Jeshi la Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja linawashikilia watu kumi na mbili kwa tuhuma za kukutwa wakila mchana hadharani kipindi hiki cha Mwezi mtukufu wa Ramadhan ambao wanaifanya kuwa idadi ya watu waliokamatwa kwa tuhuma za kutenda makosa mbalimbali kufikia sitini na mbili
Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini magharibi Unguja Kamishna Msaidizi wa Polisi ACP Abubakar Khamis Ally amesema kufuatia video iliyosambaa mitandaoni ikiwaonesha baadhi ya watu katika eneo la viwanja vya mnazi mmoja Zanzibar wakila hadharani wakati wa mchana wa Ramadhani, Jeshi hilo lilifanya msako na kuwakamata watu wapatao kumi na mbili wakiwa na vielelezo ambapo amesema wanaendelea na taratibu nyengine ili kuwafikisha Mahakamani.
Aidha ameyataja makosa mengine ni pamoja na unyang’anyi, Madawa ya kulevya na makosa mengine ambapo watuhumiwa wanashikiliwa na Polisi na wengine tayari wameshahukumiwa Mahakamani.
SAUMU YA RAMADHANI
Kufunga Saumu ni nguzo ya nne ya Kiislamu na hakika ya Kufunga ni kuacha kula na kunywa toka asubuhi mpaka magharibi kama Mungu alivyoamrisha. Na kuacha kila mambo mabaya, kama Qur'an tukufu isemavyo kwamba:-
يٰٓـاَيُّهَا الَّذِيۡنَ اٰمَنُوۡا كُتِبَ عَلَيۡکُمُ الصِّيَامُ کَمَا كُتِبَ عَلَى الَّذِيۡنَ مِنۡ قَبۡلِکُمۡ لَعَلَّكُمۡ تَتَّقُوۡنَۙ
Enyi mlioamini, mmelazimishwa kufunga Saumu kama walivyolazimishwa wa kabla yenu ili mpate kumcha Mungu.
Kusudi la Saumu limeelezwa kuwa ni kupata Taq-waa, yaani, ucha-Mungu. Neno Taq-waa, linatumiwa katika Qur'an kwa maana tatu:
(1) Kuepukana na maumivu,
(2) kuepukana na dhambi,
(3) kufikia utakatifu ulio juu wa mambo ya kiroho.
Kufunga saumu ya Ramadhani ni lazima juu ya kila Mwislam isipokuwa watoto wadogo, wagonjwa, wadhaifu sana, wenye mimba, wanyonyeshao na wasafiri.
Ijapokuwa hakuna adhabu ya kimwili ikiwa mtu ataamua kutofunga, ila Mwenye kuacha kufunga saumu ya Ramadhani bila udhuru wowote anapata dhambi kubwa na mwenye kufunga kisha akafungua bila sababu basi juu yake afunge siku sitini kwa mfululizo, au alishe maskini sitini.
Mwezi wa Ramadhani ni mwezi mtukufu zaidi kwenye kalenda ya mwaka wa kiislamu. Ni mwezi pia unaofahamika kama mwezi wa toba, kipindi ambacho waumini wa dini hiyo wanajisogeza karibu zaidi na Mola wao kwa ibada mbalimbali ili wavune thawabu.
Ni dhahiri pia kipindi hiki cha mfungo wa Ramadhani kunakuwa na mabadiliko mengi katika mfumo wa maisha na matendo ya watu.
Katika nchi ambazo raia wake ni wa dini mbalimbali kama Afrika Mashariki, maswali mengi huibuka kipindi hiki juu ya nini kinatakiwa kifanyike ama kisifanyike. Wale ambao si waislamu huwa na maswali mengi juu ya nini wanaweza kufanya ama kutofanya mbele ya ndugu, jamaa au marafiki wa kiislamu.
Tendo kubwa ambalo linaonekana moja kwa moja kufanywa na waislamu katika kipindi hiki cha mfungo ni kujizuia kunywa na kula kutoka alfajiri (kuchomoza kwa jua) mpaka magharibi (kuzama kwa jua).
