CHARLES KITIMA ACHA KUTUMIA KANISA KATOLIKI KUENEZA CHUKI ZA WAZI DHIDI YA RAIS SAMIA SULUHU
Na, Nulphin Charles Heche
Kwa mara nyingine, Kikundi kidogo cha wanachama wa Chadema ambao pia ni viongozi ndani ya Kanisa Katoliki wakiongozwa na Charles Kitima wameamua kuonyesha chuki za wazi kwa kusambaza kipeperushi kinacholenga kujenga chuki kati ya serikali na waumini wa Katoliki nchini.
Charles Kitima ambaye amekuwa akifanya shughuli mbalimbali za Chadema bila kificho amevuka mipaka ya kazi zake kama kiongozi wa kidini akijikita katika kutengeneza na kusambaza chuki dhidi ya serikali kwa madai ya kupinga uwekezaji katika Bandari ya Dar es salaam kama ilivyo ajenda ya chama chake.
Mawasiliano mbalimbali yanayofanywa na Ndg. Charles Kitima na kundi lake kuwashawishi viongozi wengine wa Kanisa Katoliki nchini ili waunge mkono hoja za Chama cha Demokrasia na Maendeleo na kueneza chuki dhidi ya serikali ni kinyume cha taratibu kwani Kanisa Katoliki si la CHADEMA.
Heshima ya Kanisa Katoliki ni kubwa kuliko maslahi ya Charles Kitima na rafiki zake wachache. Kueneza chuki dhidi ya Rais na serikali yake ni ukosefu wa uzalendo na kujisahau. Tanzania ni kubwa kuliko fedha au tija yoyote binafsi. Uwekezaji katika bandari ya Dar es salaam ni kwa maslahi ya umma na si vinginevyo.
Mageuzi yanayoleta tija kwa uchumi wa nchi yetu ni pamoja na kuvutia uwekezaji katika maeneo ya kimkakati kama vile Bandari. Kwa miaka zaidi ya thelathini Bandari yetu imekuwa ikiendeshwa na kampuni ya TICS na Charles Kitima hakuwahi kuhoji juu ya ufanisi hafifu lakini amepata ujasiri wa kueneza chuki dhidi ya serikali katika kipindi hiki muhimu, hili ni jambo la kushangaza na linatia aibu kwa kiongozi huyu anayejaribu kutumia Kanisa kuchafua serikali wazi wazi.