LISU LEO UMEFURAHISHA WALIOWENGI, HONGERA SANA
Na, Robert Heriel
Siku ya Leo imeisha vizuri kwa waliowengi, hasa walioisikiliza Hotuba fupi ya Tundu Lisu. Ilikuwa Hotuba iliyobeba matumaini makubwa sana kwa kila mwenye akili.
Lisu amezungumzia mambo makuu yafuatayo;
1. Katiba Mpya
2. Maslahi ya Wafanyakazi
3. Elimu, kubadilisha falsafa katika elimu yetu.
4. Ajira
5. Uhuru katika maendeleo na wala sio utumwa katika maendeleo.
6. Kodi na biashara n.k.
1. Katiba Mpya
Katiba Mpya ile ya Warioba itarudishwa na kupitishwa. Mamlaka ya Rais yataangaliwa na kufanyiwa maboresho kwa kupunguza mamlaka. Katika hili amegusa Watanzania wote. Ni kusema Kila Mtanzania atakayesikia habari hii lazima amuunge Mkono. Labda awe mwendawazimu au mtoto mdogo asiyeelewa mambo ndio atapingana na Tundu Lisu. Katika hili Lisu angepewa Kura 99% na Watanzania kupitia hoja hiyo tuu, 1% wasingempa kura kwa sababu ya uelewa mdogo au wehu.
2. Maslahi ya Wafanyakazi
Lisu hapa angegusa kundi la watumishi wa serikalini, waalimu, manesi, madaktari, Polisi, n.k. Kundi hili lingemuunga mkono kwa 80%, 20% hawa wasingemuunga mkono kutokana na imani yao kuwa ndogo.
Lisu anasema kuwa wafanyakazi hawajaongezwa mishahara tangu 2015. Yeye kasema ataangalia namna ya kufidia ugumu huo, na serikali yake itajali maslahi ya wafanyakazi.
Pia habari ya mifuko ya kijamii, fao la kujitoa, mafao aligusia.
3. Elimu
Lisu hapa kawagusa Watanzania wote kwa ujumla. Hata wajinga hawapendi kuwa wajinga, wanapenda elimu. Hoja hii itaungwa mkono na makundi yote, kuanzia watoto wadogo, mpaka wazee.
Elimu yenye maarifa itakayomjenga mwanafunzi kukabiliana na mazingira pale amalizapo masomo. Sio elimu ya kukabiliana na mitihani shuleni huku kichwa kikibaki kopo
4. AJIRA
Amesema, atahakikisha sekta binafsi zinaendesha shughuli zake veyma kwa kupunguza kodi, na kuweka mazingira rafiki kwa kila atakayetaka kuwekeza mtaji wake huko.
Anafahamu serikali haiwezi kuajiri vijana wote lakini inachoweza kusaidia vijana ni kuwatengenezea mazingira rafiki hasa kwa upande wa kodi ili kuwapa vijana nafasi nzuri ya kujiajiri na kuajiriwa. Hapa kagusa vijana wpte na watu wenye umri wa kufanyakazi.
5. Uhuru Katika Maendeleo na sio Utumwa katika maendeleo
Moja ya mambo anayosisitiza Tundu Lisu ni pamoja na uhuru katika maendeleo. lisu anamtazamo kuwa Maendeleo yanayogusa uhuru wa watu hayo sio maendeleo bali ukandamizaji.
Watu wawe huru kutoa maoni yao, kila mtu awe sawa mbele ya sheria, pasiwepo miungu watu. Hapa kagusa maisha ya watu wote
6. Kodi na Biashara
Kutokana na muda kuwa mdogo Lisu hakuweza kuendelea na kujieleza vyema.
Tumefurahishwa sana na Hotuba yako ndugu Tundu Lisu. Umefurahisha watu wengi
MAMBO YA KUBORESHA
1. MUDA WA UWASILISHAJI
Chadema mjitahidi sana kurekebisha Ratiba zenu kusudi zisimbane sana Mgombea wenu. Angalau Tundu Lisu uanze hotuba zako saa 11:00 na kuzihitimisha saa 12:00. Uwe na Lisaa limoja la kuelezea wananchi kile ulichofanya leo.
2. UPANGAJI WA HOJA
Tundu Lisu jitahidi uanze na hoja zinazoamsha hisia za watu wengi zenye manufaa. Kwa mfano hoja ya Maslahi ya wafanyakazi, ajira, ulinzi na usalama, uhuru, biashara, kilimo n.k Hoja ya kubomolewa nyumba ni nzuri lakini haikupaswa iwe namba moja huku ukijua muda wako ni mdogo. Kumbuka Hoja zote ni muhimu lakini lazima uwe na mpangilio mzuri kulingana na uzito.
3. VYOMBO VYA HABARI
Watanzania sio wajinga, wengi wanafahamu hila mnazofanyiwa. Lakini ni lazima mjitahidi kutafuta utaratibu wa kuhakikisha mikutano yenu inaonekana. Nimeona mna CHADEMA Online Tv, nunueni drone kisha zichukue habari kwa namna ipendezayo.
Fuatilieni ni kitu gani kinafanya mnakata kata pindi mnapokuwa live. Ingawaje hila zinaweza kuhusika.
Hakikisheni mchukua Kamera anaonyesha mambo kwa lengo maalumu. Kamera isionyeshe sehemu moja, hii itaondoa tension ya watazamaji, na hata kamera ikihama hama basi kamareman ajue kwa nini anaihamisha.
