Na Jonas Bernard Pambili
Mkatekumeni.
Ilala, Dar es Salaam.
Nimesoma tamko la Baraza la Maaskofu (TEC) na leo Jumapili nimewasikiliza Mapadre wakilisoma kwenye Ibada.
Ni tamko la kupinga uwekezaji katika bandari ya Dar es Salaam ambao Serikali ya Awamu ya Sita inakusudia kuufanya baada ya kukubaliana na Serikali ya Dubai. Nimezisoma hoja zilizoandikwa na nimejiuliza maswali mengi na kwa kweli nimeshangaa sana sana.
Kwa nilivyofuatilia kwenye vyombo vya habari kuhusu jambo hili, viongozi wa Dini wakiwemo viongozi wa Kanisa Katoliki wakiongozwa na Padre Dk. Charles Kitima walipata muda wa kukutana na viongozi wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi na Mamlaka ya Bandari na wakafafanuliwa kipengele kwa kipengele na Washeria wa Serikali waliohusika kuandika mkataba wa makubaliano kati ya Serikali yetu na Dubai.
Nilimsikia huyuhuyu Katibu wa TEC Padre Dk. Charles Kitima akisema wameelewa na wanawataka Serikali waendelee kutoa elimu ya kutosha.
Lakini pia nilibahatika kufuatilia mdahalo kati ya Serikali na Wahariri uliofanyika katika hoteli ya Rotana Dar es Salaam na mkataba ulichambiliwa kipengele kwa kipengele. Kwangu mimi mkutano ule ulimaliza maswali yote na wasiwasi wote,
kwamba kumbe;
1. Hakuna bandari inayouzwa
2. Hakuna mkataba wa milele
3. Katika bandari ya Dar es Salaam uwekezaji utakaofanyika utahusu sehemu ya bandari kulingana na mikataba kati ya TPA na DP World wakavyokubaliana.
4. Kwamba umri wa mkataba utategemea umri wa mikataba ambayo itakayoingiwa kati ya TPA na DP World. Yaani kama mikataba hiyo itakuwa ni miaka 20 basi na mkataba huu utakuwa miaka 20 kama itakuwa miaka 22 kama ilivyokuwa TICTS mkataba huu pia utakuwa miaka 22.
5. Kwamba sio kweli kwamba DP watapewa bandari zote za Tanzania. Ni sehemu ya bandari ya Dar es Salaam tu.
6. Kwamba endapo DP World watapewa mkataba wa uwekezaji basi watapewa haki ya kutumia ardhi na sio kumiliki ardhi.
7. Kwamba uwekezaji huu hauna tofauti na TICTS ambao baada ya mkataba kuisha wameondoka. Kumbe hata wakija DP World kuna siku wataondoka.
8. Kwamba kumbe mkataba unaweza kuvunjwa wakati wowote upande wowote utakapoona inafaa.
9. Kwamba ajira za Watanzania zitalindwa na zitaongezeka.
10. Kwamba mapato ya forodha yataongezeka kutoka shilingi trilioni 7.7 hadi trilioni 26.6 kutokana na kuongeza kwa mzigo wa bandari kutoka tani Milioni 20 za sasa hadi tani Milioni 58 kwa mwaka.
11. Kwamba uendeshaji wa sasa wa bandari una mapungufu makubwa ya kimifumo na teknolojia na wawekezaji watatatua changamoto hizo ili wizi na utoroshaji wa mizigo vikome na pia ukwepaji kodi ukomeshwe.
12. Kwamba kwa kutowekeza katika bandari yetu tumeanza kupoteza biashara na kuna hatari huko mbele tukapoteza kabisa licha ya kuwa katika eneo zuri la kibiashara kutokana na sababu za jiografia.
13. Kwamba tusipofanya uwekezaji huu, wenzetu Kenya na Msumbiji wanaendeleza bandari zao kupitia sekta binafsi na watakuja kuchukua biashara yote ya bandari.
14. Kwamba tusipopanua uwekezaji bandarini hata reli yetu (SGR) itakosa biashara.
15. Na kwamba hali ilivyo sasa bandari yetu ina gharama kubwa na hivyo haivutii wateja.
Nilitegemea kutokana na sababu hizi na nyingine ambazo kwa bahati mbaya zinapotoshwa sana na vyama vya upinzani hasa CHADEMA na wamezichukua kama hoja yao ya kisiasa, TEC wangekuja na mtazamo wenye ukweli na kuwaongoza Wakatoliki kwenye ukweli.
Nilitegemea kama TEC hawakubaliani wangekwenda kuwaona viongozi wa Serikali akiwemo Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ambaye wamekuwa na mikutano nae na kumueleza wasiwasi wao badala ya kutoa tamko lenye mtizamo wa siasa za upinzani.
Sikutegemea kuona namna Padre Dk. Kitima anavyohamasisha kwa mbwembwe na ushabiki kupinga uwekezaji huu.
Sikutegemea kuona TEC wanatoa maelekezo ya kusomwa kwa tamko hilo katika Ibada za leo Jumapili kwa Waumini wa Kanisa Katoliki kote nchini. Wametukosea sana.
