MGOMBEA urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk John Magufuli, amewataka wanaosema kuwa hataweza kuleta mabadiliko kwa kuwa yuko ndani ya mfumo wa chama hicho, wakajifunze China.
Akizungumza katika mikutano, Dk Magufuli alisema China imefanya mabadiliko makubwa ya kiuchumi, kiteknolojia na kijamii, kwa kutumia chama cha Kikomunisti chenye mfumo wa kijamaa kama CCM.
Kwa mujibu wa Dk Magufuli, walichofanya katika nchi hiyo ni kutumia watu wa ndani ya chama hicho cha Kikomunisti, kuleta mabadiliko yanayoonekana dunia nzima leo mpaka Marekani imeshangazwa.
Nchi ya China ilikuwa chini ya Chama cha Kikomunisti chini ya Mwenyekiti Mao, walipopata uzoefu wakafanya mabadiliko bila kuondoa chama kilichokuwepo madarakani, alisema.
Dk Magufuli pia aliwaonya Watanzania kuwa uongozi wa nchi haujaribiwi na hata yeye alipochukua fomu za kuwania urais, alijua kuwa haombi urais kwa ajili ya majaribio, ndio maana alichukua fomu na kutafuta wadhamini kimya kimya, huku akimtanguliza Mungu mbele.
Aliwahadharisha Watanzania uwezekano wa kutokea watu watakaowapa fedha, ili wawachague na kuwataka wawaepuke kwa kuwa watakuwa na deni watakalotakiwa kulipa huko walikotoa fedha.
Alisema yeye deni lake ni kutumikia Watanzania wote bila kujali vyama vyao, lakini si deni la fedha kwa watu wenye fedha kwa kuwa hatoi fedha mahali popote ya kuomba kuchaguliwa.
Magufuli akielekea uwanjani ili kujinadi katika mkutano uliofanyika katika viwanja vya Ruanda Nzonve, Mbeya
Magufuli akiwa na watoto ambao walikuwa na hamu ya kutaka kumsalimia kwa kumpa mikono.
Magufuli akijinadi kwa wananchi katika mkutano
Wananchi wakisikiliza kwa makini hotuba ya Mgombea Urais kwa Tiketi ya CCM, John Magufuli
JPM