4. MICHANGO
Kuna michango ya hali na mali. Mali mmefanya vyema kuwachangisha watu pesa, sasa lazima kwenye suala la hali, mtafute vijana werevu, wenye vipaji vya uhakika, wala sio vya kubeza, Kisha muandae namna ya kufungua mkutano.
Kwa mfano; Jumatatu mtakuwa Arusha, Mnaweza kutafuta vijana chipukizi wenye mapenzi na Chama chenu. Waandalwe kwa siku moja ku-perfome iwe ni igizo, iwe kichekesho, iwe nyimbo. waanze kufanya mambo hayo saa nane mpaka saa kumi. Kisha mambo ya kisiasa yaanze saa kumi mpaka 12. Muhimu hakikisheni mnafanya mambo kisomi, kama watu wenye akili, kwa utaratibu.
Vijana chipukizi ni muhimu kwa sababu kwao itakuwa uwanja wa wao kujitangaza na kuonyesha vipaji vyao,. Sio gharama sana.
5. WATAKAOSIMAMA JUKWAANI
Hakikisheni mnasimamisha watu wanaojua nini wanaongea kwa sababu gani. Kila atakayeongea hakikisheni anawatia hamasa watu, hakikisheni watu wanatamani aendelee kuongea. Kila atakaye ongea awe amebeba ujumbe mahususi, kisha atoe ujumbe wa jumla ambao ni msisitizo kwa kila atakayepanda.
Wasemaji muwagawe katika makundi yafuatayo
1. Watoa ujumbe mkali wenye kuamsha hisia
2. Wachekeshaji na wenye kutia moyo
3. Watoa takwimu na historia
4. Watoa hoja tuli zisizoamsha hisia lakini zinazoingia akilini.
Hakikisheni kila anayepanda anazingatia hivyo. Watu wasijikite kwenye mfumo mmoja tuu. Sio mzungumzaji wa kwanza kaongea kwa kuamsha hisia za huzuni na kusikitisha, na kamaliza hivyo hivyo kisha mzungumzaji anayefuata anaendelea vile vile, hapana, haiwi hivyo. Muweke mambo kimkakati, kama wa kwanza kaumiza hisia za watu, basi anayefuata atoe matumaini kuwa hayo yote yamefanyiika lakini huo ndio mwisho wake, sisi tutafanya a, b, c ......!
6. MASHAMBULIZI
Tumieni muda mchache kushambulia, yaani shambulieni 30% alafu 70% elezeni kwa nini ninyi bora. Kwa mfano mtoa hotuba mwenye lisaa limoja, hakikisha kila baada ya dakika kumi dakika mbili unashambulia adui kisha nane unaonyesha kwa nini wewe ni bora. Muda wa mashambulizi ndio kutupiana vijembe, kejeli, mizaha, mafumbo n.k
7. UMALIZIAJI
Hakikisha unamalizia hotuba zako kwa kuwatia watu changamoto, hasa ukiwaonyesha madhaifu ya adui yako. Kisha uwaachie homework ya kuwataka je hawataki kufanyiwa mambo bora na kuondokana na kadhia hiyo.
MADHAIFU
1. Hoja ya kubomolewa nyumba watu, umeshindwa kuielezea vyema.
Ulipata ukakasi na maelezo yako yalikuwa yanachechemea. Pengine ungeulizwa kwamba ni halali kujenga eneo la barabarani sijui ungejibu nini
2. Hoja ya kupunguza kodi ilikuwa na ukakasi pia
Ukipunguza kodi hasa kwa waagiza mizigo nje ya nchi, huku ukishindwa kueleza namna viwanda vya ndani vinavyozalisha bidhaa zetu vitawezaje kukua, hapo kidogo kuna ukakasi. Kodi na tozo hasa kwa bidhaa kutoka nje hujui ni mbinu ya kulinda viwanda vyetu vya ndani? Kwa upande wa kodi za ndani, hujaeleza ni kwa namna gani serikali yako itapata mapato kwa nji nyingine(vyanzo vipya vya mapato) ili ukipunguza kodi kwa wananchi serikali yako iweze kujiendesha. Umeeleza kwa hoja inayoteleza ubongoni.
3. Muda wako ni mdogo wa kuwasilisha, pengine ungeweza kujieleza katika madhaifu hapo juu kama ungekuwa na muda wa kutosha.
Msijikite kwenye malalamiko, zaidi mjikite kwenye namna mtakazokabiliana na changamoto zinazowakabili. Kama mlivyofanya kwenye suala la michango, hamkulalamika.
Mwisho niseme kuwa, sasa Kampeni ndio zimeanza, nimefurahishwa na Hotuba fupi ya Tundu Lissu.
Kesho nitaeleza Hotuba ya Mhe. Magufuli. Kisha nitatoa muelekeo wangu kuwa nani ninamuona anaweza kuwafurahisha Watanzania.
Zingatia: Sitapendelea mtu. Kile ulichoongea ndicho nitaki-judge na kukitolea muelekeo wangu. Sina Maslhai na chama chochote, sina maslahi na mgombea yoyote. Hakuna watakachoniongezea binafsi. Ninamaslahi na nchi hii. Sitakuwa mnafiki kwa yeyote, sina ninayemhofia.
Tuipende nchi yetu.
Acha nipumzike kwanza, leo sitaki maswali
Robert Heriel
Taikon wa Fasihi
0693322300