Michango ya Mwenge yazua manung`uniko Mbeya
Na Thobias Mwanakatwe
17th May 2011
B-pepe
Chapa
Maoni
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, John Mwakipesile
Mwenge wa Uhuru umezua kizaa zaa mkoani hapa baada ya serikali kutangaza kusitisha sherehe za kuuwasha mkoani hapa kama ilivyokuwa tangu mwaka jana ambapo watumishi wa serikali na wananchi wametaka warejeshewe fedha zao zaidi ya Sh.milioni 100 walizokuwa wamechangishwa kwa ajili ya kazi hizo.
Wakizungumza na NIPASHE jana kwa nyakati tofauti mjini hapa, walisema hawakubaliani na tamko la Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, John Mwakipesile kwamba fedha zilizokusanywa kwa ajili ya kazi hiyo zitawekwa benki ambapo zitatumika mwakani wakati wa mbio za Mwenge wa Uhuru.
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, John Mwakipesile juzi akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake alisema Mwenge wa Uhuru hautawashwa tena mkoani hapa na badala yake utakwenda kuwashwa kijijini Butiama mkoani Mara kwa ajili ya kumuenzi Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere.
Mwakipesile alisema hatua ya kuuwasha Mwenge huo kijijini Butiama inatokana na kwamba huu ni mwaka wa 50 tangu nchi ipate uhuru hivyo viongozi wa kitaifa wamekaa na kukubaliana kuwa ukawashwe kijijini kwa Baba wa Taifa ikiwa ni ishara ya kumuenzi.
Hata hivyo, watumishi wa serikali ambao waliomba majina yao yasitajwe walisema kwa kuwa Mwenge wa Uhuru hautawashwa tena Mbeya, serikali ya Mkoa wa Mbeya itumie busara kuwarejeshea fedha zao kwasaabu hawana imani kama kweli zitakuwa na usalama zikiwa chini ya viongozi waliopewa jukumu ya kuzikusanya.
Tunachotaka turejeshewe fedha zetu hiyo hadhithi ya kwamba tutaziweka benki hatukubaliani nayo, hivi sasa serikalini ufisadi umetawala kila kona kwa hiyo tuna uhakika hata fedha zetu tulizochangishwa zitachakachuliwa,alisema mfanyakazi mmoja kutoka Halmashauri ya Jiji la Mbeya ambaye aliomba jina lake lisitajwe.
CHANZO: NIPASHE
0 Maoni | Kuwa wa kwanza kutoa maoni