1. Utangulizi:
Mh. Mwenyekiti na Wajumbe,
Kama wengi wetu tunavyojua Kikosi Kazi cha Mh. Rais kiliundwa tarehe 23 Desemba 2021, kikiwa na wajumbe ishirini na nne (24). Kikosi Kazi kiliwasilisha mapendekezo yake kwa Mh. Rais tarehe Oktoba 21, 2022.
Kikosi kazi kilipitia hadidu za rejea, kikachambua hotuba za ufunguzi za Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, kikachambua mapendekezo yaliyotolewa katika mkutano wa wadau huko Dodoma, kikapokea maoni kutoka kwa wadau mbalimbali, na hatimaye kuainisha na kuandaa mapendekezo baada ya kufanya kazi kwa mda wa miezi kumi. Mapendekezo haya yaliyowasilishwa kwa Mh. Rais na Watanzania wote kwa ujumla hapo Oktoba, 2022, Ikulu Dar es Salaam.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuokoa mda, ninawasilisha mapendekezo tu. Nayo ni haya yafuatayo:
2. Mikutano ya Vyama vya Siasa
2.1. Kuhusu mikutano ya hadhara na mikutano ya ndani ya vyama vya siasa
Kikosi Kazi kilipendekeza kuwa:
Mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa iruhusiwe kufanyika kwa mujibu wa Katiba na Sheria;
Mikutano ya ndani ya vyama vya siasa iendelee kufanyika bila vikwazo vyovyote;
yafanyike marekebisho ya Sheria, ili kuhakikisha mikutano ya hadhara inafanyika kwa ufanisi. Sheria hizo ni pamoja Sheria ya Vyama vya Siasa Sura ya 258, Sheria ya Jeshi la Polisi na Huduma Saidizi Sura ya 322 na Kanuni za Maadili ya Vyama vya Siasa za Mwaka 2019.