Nimeshangaa sana juu ya mwelekeo huu wa Maaskofu, nikijiuliza;
1. Maaskofu wameamua kuwa wapinzani wa Serikali iliyowekwa na Watanzania?
2. Kwamba Maaskofu wanataka Wakatoliki waanze kunyukana na Serikali?
3. Maaskofu hawajui ndani ya viongozi wakuu wa Serikali wamo viongozi Wandamizi akiwemo Makamu wa Rais ambaye anahudhuria Ibada kila siku na kila Jumapili? Wanamweka kwenye wakati gani?
4. Maaskofu (TEC) wakiambiwa wadhibitishe hayo waliyoyaandika wanao ushahidi?
5. Na endapo Serikali itaamua kuendelea na utekelezaji ndio tuseme uhusiano wa Kanisa Katoliki na Serikali umeingia doa?
6. Wanadai Watanzania wanakataa mkataba huu, wamekusanya lini maoni ya Watanzania na kwa mfumo upi? Au siku hizi TEC ikisikia maoni ya CHADEMA ndio yanakuwa maoni ya Watanzania?
Lakini kubwa kuliko yote, hivi TEC wanajua hii vita ya kupinga uwekezaji bandarini chanzo chake ni nini?
Au Baraza letu wamepata ushawishi wa watu wasiopenda uwekezaji Bandarini? Wasiopenda mifumo itakayodhibiti upigaji ifungwe? Au kitu gani hiki?
Mimi Mkatoliki kama nilivyosema, lakini kwa nini wanatoa tamko kama hili wakati wanajua Kanisa lina watu wengi ambao hatuna msimamo huo? Kwa nini hawakuitisha makongamano ya Kikanisa tujadili ili wasikie maoni ya Waumini Wakatoliki?
Kwa nini Padre Dk. Kitima unawaongoza Maaskofu kutoa matamko kama haya?
Na naomba niwe mkweli, huyu Padre Kitima mara nyingi ameongoza kutoa matamko yanayoharibu uhusiano wa Kanisa Katoliki na Serikali, hakuna wakati amewahi kuwa katika uhusiano mzuri na Serikali. Kwa sisi tunaomjua kutoka Chuo cha Kanisa Katoliki cha SAUT ni mtu ambaye huwezi kumtofautisha na viongozi wa upinzani, yeye kwake kila kinachofanywa na Serikali ni kibaya tu. Sasa sisi Wakatoliki sio wote ni wanachama wa upinzani.
Nawaomba Maaskofu mtafakari tamko lenu, lakini naomba mtafakari kuendelea kuwa na Padre Kitima kama Katibu wa Baraza. Haya mambo hayatujengi kama taasisi ya Dini yenye heshima katika nchi yetu, yanatuweka kwenye mwelekeo wa kisiasa kuliko mwelekeo wa kiimani. Najua mnajenga hoja zenu mara nyingi kuhusu uhalali wa kuingilia masuala ya Kisiasa, hivi mmewahi kufikiria kama Mufti nae akitoa matamko kama hili lenu hadharani nchi tunaiweka wapi?
Sisi Waumini wa Makanisa na Misikiti tunapokuja Kanisani na Msikitini kusali na kuswali tunakuja kupata neno la Mungu na sio kusikiliza siasa. Tunakuja kupata tulizo la moyo na sio taharuki. Tukitaka siasa tunakwenda kwenye mikutano ya CCM au CHADEMA au ACT na vingine.
Haya mmetoa tamko mimi sikubaliani nanyi, ukatoliki wangu mbele yenu Maaskofu ambao ndio viongozi wangu Wakuu nauweka wapi? Nakujaje kuungama kwa mtu ambaye sina imani nae.
Haya mambo yamesababisha watu wengi hawapendi kwenda Makanisani kwa sababu kwa mtu mwenye akili za kuchambua mambo anaanza kuona Kanisa linaingia kwenye ajenda zisizo zake.
Jambo hili limeanza pia kuchukua sura ya kutugawa Watanzania kwa misingi ya Kidini na Kikanda, je mnataka tuingie huko? Nilitarajia TEC ndio muongozo kuondoa dosari hii badala ya kuchochea.
Kwa kweli Maaskofu mmetukosea sana na nawaomba Wakatoliki wenzangu tukatae mambo haya. Na tuwaambie viongozi wetu waziwazi kuwa wanatukosea. Ingekuwa Serikali imewashambulia Kanisa ningeelewa lakini kwenda kuishambulia Serikali ambayo siku zote imefungua milango ya kuwasiliana na Kanisa Katoliki sio sawa, tena Serikali ambayo imetangaza mara nyingi kuunga mkono Kanisa. Na kama kuna viongozi wa Kanisa wanapenda siasa, waruhusiwe kwenda kufanya siasa na sio kutumia nyumba za Ibada kufanya siasa, mnatukwaza tusiopenda mabishano ya kisiasa.
Naamini ujumbe umefika na asanteni sana.
Mwisho naomba kuwasihi Wakatoliki tusali sana, tuliombee Kanisa na tuwaombee viongozi wetu wa Kanisa wakumbuke misingi ya Kanisa, wakumbuke wanaongoza watu wenye itikadi tofauti, wakumbuke amani ni Ibada.