Haijalishi, mtu awe masikini ama tajiri, awe na chakula ndani ama asiwenacho, madhali wanakiri kwa yakini kuwa ni waislamu basi hujizuia kula na kunywa.
Katika mazingira yenye watu wa imani tofauti, mathalani mtaani, shuleni au hata kazini sio wote wanaofunga, na wengine hutembea na vyakula vyao.
SWALI HUWA, JE, NAWEZA KULA MBELE YAKO AU MBELE YA WATU WENGINE?
Jibu lake hutegemeana na mtu na mazingira husika. Kuna wale ambao hawana tatizo lolote kwa mtu kula mbele yake anapokuwa amefunga, ila wengine wanatafsiri ukifanya kitendo hicho kama kutowaheshimu na kuwapa majaribio ya kiimani kwa makusudi. Kama upo kazini ama shuleni, ni vyema zaidi ukatumia maeneo maalumu yaliyotengwa kwa chakula.
Mazingira ya eneo pia huchangia katika hili. Katika nchi nyingi ambazo zinafuata sheria za kiislamu, kula hadharani wakati wa mchana wa mwezi wa Ramadhani huwa ni kosa. Na ukifanya hivyo unaweza kujipata mikononi mwa vyombo vya usalama,
Ambapo jambo hili sio sheria wala sio Fundisho la Islam sawa na Mtukufu Mtume Muhammad saw alivyotuelekeza na Kutufundisha.
Ndiyo maana Ramadhani kwa hakika inahusu kujiboresha katika ngazi zote:
kujenga uhusiano wa kina zaidi na Mwenyezi Mungu, kutimiza vyema haki za wanadamu wenzetu, na kurekebisha maadili na matendo yetu wenyewe ili kuwa watu bora zaidi.
RUHUSA ZA MTU KULA NDANI YA MWEZI WA RAMADHANI.
1️⃣
Ugonjwa
Yaruhusiwa kwa mgonjwa kula ndani ya mwezi wa Ramadhani; kwa kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu:
اَيَّامًا مَّعۡدُوۡدٰتٍؕ فَمَنۡ كَانَ مِنۡكُمۡ مَّرِيۡضًا اَوۡ عَلٰى سَفَرٍ فَعِدَّةٌ مِّنۡ اَيَّامٍ اُخَرَؕ وَعَلَى الَّذِيۡنَ يُطِيۡقُوۡنَهٗ فِدۡيَةٌ طَعَامُ مِسۡكِيۡنٍؕ فَمَنۡ تَطَوَّعَ خَيۡرًا فَهُوَ خَيۡرٌ لَّهٗ ؕ وَاَنۡ تَصُوۡمُوۡا خَيۡرٌ لَّـکُمۡ اِنۡ كُنۡتُمۡ تَعۡلَمُوۡنَ
Kwa siku zilizohesabiwa. Lakini miongoni mwenu
awaye mgonjwa au katika safari, basi atimize hesabu katika siku zingine. Na wale wanaoweza, watoe fidia kwa kumlisha maskini. Na atakayefanya wema kwa radhi ya nafsi yake, basi ni bora kwake; na kama mkifunga ni bora kwenu, ikiwa mnajua.
2️⃣
Safari
Inaruhusiwa kwa msafiri kula ndani ya Mwezi wa Ramadhani, na inamlazimu kuilipa saumu hiyo baadaye, kwa kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu:
اَيَّامًا مَّعۡدُوۡدٰتٍؕ فَمَنۡ كَانَ مِنۡكُمۡ مَّرِيۡضًا اَوۡ عَلٰى سَفَرٍ فَعِدَّةٌ مِّنۡ اَيَّامٍ اُخَرَ
Kwa siku zilizohesabiwa. Lakini miongoni mwenu awaye mgonjwa au
katika safari...
3️⃣
Wajawazito na Wanyonyeshao n.k