Leo nimeisikiliza hotuba fupi ya Mwenyekiti wa CHADEMA, Bwana Freeman Mbowe.
Katika hotuba yake hiyo fupi, Bwana Mbowe kapendekeza Rais Magufuli aitumie nafasi yake ya urais kuleta maridhiano nchini.
Mimi sikubaliani na hilo. Maridhiano [reconciliation] ya nini? Kwani Watanzania tumetendeana ubaya kiasi cha kufikia hatua ya kuwa na maridhiano?
Afrika Kusini ilibidi wawe na maridhiano baada ya Apartheid kuondolewa. Hilo lilibidi kwa sababu ya ukiukwaji mkubwa wa haki za kibinadamu uliotendeka kipindi cha Apartheid. Ilibidi waandike ukurasa mpya wa historia ya taifa lao.
Rwanda nao ilibidi waunde tume ya kudumu ya Umoja wa kitaifa na maridhiano. Kilichotokea Rwanda nacho kilikuwa ni ukiukwaji mkubwa kupita maelezo wa haki za binadamu. Hakukuwa na njia nyingine ya kusonga mbele kama taifa kama wasingesameheana na kuridhiana kutokana na kilichotokea mwaka 1994.
Mwaka 2008 Kenya nao ilibidi waunde tume ya Ukweli, Haki, na Maridhiano kwa kile kilichotokea baada ya uchaguzi wa mwaka 2007 na pia kwa matukio mengine yaliyotokea kabla ya hapo.
Sasa sisi Watanzania maridhiano ni ya nini?
Ndiyo, kuna matukio ya hapa na pale ambayo yametokea. Baadhi ya matukio hayo yana mwelekeo na harufu ya kisiasa na yenye kukiuka haki za kibinadamu.
Lakini, kama taifa, bado kabisa hatujafikia kiwango cha kuwa na sababu ya maridhiano.
Watanzania bado tuna umoja. Kwa ujumla hatuchukiani kwa misingi ya kikabila, kidini, wala kisiasa.
Tumechanganyikana mno. Waislamu wameoana na kuzaa na Wakristo. Wasio na dini nao wamo humo humo.
Watu wamechangiana makabila. Unakuta mtu babu yake ni Mpare, bibi yake ni Mnyamwezi, mke wake ni Mhaya, yeye mwenyewe ni nusu Mnyamwezi nusu Mhaya, wanae wana asili ya Uhehe, Upare, Uhaya, Unyamwezi, na kadhalika.
Ambalo naliona ni la muhimu ni ustaarabu.
Ustaarabu [civility] katika namna tunavyotendeana licha ya kuwa na tofauti zinazotutenganisha kisiasa na kiitikadi.
Tumezikubali siasa za vyama vingi. Siasa za vyama vingi ni siasa za kiushindani. Ushindani una mambo mengi. Mambo hayo, kwa uchache, ni propaganda, hisia kali, kutambiana, na kadhalika.
Sasa, kwenye muktadha huo wa ushindani, tunaweza kukumbushana kuhusu ustaarabu na uungwana, utawala wa kisheria, haki sawa kwa wote, na ufuatwaji wa katiba. Kwenye hayo sina tatizo.
Lakini hizi habari za kusema sijui tuwe na maridhiano sizikubali. Bado kabisa hatujafika huko.
Najua mpo mtaosema kwamba si busara mpaka tufike huko ndo tuwe na maridhiano na blah blah.
Nami nasema hivi, kama hatujafika huko kwa nini tufanye kitu juu ya jambo ambalo halipo ilhali kuna mengine tuwezayo kuyafanya ili kuboresha hali iliyopo?
Hatuhitaji maridhiano. Tunachokihitaji ni ustaarabu na uungwana katika vile tunavyotendeana.