefanya tendo ambalo ni crime, anakuwa criminal. Crime ni jinai. Kwa wale waliopotosha kauli ya Papa, hivi wanaamini kuwa ushoga ni jinai?
Papa alikemea tabia ya baadhi ya Serikali kufanya ushoga kuwa ni jinai, na baadhi ya Serikali kuweka sheria kali, ambapo shoga akithibitika, adhabu yake ni kifo.
Sin, ni dhambi. Dhambi ni tendo lolote lile ambalo hata kama wanadamu wote mkakubaliana ni jema, lakini maagizo ya Mungu ni tofauti, hilo lililokatazwa ukalitenda, itakuwa ni dhambi.
Kuna matendo ambayo ni dhambi (sin) na ni jinai (crime). Mathalani kuua ni dhambi, na ni jinai. Kuiba ni dhambi na ni jinai.
Kuna matendo ni dhambi lakini siyo jinai. Kwa mfano, uzinzi ni dhambi, lakini kwa mataifa mengine siyo jinai, ndiyo maana kuna baadhi ya mataifa hutoa mpaka leseni za kufanya biashara ya uzinzi. Kutowaheshimu wazazi wako ni dhambi lakini siyo jinai.
Sasa kwa msimamo wa Kanisa, na mafundisho ya Kristo, mtenda dhambi anafundishwa, na wakati mwingine anakemewa, lakini kwa upole na upendo, ili abadilike. Hatengwi. Na ndicho alichokisistiza Papa.
Yesu, katika utume wake, alikaa na kula na watu ambao wayahudi waliamini ni watenda dhambi, na wakamshutumu kuwa huyu si mwana wa Mungu, mbona anakula na kunywa na wenye dhambi? Naye akawaambia kuwa tabibu hayupo kwaajili ya walio wazima bali wagonjwa. Tena akaongeza kuwa, ni furaha ilioje mkosefu mmoja akiongoka. Na akatoa mfano juu ya mfugaji wa kondoo 100, ambaye kondoo wake mmoja akitoweka, huwaacha tisini na kenda, akamfuata yule mmoja aliyepotea. Na akimpata huyo mmoja aliyepotea hufanya sherehe. Akasema ndivyo alivyo Baba wa Mbinguni, maana yake Mungu huweza kuwaacha mamilioni walio wema na kumfuata mkosefu mmoja ili arudi kwenye kundi lake. Na mkosefu huyu akibadilika na kuongoka, huwa na furaha kubwa kwa ufalme wote mbinguni.
Mafundisho ya Kanisa Katoliki yanaegemea sana sehemu mbili, yaani maandiko matakatifu na mapokeo. Tena mapokeo yanachukua nafasi kubwa zaidi. Sababu ipo wazi, Yesu alipoondoka, hakuacha kitabu/biblia, bali aliwaacha mitume. Biblia tunayoisoma leo, imekuja kuwa kwenye muundo unaokaribia sana na wa sasa, karibia miaka 300 baada ya Kristo.
Kwa kuzingatia mapokei, ndiyo maana kuna maswali ambayo Kanisa Katoliki huwa halijitesi kutafuta sababu za kisayansi au kijamii. Kwa mfano, kwa nini wanawake hawawi makasisi? Hatujui, lakini tunachojua ni kwamba katika wale mitume wa Kristo, hakumchagua hata mwanamke mmoja kuwa mtume. Na hata wale mitume, baada ya Kristo kupaa mbinguni, hawakuwahi kumwekea mikono mwanamke yeyote kuwa mtume. Hilo ndiyo jibu. Wapo wanaharakati wa kutetea haki za wanawake, kwa nyakati tofauti wamepigania ili wanawake wawe na nafasi sawa katika utumishi wa Kanisa, lakini haiwezekani kwa sababu ya hizi sababu za kimapokeo. Lakini tunajua kila walikoenda mitume na hata Yesu, kuna akina mama waliandamana nao, wakiwaandalia chakula, na wengine wanasifika sana kwa unyofu na utakatifu wao. Kanisa likawaandalia nafasi yao ndani ya Kanisa, hao ndio wanaitwa watawa.
Kama kuna jambo lolote lile ambalo ni agizo la Kristo, Mungu Baba kwa kupitia manabii, au ni agizo la mitume wa Kristo, nina hakika, hata kufanyike jitihada gani ya kulibadili, na hata mataifa yote Duniani yaafiki, Kanisa Katoliki haliwezi kuridhia.
Kanisa Katoliki, ndiyo la kale zaidi na ndiyo lenye kumbukumbu nyingi za historia ya Ukristo, kuliko Kanisa jingine lolote, na ndilo lililokataa kuwa haliwezi kwenda na wakati katika mambo ya kiimani.
Ushoga ni dhambi, siyo kwa sababu ya wanaume wawili kuishi pamoja, au wanawake wawili kuishi pamoja, bali ni kutokana na tendo la kuingiliana kinyume cha maumbile, UFIRAJI na ULAWITI. Na kwa msingi wa kiimani, hata mwanaume anayemwingilia mkewe kinyume cha maumbile, ni mtenda dhambi, sawa na shoga maana kitendo wanachokifanya ni kile kile kilichokatazwa na Mungu. Kanisa linaweza kumbariki mtu anayefanya ushoga lakini siyo ushoga. Kwa mfano, shoga ambaye ameamua kuanza process ya kuacha ushoga, akaenda kwa Kasisi kuomba ambariki katika safari yake ya kutaka kubadilika, atabarikiwa. Atabarikiwa yeye, siyo ule ushoga wake. Ni sawa na mtu mwenye mitala, anataka aachane na baadhi ya wake zake, na kuna mchakato wa kuufuata ili kila jambo liende kwa mwongozo wa Mungu, anaweza kwenda kwa Kasisi kuomba baraka yake ili akamilishe dhamira yake njema inayoendana na ukristo. Huyo anayebarikiwa mpaka wakati huo atakuwa ni polygamist, lakini kilichobarikiwa siyo polygamist relationship yake.
Je, tubebe mawe kuwaua au tuwatie jela mashoga tunaowafahamu, na wanaume wote wanaowaingilia wake zao kinyume cha maumbile? Au vijana wanaowatafuta wasichana halafu wanawaingilia kinyume cha maumbile?
Kama ilivyo dhahiri kuwa Kanisa haliwezi kubariki ushoga, ndivyo vile lisivyoweza kubariki ufiraji, utoaji mimba, ulawiti, uzinzi, uwongo, au uabudu miungu na sanamu, na mengine yanayofanana na hayo, japo mambo hayo yapo, na wanaoyatenda tunaendelea kuhysiana nao kwenye maisha yetu ya kila siku.
Lakini kiimani, watu hawa wote tuwaendee kwa upole, upendo na unyenyekevu tuwafikishie ujumbe wa Mungu, kuwa Mungu anawapenda, na anawataka wabadilike, waoshi kwa kadiri ya maagizo na mpango wake.
Papa, katika kusisitiza kuwa Kanisa haliwezi kubariki dhambi, amesaini waraka maalum wa kuwaelekeza makasisi wote wote kuwa hairuhusiwi kubariki muungano wa mashoga (homosexuality union). Lakini shoga, bado ni mwana wa Mungu, anayestahili kutubu, na wana wa Mungu tunatakiwa kumwendea kwa upole na upendo kumfikishia ujumbe wa Mungu.