Viongozi wa dini katika madhebu mbalimbali nchini wameshauriwa wasiwe wanasiasa wala kuwa sehemu ya wachochezi kwa kuwa wao ni sehemu ya kimbilio pindi nchi inapokuwa katika changamoto.
Aidha, wamekumbushwa wajibu wa kuiombea Tanzania hususan katika mwaka huu wa uchaguzi mkuu.
Hayo yameelezwa na wachungaji kutoka Tanzania na Kenya wa Kanisa la Wadventista Wasabato walipokuwa wakihitimisha Wiki ya Uamsho iliyokuwa na maombi mbalimbali ikiwemo kuiombea amani, umoja na mshikamano wa taifa.
Wiki ya Uamsho imeandaliwa na Kwaya ya Gethsemane Group Kinondoni (GGK) kutokea Kanisa la Wadventista Wasabato Kinondoni Jijini Dar es Salaam ambapo katika maombi hayo pia wamewaalika wachungaji wa Kanisa hilo kutoka nchini Kenya.
Katibu wa Jimbo la Mashariki Kati mwa Tanzania wa Kanisa la Waadvestita Wasabato Tanzania Mchungaji Shashi Musa Wanna, amesema wamekuwa katika maombi kwa wiki nzima, pia wametumia nafasi hiyo kuwa na mahubiri pamoja.
"Tulikuwa na wiki ya uamsho wa kiroho katika kanisa letu lakini pia kuliombea taifa letu na wachungaji wenzetu kutoka Kenya ambao tulikuwa nao. Wenzetu wana uzoefu mkubwa wa mambo ya siasa yanayoendelea Kenya. Tumehimiza maombi na umuhimu wa amani katika nchi yetu.
Kwa upande wake Mhubiri kutoka Kenya, Mchungaji Patrick Muthee amesema katika zama hizi ambazo dunia imeharibika wakati mwingine makanisa na waumini wake wanajaribiwa huku akitahadharisha kuwa Kanisa linapoingia katika siasa ni changamoto kwa sababu roho ya Mungu inaondoka.
"Kazi ya Kanisa ni kuleta watu pamoja na tunatambua Mungu ndio huchagua viongozi sisi kama waumini Mungu anatutumia katika hali ile ya kupiga kura, lakini Mungu anajua njia iliyo bora. Hivyo Kanisa, viongozi, wachungaji na masheikh tuzungumze na waumini wetu," amesema.
Kwa upande wake Mchungaji Haruni Muturi wa Kanisa la Wadventista Wasabato kutoka Kenya, amesema katika wiki ya uamsho wametumia nafasi hiyo kujihoji myoyoni na kujitoa upya kwa Yesu Kristo kwa sababu wanajua kuna majaribu.